Wednesday, 20 April 2016

WAUGUZI WATUMIA DRIPU KUOSHA MIKONO- BAGAMOYO



WAUGUZI katika wodi ya wazazi Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo, mkoani Pwani, wanalazimika kuosha mikono kwa kutumia dripu, kutokana na kukosekana huduma ya maji hospitalini hapo.



Hali hiyo inatokana vyombo husika kuchelewesha ombi la hospitali hiyo la ununuzi wa tangi la kuhifadhia maji tangu Desemba, mwaka jana.
Kutokana na ukosefu huo wa maji na uhaba wa mashine za kufulia, mashuka na mazingira ya hospitali hiyo yamekuwa machafu.
Nipashe lilishuhudia baadhi ya mashuka yakiwa yameganda usaha na damu na kutoa harufu mbaya kwenye baadhi ya wodi kutokana na uchafu.
Hayo yalibainika mwishoni mwa wiki wakati wa ziara ya viongozi wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Bagamoyo, walipotembelea kujionea matatizo yaliyopo kwenye hospitali hiyo kwa ajili ya kuyatafutia ufumbuzi .


Mganga Mkuu Mfawidhi wa hospitali hiyo, Tumaini Bailon, alisema tatizo la maji linawapa wakati mgumu. Alisema tatizo hilo linasababisha mashuka kutofuliwa kwa wakati, huku wagonjwa na wauguzi nao wakikosa huduma hiyo kwa ajili ya shughuli mbalimbali za usafi na tiba.
Alisema kwasasa wanapata maji kwa mgao mara moja ama mara mbili kwa mwezi, huku tanki la maji linalotumika likiwa ni moja ambalo huwekewa maji baridi kwa ajili ya kufulia.
Dk. Bailon alisema awali yalikuwapo matanki mawili, lakini kwa sasa lipo moja la lita 5,000 tu baada ya jingine kuharibika na wamepeleka taarifa Halmashauri ya Bagamoyo , lakini tatizo linaonekana ni idara ya manunuzi ambayo inachelewa kufanya manuzuzi hayo.
Alitaja matatizo mengine yanayoikabili hospitali hiyo kuwa ni, uhaba wa majengo na vyumba vya waganga wanaohudumia wagonjwa wa kawaida ambavyo vipo vinne na mahitaji ni vyumba saba ili kukidhi mahitaji.
Changamoto nyingine alisema ni ukosefu wa umeme, dawa na vyandarua, upungufu wa watumishi 100 wakati mahitaji ni zaidi ya 250.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Bagamoyo, Abdulzahoro Sharif, alitoa wiki moja kwa idara ya manunuzi kushughulikia ombi la tanki la maji na endapo wakishjindwa kufanya hivyo jumuiya italinunua.
Alisema ni bora kununua tanki la maji kuliko baadhi ya wauguzi kutumia dripu ambazo ni ghali na zipo kwa ajili ya kusaidia wagonjwa.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!