Friday, 18 March 2016

UAMUZI WA MWAPACHU WAZUA MJADALA MZITO


Siku moja baada ya msomi na mwanadiplomasia maarufu nchini, Balozi Juma Mwapachu, kutangaza kurudi Chama Cha Mapinduzi (CCM), makundi mbalimbali ya jamii wakiwamo wasomi, wanasiasa na wachambuzi wa masuala ya siasa wametoa maoni yao kuhusiana na hatua hiyo.

Balozi Mwapachu alitangaza kujiengua CCM Oktoba 13, mwaka jana, kwa maelezo kuwa chama hicho kimepoteza misingi ya demokrasia kutokana na kutomteua Edward Lowassa kuwania urais kupitia chama hicho.
Hata hivyo, Balozi Mwapachu juzi alitangaza kurejea CCM, akisema  amechukua hatua hiyo baada ya kutafakari kwa kina.
Profesa wa sheria, ambaye pia Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, Prof. Abdallah Safari, alisema hatua ya Balozi Mwapachu kurudi CCM inaonyesha kuwa hakutafakari kwa kina kabla ya kuondoka.
 “Mfano mimi nilipofikiria kuondoka Chama Cha Wananchi (CUF), nilitafakari kwa kina ndiyo maana hadi leo sifikirii kurudi tena CUF,” alisema.
Prof. Safari alisema wakati Balozi Mwapachu anahama CCM, alidhani Lowassa angeshinda urais ili apate fursa ya uongozi, lakini alipoona upinzani umeshindwa, ameamua kurudi ili kuangalia fursa nyingine CCM.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Bashiru Ally, alisema  hatua ya Mwapachu kurudi CCM ni haki yake ya msingi.
Alisema ni hiari ya mtu kuamua kujiunga au kuondoka ndani ya chama chochote na kujiunga na kingine.
“Siwezi kumtolea maoni hili ni jambo la hiari ya mtu,” alisema.
Richard Hiza, maarufu kama Tambwe,  ambaye aliwahi kuwa Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Propaganda cha CCM, alisema Balozi Mwapachu hakuwahi kujiunga na chama chochote cha upinzani nchini, baada ya kuondoka chama tawala, hivyo alichokifanya ni kumaliza likizo yake ya muda mfupi na kurejea.
Tambwe ambaye pia alishawahi kuwa kiongozi katika vyama vya NCCR-Mageuzi na CUFf na CCM kabla ya kujiunga na Chadema, alisema Mwapachu hataongeza chochote ndani ya CCM wala kupunguza jambo kwani hana ushawishi wa kisiasa.
Alisema: “Mwapachu si maarufu hata kwenye chama chake, hakuwahi kufanya jambo ambalo watamkumbuka.”
Kuhusu msimamo wake kama anaweza kurudi CCM, alisema hana mpango huo kwa kuwa hakuna jambo jipya ambalo halifahamu kutoka CCM linaloweza kumrudisha huko.
Mwenyekiti wa zamani wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, ambaye aliihama CCM na kujiunga na Chadema mwaka jana kumfuata Lowassa, alisema sababu zilizomwondoa Balozi Mwapachu CCM ndizo zinazomrudisha, hivyo ni haki yake kufanya hivyo.
Mgeja alisema: “Sioni cha ajabu sana kwa sababu ni hali ya kawaida.”
Kuhusu msimamo wake kama ataendelea kubaki Chadema, alisema jambo hilo hawezi kulizungumzia na kwamba kwa sasa anafanya shughuli zake binafsi.
“Haiwezekani kila wakati tuwe kwenye siasa tu, nina shughuli zangu binafsi nafanya, lakini sijastaafu siasa,” alisema Mgeja.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!