Saturday 26 March 2016

WAZUNGU WA TUMBILI KIZIMBANI JUMANNE

 
Raia wawili wa Uholanzi wanaoshikiliwa na Kikosi cha Kupambana na Ujangili tawi la Uwanja wa Ndege wa Kia kwa tuhuma za kujaribu kusafirisha tumbili 61, watafikishwa mahakamani Jumanne.
 
Taarifa za uhakika zilizothibitishwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe zinaeleza kuwa, Waholanzi hao watapandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi Jumanne.
 
“Tayari nimeshaagiza maofisa wa idara ya wanyamapori ambao wamekabidhiwa jukumu la kuwalinda tumbili hao, wahakikishe wanalishwa vizuri, hadi watuhumiwa watakapopelekwa mahakamani Jumanne ijayo, mjini Moshi,” alisema Waziri Maghembe.
 
Hata hivyo, Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Kamishna Msaidizi, Wilbrod Mtafungwa alisema hana uhakika kama wazungu hao watafikishwa kweli katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi siku hiyo.
 
“Bado uchunguzi ni mbichi," alisema Mtafungwa "kwa sababu tunachunguza mwenendo mzima chini ya task force (kikosi kazi)."
Alisema kikosi kazi hicho kinashirikisha wachunguzi kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Kikosi cha Kupambana na Ujangili, Idara ya Wanyamapori, Uhamiaji na Usalama wa Taifa.
 
“Unajua hili suala ni nyeti, na lina maslahi mapana kwa taifa, kwa hiyo siwezi kusema chochote kwa sasa, isipokuwa hatujakamata watu wengine kuhusiana na tuhuma hizo za utoroshaji wa wanyama hai kwenda ughaibuni.”
 
Waholanzi hao Artem Alik Varbanyian (52), ambaye ni Mkurugenzi wa Mgahawa mmoja nchini humo na Edward Alik Varbanyian (44), Meneja wa Hoteli nchini Uholanzi, walikamatwa Jumatano saa 1:30 usiku katika uwanja wa ndege wa Kia, uliopo Wilaya ya Hai.
 
Ndugu hao wa familia moja, walikuwa wakitaka kuwasafirisha tumbili hao kwenda Ulaya Mashariki, kinyume cha sheria za nchi, kwa kutumia Ndege ya Shirika la Afrika ya Kusini.
 
Haijafahamika wanyama hao waliwindwa na kukamatwa katika eneo gani la hifadhi za taifa au mapori tengefu, ama maeneo ya kilimo yenye idadi kubwa ya tumbili.
 
Desemba 18, mwaka jana, kikosi hicho pia kilimtia nguvuni mlinzi wa mfalme wa Qatar, Jasim Mbarakke Alhkubaisi (43), kwa tuhuma za kusafirisha fuvu la twiga kwenda uarabuni.
 
Wakati mlinzi huyo akiwa mikononi mwa dola, wiki moja iliyotangulia alikamatwa raia mwingine wa Vietnam, Hoang Nghia Trung (49), akiwa na kucha 261 na meno 60 ya simba.
 
Matukio hayo ya kutorosha wanyama hai yanazidi kushamiri, huku taifa likiwa bado halijasahau tukio la Novemba 26, mwaka 2010 la kusafirishwa kwa wanyama hai 152, wakiwamo twiga kwenda Falme za Kiarabu, kupitia uwanja wa Kia.
 
Raia wa kigeni, Ahmed Kamran, mtuhumiwa wa utoroshaji wa wanyama hao kwa mwaka 2010, hajapatikana hadi sasa, licha ya kushtakiwa na kuhukumiwa kifungo cha miaka 60 jela, Desemba 5, mwaka 2014.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!