Saturday, 23 April 2016

MAHAKAMA YA MAFISADI KUANZA JULAI


ULE msemo wa Kiswahili usemao hayawi hayawi sasa yamekuwa umetimia baada ya kutangazwa kuwa Mahakama Maalum ya Mafisadi iliyoahidiwa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na Rais John Magufuli itaanza kazi Julai.



Tamko la kuanza kazi kwa Mahakama hiyo lilitolewa jana bungeni na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi yake.
“Kuhusu ahadi ya kuanzisha Mahakama Maalum ya Ufisadi napenda kuliarifu Bunge lako kwamba, Serikali imeanzisha Divisheni ya Mahakama ya Rushwa na Ufisadi katika Mahakama Kuu itakayoanza kufanya kazi mwezi Julai 2016,” alisema Majaliwa.
Aidha, Waziri Mkuu alisema pia Serikali itaimarisha Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kwa pamoja ziweze kuharakisha utoaji wa haki kwa kesi zitakazofikishwa kwenye mahakama hiyo.
Kiongozi huyo wa serikali aliongeza: "Serikali itaimarisha ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kwa pamoja ziweze kuharakisha utoaji wa haki."
Rais Magufuli alitoa ahadi ya kuanzisha mahakama hiyo kwenye mikoa kadhaa aliyopita kwa ajili ya kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Aidha, katika siku ya kilele cha Wiki ya Mwaka Mpya wa Mahakama Jijini Dar es salaam mapema mwaka huu, Rais Magufuli alimtaka Jaji Mkuu, Othman Chande kutosubiri Bunge kupitisha Sheria ya Uanzishwaji wa Mahakama ya Mafasidi, badala yake mahakama hiyo ianze kufanya kazi haraka iwezekanavyo.
Alisema kuchelewesha kuanza kwa mahakama hiyo kunatoa mwanya kwa mafisadi kuendelea kuangamiza nchi na kuifanya kuwa masikini wakati ina rasilimali za kutosha ambazo zinaweza kuiendesha nchi bila kutegemea fedha za wafadhili.
Rais Magufuli alisisitiza umuhimu wa uanzishwaji wa mahakama hiyo ambayo alitaka ifanye kazi ndani ya mahakama kuu kama zilivyo Mahakama za Ardhi na Biashara.
Akifunga maadhimisho hayo, Rais Magufuli alisema azma yake ni kuona nchi inakuwa na uchumi mzuri ambao utamnufaisha kila mtanzania na rasilimali zilizopo badala ya kumilikiwa na watu wachache.
SH. BILIONI 12.3
Akizungumza Bungeni jana, Majaliwa alisema katika jitihada za kukabiliana na changamoto ya uhaba wa majengo ya mahakama na vitendea kazi katika ngazi zote, Rais Magufuli ametekeleza ahadi yake aliyoitoa Februari 4, mwaka huu ya kutoa fedha za maendeleo ya mahakama Sh. bilioni 12.3.
Alisema hatua hiyo imewezesha mahakama kuendelea na ukarabati na ujenzi wa mahakama katika ngazi mbalimbali pamoja na ununuzi wa vitendea kazi.
Majaliwa alisema serikali imedhamiria kupunguza kero ya mlundikano wa mashauri mahakamani ili wananchi wapate haki kwa wakati.
Katika kufanikisha dhamira hiyo, Waziri Mkuu alisema serikali imeimarisha utendaji wa mhimili wa mahakama kwa kuongeza rasilimali watu na fedha.
"Serikali pia imeboresha na kuongeza ufanisi katika upelelezi na uendeshaji wa mashauri kwa kutenganisha jukumu la upelelezi na uendeshaji mashuari,” alisema Majaliwa.
Uongozi wa mahakama, alisema zaidi Majaliwa, umejiwekea utaratibu wa majaji na mahakimu kuwa na malengo ya idadi ya mashauri ambayo wanapaswa kuyasikiliza kila mwaka.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!