Saturday, 23 April 2016

Wauguzi wampa mume glovu amzalishe mkewe




Dar es Salaam. Wakati wafanyakazi wa Hospitali ya Temeke wakihaha kuwasilisha vyeti wakati wa ukaguzi wa watumishi hewa hospitalini hapo, wauguzi wawili wa zahanati ya Kijiji cha Uzia mkoani Rukwa wamesimamishwa kazi kwa tuhuma za kumtelekeza mjamzito na kumpa mumewe glovu amzalishe na kusababisha kifo cha mtoto.


Mwanamke huyo, ambaye jina lake halijapatikana, alipelekwa na mumewe kwenye zahanati hiyo usiku baada ya kupatwa uchungu, lakini alipofika wauguzi hao waliona kuwa anachelewa kujifungua.
“Waliamua kumuita mumewe na kumvisha gloves (mipira ya kujikinga), kisha wakaondoka,” alisema mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga, Kalolo Joseph Ntila na kuongeza: “Usiku mzima mume alifanya kazi ya kuhangaika na mke wake na waliporudi asubuhi, wakakuta mama anajifungua, mtoto akiwa amechoka na akafariki dunia. “Kwa hiyo tumeunda kamati wakati wao wakiwa nje kwa muda kupisha uchunguzi na ikibainika wana makosa tutawachukulia hatua zaidi.”
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo hakuweza kukumbuka jina la mjamzito huyo na mumewe na juhudi za kuwapata wawili hao hazikuzaa matunda.
Katika tukio jingine; halmashauri hiyo imewasimamisha kazi wauguzi na madaktari wasaidizi wa zahanati za vijiji vya Uzia, Muze na Mpui kwa tuhuma za uzembe na kusababisha vifo ya wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano.
Awali, mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo, Adam Missana alisema watumishi wengine wanne wamefukuzwa kazi wakiwamo mafundi, wahudumu wa maabara, wauguzi na wahudumu wa afya kutokana na utoro kazini.
Taharuki Hospitali ya Temeke
Hali ya sintofahamu jana asubuhi iliikumba Hospitali ya Temeke baada ya wakaguzi kufika kufanya uhakiki wa watumishi hospitalini hapo na kusababisha wagonjwa kutelekezwa kutokana na wauguzi kufuata vyeti majumbani mwao.
Maeneo yaliyoathirika na purukushani hiyo ni pamoja na upande wa huduma kwa wazee, wajawazito, wagonjwa wa kawaida na katika baadhi ya wodi.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliagiza wakuu wa wilaya zake kuacha masuala mengine na kujikita kwenye ukaguzi wa watumishi hewa kwenye sekta zote.
Mgonjwa aliyekutwa hospitalini hapo, Monica Kessy alisema daktari aliyekuwa akiwahudumia aliondoka, hivyo kuwalazimu wagonjwa kupanga foleni kwa daktari mmoja pekee. “Ilipofika saa 5:00 hivi tukaona wanatoka na kukaa vikundi vikundi wakielezea kuna uhakiki. Wengine wakaanza kuondoka. Baadaye tukasikia tangazo kuhusu uhakiki, manesi na madaktari wengi wakaondoka,” alisema Monica.
“Usipowasilisha vyeti utaonekana wewe mtumishi hewa, hivyo katika kuliepuka hilo kila mmoja anatetea ugali wake. Masjala hatuwezi kutosha mule, wengine tukarudi majumbani mwetu kuchukua vyeti,” alisema mmoja wa wauguzi ambaye hakupenda kutaja jina.
Mganga mkuu wa hospitali hiyo, Dk Amani Malima alisema hitilafu hiyo imetokana na uhakiki wa watumishi ambao unaendelea kufanyika hospitalini hapo.
“Huduma zinaendelea si kusema kwamba imesimama. Watumishi walitangaziwa tangu jana kutakuwa na uhakiki mwingine. Kazi lazima iendelee,” alisema.

MWANANCHI

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!