Friday, 18 March 2016

KULALAMIKA HAKUTAMALIZA UMASKINI WETU-IRENE KIWIA



Imekuwa desturi kwa Watanzania hususan vijana kulalamikia ugumu wa maisha, ilhali wengi wao kutojaribu kujikwamua kukabiliana na hali hiyo.



Kinyume chake wengi wamekuwa wakikaa kwenye vijiwe na vikundi wakiendelea kutupia lawama Serikali na kusahau jukumu lao, wakiamini kuwa inachangia kwa kiasi kikubwa kuwaweka kwenye umaskini.
Mawazo hayo yanapingwa na Irene Kiwia, mjasiriamali na mwanaharakati aliyejikita katika kuelimisha jamii kuhusiana na haki za wanawake.
Kiwia anasema ili kukabiliana na changamoto ya umaskini inawalazimu vijana kutafuta njia sahihi ya kujiondoa kwenye hali hiyo kwa kufanya kazi.
“Hakuna mafanikio yanayoweza kupatikana kwa kulalamika, lazima ziwepo jitihada binafsi ili kujiondoa kwenye umaskini.
Ifike wakati vijana tuweke visingizio pembeni na kuangalia fursa lukuki zilizopo nchini na kuzitumia ipasavyo. Hatuwezi kuwa na matokeo mazuri kama mambo yanafanyika vilevile kila siku,” anasema Kiwia.
Anasema ni muhimu kwa kijana kujitafakari na kutambua uwezo wake, na namna ambavyo anaweza kufanya ili kuleta matokeo chanya.
Anasema hiyo haimaanishi kusubiri kuajiriwa kwa kuwa ndani ya jamii kuna fursa kadha wa kadha, ambazo vijana wanaweza kuanza kwa kujitolea na baadaye zikawa na mafanikio kwao.
Kiwia anasisitiza pia mfumo wa elimu unapaswa kuwaandaa vijana kujiajiri na kukizi vigezo vya ajira, siyo kuwakaririsha ili waweze kujibu mitihani.
“Binafsi naona kuna haja ya kuutupia jicho mfumo mzima wa elimu, kwa kiasi fulani unachangia kuzalisha wasomi wengi wasio na vigezo vya kufanya kazi, ndiyo maana tatizo la ukosefu wa ajira linaonekana kuwa kubwa.
Ifike wakati mhitimu wa ngazi fulani ya elimu awe na uwezo wa kufanyia kazi kitu alichosomea, ili iwe rahisi hata kukidhi vigezo inapotokea nafasi za ajira.
Sambamba na hilo mhitimu aliyeiva vizuri kwenye fani yake itamuwezesha kubuni njia mbadala za kujipatia kipato pasi na kutegemea kuajiriwa.
Alianzaje masuala ya harakati
Nilipohitimu shahada ya kwanza nilipata nafasi ya kuzunguka maeneo mbalimbali nchini, ndipo nilipokutana na wasichana wengi ambao hawakufanikiwa kupata fursa ya elimu kama niliyokuwa nayo.
“Niligundua kuwa wanakabiliwa na changamoto lukuki, nikaona wazi kupitia bahati niliyopata nina kila sababu ya kusaidia wengine,” anasema.
Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa kushirikiana na washirika wenzake, walianza kutoa elimu ya ukombozi wa fikra kwa wanawake na wasichana ili waweze kutambua nguvu yao.
“Tulifanya jitihada mbalimbali, mojawapo ikiwamo shindano la Kisura ambalo lilijulikana na Watanzania wengi, ila kwa kifupi tulifanya shughuli nyingi mpaka kufikia uanzishaji wa tuzo za wanawake wenye mafanikio,” anaeleza Kiwia.
....katika ujasiriamali
Kiwia ambaye ni mama wa watoto watatu, anamiliki kampuni inayojihusisha na masuala ya habari na matangazo inayofahamika kama Frontline Porter Novelli. Kupitia kampuni hiyo Kiwia ameingia kwenye kundi la wajasiriamali wakubwa na kufanikiwa kutoa ajira kwa vijana wengine kadhaa.
Anasema kampuni hiyo imemuwezesha kujiajiri na kumpa fursa ya kujipangia namna ya kuendesha maisha yake, sambamba na kukuza uchumi wa familia.
“Namshukuru Mungu nimeajiri na kutoa ajira kwa watu wengine, hilo linanifanya kuongeza ubunifu katika kazi ili kampuni yangu iendelee kuwapo na uchumi kwenye familia zetu kukua,” anasema.
Maisha yake na familia
Anaeleza kuwa kujiajiri ni fursa ya aina yake inayomuwezesha kupata muda mwingi wa kuwa na familia.
“Ni furaha ya aina yake kuwa mama asikwambie mtu, pamoja na shughuli nyingi nilizonazo nafanya kila ninaloweza kushiriki kwenye malezi ya watoto wangu. Kupenda watoto nilianza tangu nikiwa mdogo hivyo nilisubiri kwa muda mrefu kuwa mama na wakati ulivyofika nilipokea zawadi hiyo kwa mikono miwili,” anaeleza.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!