Friday, 1 April 2016

MKE WA MTUHUMIWA KESI YA TUMBILI AFARIKI DUNIA


WAKATI watuhumiwa wa kesi ya kukutwa na tumbili 61 wakiwa bado rumande kwa zaidi ya wiki sasa, mke wa mtuhumiwa mmojawapo raia wa Uholanzi, Arten Vardanian, Mariam, amefariki dunia juzi kwa mshtuko baada ya kusikia mumewe amekamatwa kwa tuhuma hizo.


Mke huyo alifariki juzi katika Hospitali ya Staint Grigor Lusavarich Medical Center katika Jamhuri ya Armenia akiwa katika chumba cha uangalizi maalumu (ICU). Taarifa ya kifo iliyotolewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma ya Dharura katika hospitali hiyo, Gagik Manukyan, ambayo nakala yake gazeti hili linayo, ilithibitisha kifo hicho na sababu kuwa mshtuko.
Hata hivyo ilieleza kuwa Mariam alifikishwa hospitalini hapo akiwa na hali mbaya na ilizidi, baada ya mshtuko wa taarifa kuhusu mumewe na alifariki juzi Machi 30, mwaka huu saa 8:45 alasiri majira ya Armenia.
Taarifa hiyo ilisema Mariam alifikishwa hospitalini hapo Machi 9, mwaka huu, akiwa katika hali isiyo nzuri akiumwa ugonjwa ambao hawakuubainisha na ilieleza kuwa juzi baada ya kusikia kukamatwa kwa mumewe akituhumiwa kusafirisha tumbili, alipata mshtuko na kufa.
Wakili anayewatetea watuhumiwa hao wa Kampuni ya Stratton and Company Advocates ya jijini Arusha, Kisaka Mzava, alithibitisha pia suala hilo. Wakili Mzava aliwataja watuhumiwa anaowatetea kuwa ni Arten Vardanian (53), raia wa Uholanzi na Edward Vardanian (44), raia wa Russia na kwamba ni ndugu.
Watuhumiwa hao pamoja na wengine akiwemo Ofisa Mfawidhi Kanda ya Kaskazini anayehusika na matumizi endelevu ya wanyamapori nchini, (CITES), Nyangabo Musika, Idd Misanya anayetuhumiwa kuuza wanyama hao na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Wanyamapori wa Matumizi Endelevu, Dk Charles Mulokozi na Mkurugenzi wa Manyara Bird, Juma Eliasa nao wanashikiliwa.
Tangu kukamatwa kwa watuhumiwa hao Machi 24, mwaka huu saa 1 usiku Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), na kuchukuliwa maelezo siku tatu baadaye katika kituo cha Polisi uwanjani hapo, watuhumiwa hao bado hawajafikishwa mahakamani mpaka jana.
Wakili anayewatetea, alisema tumbili wanaodaiwa kukamatwa, sio wa wateja wake, isipokuwa ni wa mfanyabiashara mmoja, Artur Khatcharyan, raia wa Armeria anayemili kampuni ya Zoo Fauna Art. LLC ya nchini humo. Idadi ya watu waliokamatwa hadi jana kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Wilbroad Mtafungwa, ni saba.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!