Mwanza. Polisi inawashikilia watu watatu kuhusiana na tukio la mauaji ya Imamu wa Msikiti wa Rahman, Feruz Ismail (27) na waumini wengine wawili, Mbwana Rajab (40) na Khamisi Mponda (28), waliouawa usiku wa kuamkia jana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema jana kuwa watu hao walikatwa sehemu mbalimbali za miili yao kwa kitu chenye ncha kali.
Katika tukio hilo, mtoto Ismail Abeid (13) alinusurika baada ya kupita kwenye mlango mwingine, tofauti na ule ambao wavamizi walielekeza utumike ambako walijeruhiwa kwa kukatwa na mapanga vichwani walipopita.
Ingawa Kamanda Msangi alisema polisi haijapata ushahidi wa kutosha kuhusisha tukio hilo na masuala ya kiimani au ugaidi, maelezo ya walionusurika katika tukio hilo yanaibua hofu ya wavamizi hao kusukumwa na imani ya kidini kutokana na ujumbe waliouandika kwenye kitambaa walichokuwa wamekishikilia kama bendera pamoja na kauli zao kwa waumini.
Mmoja wa watu walionusurika katika uvamizi huo, Abubakar Makabwe alisema: “Mmoja kati ya watu hao waliofunika nyuso zao alikuwa amebeba kitambaa cheusi mfano wa bendera kilichoandikwa kwa maandishi yanayosomeka ‘Islamic State’ yaliyokuwa yameandikwa kwa rangi nyeupe. Kabla ya kuanza kushambulia waumini kwa mapanga, watu hao walihoji kwa nini tunaswali huku wenzetu wanashikiliwa na polisi.”
Imeelezwa kuwa kabla ya kuanza kuwashambulia waumini kwa mapanga, wavamizi hao waliamuru watoto waliokuwamo msikitini humo kutoka nje kupitia mlango wa nyuma unaotumiwa na wanawake.
“Maswali na maelekezo yote yalikuwa yanatolewa na mtu ambaye kwa mujibu wa sauti yake, alikuwa ni mwanamke ambaye pia ndiye aliyeamuru imamu awe wa kwanza kuchinjwa,” alisema manusura mwingine, Ridhwan Abdallah.
Vikundi vya mazoezi ya karate
Kabla ya tukio la juzi, inadaiwa kuwa polisi walivamia na kuwatia mbaroni baadhi ya vijana waliokuwa wakiendesha mafunzo ya karate eneo la karibu na msikiti huo.
Akizungumzia kukamatwa kwa vijana hao, Kamanda Msangi alikiri polisi kuwashikilia watu kadhaa kwa mahojiano kuhusiana na matukio ya uhalifu.
“Siwezi kusema ni watu wangapi tunawashikilia kwa sababu bado tunaendelea na upelelezi. Lakini ni kweli tumewakamata watu kadhaa,” alisema.
Mwenyekiti wa mtaa huo, Jukaeli Kiula alisema alipata taarifa kutoka kwa mmoja wa waumini akidai kuna watu wamechinjwa msikitini. “...Tulikusanyika nikiwa na baadhi ya wananchi na kufika eneo la tukio, kweli tulikuta watu hao wamechinjwa ndipo nikapiga simu polisi na baada ya muda mfupi wakafika. Kuna mtoto mmoja simjui jina ila anakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 12 – 14, jana (juzi) hiyo, tukiwa hapa eneo la tukio polisi walimuuliza kuwa wewe ulikamatwa ukaachiwa halafu umekuja huku tena kufanya nini? hivyo na yeye waliondoka naye,” alisema Kiula.
Zena Ismail, mke wa marehemu Rajab, alisema mumewe alikwenda msikitini kusali saa mbili usiku, lakini baada ya muda alisikia watoto wakipiga kelele.
“Watoto walikuwa wakilia, tumevamiwa tumevamiwa, huku wakikimbia, baada ya hapo ndipo nilipata taarifa kuwa baba Mboni (mumewe) amekatwa mapanga na kufariki dunia,” alisema.
No comments:
Post a Comment