Thursday, 7 April 2016

WATOTO WA KIKE 20,000 KUNUFAIKA NA MFUKO WA GRACA MACHEL MKOANI MARA.

????????????????????????????????????
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. George Simbachawene (kulia) akiongea na Mama Graca Machel (kushoto) alipomtembelea ofisini kwake leo jijini Dar es salaam.


sim2
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. George Simbachawene (kulia) akiagana na Mama Graca Machel (kushoto) mara baada ya mazungumzo ofisini kwake leo jijini Dar es salaam.
(Picha na Eleuteri Mangi-MAELEZO)
……………………………………………………………………
Na Eleuteri Mangi-MAELEZO
Watoto wa kike 20,000 kutoka mkoa wa Mara watanufaika kwa fursa ya kupata elimu kupitia Mfuko wa Graca Machel (Graca Machel Trust) ambao umejikita katika kusaidia wanawake na watoto nchi kadhaa za Afrika.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. George Simbachawene mara baada ya mazungumzo na Mama Graca Machel alipomtembelea ofisini kwake leo jijini Dar es
salaam.
 “Ni fursa nzuri ya kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi kuwasaidia watoto wetu wa kike kielimu ambayo itawasaidia kutoka katika jamii ya umasikini na kuhakikisha wamepata fursa ya kuvuka umri wa vishawishi na maamuzi yasiyo sahihi” alisema Waziri Simbachawene.
Watoto hao watakaonufaika na Mfuko huo mkoani Mara watatoka katika shule 104 ambapo inatarajiwa kuwafikia watoto wa kike wengi zaidi mara baada kuanza kutoa huduma hiyo mkoani humo.
Waziri Simbachawene amesema kuwa Mama Graca Machel amechagua kuja katika Tanzania kutokana ushirikiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Msumbiji kwa kuzingatia mchango mkubwa wa Tanzania kwa nchi hiyo.
\
Aidha, Waziri Simbachawene amemshukuru Mama Graca Machel kwa kujali na kuuchagua mkoa wa Mara ambao ndio mkoa alipozaliwa Mwasisi wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Kwa upande wake Mama Graca Machel amemshukuru Waziri Simbachawene kwa mapokezi na ushirikiano alioupata katika Serikali ya Awamu Tano iliyopo madarakani na kuahidi kuendelea kusirikiana nao ambapo anaamini mpango wa kuwasaidia watoto wa kike kupita taasisi yake utapanuka na hatimaye kuweza kuwafikia watoto wa kike wengi zaidi kupitia mikoa yote nchini.
“Lengo ni kuwabakisha watoto wa kike shuleni ili wapate elimu, ni lazima tusaidiane wote, tuna kila sababu ya kusaidiana” alisema Mama Graca Machel.
Uhusiano wa Tanzania na Msumbiji ni wa kihistoria kwani wananchi wa nchi hizo walishirikiana katika shughuli mbalimbali chini ya mwavuli wa unasaba na ushirikiano katika biashara na tamaduni kwenye miji ya Unguja, Kilwa, Lindi na Mtwara kwa upande wa Tanzania na katika miji ya Chilimbo, Tete, Pemba na Sofala nchini Msumbiji.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!