RAIS Mteule wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein anaapishwa leo kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa. Kuapishwa kwa Dk Shein kunamfanya apate fursa nyingine ya kuongoza Zanzibar kwa muda wa miaka mitano ijayo, baada ya mgombea huyo wa CCM kushinda urais wa Jumapili kwa kujinyakulia asilimia 91 ya kura zilizopigwa.
Serikali pia imetangaza kuwa leo pia ni siku ya mapumziko visiwani hapa ili kuwapa fursa wananchi wahudhurie sherehe za kuapishwa kwa kiongozi wao. Wageni ambao wanatarajia kuhudhuria kwenye sherehe hizo ambazo zitaanza saa 2 asubuhi ni Rais John Magufuli na viongozi wengine wa ngazi ya juu wa kitaifa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud alithibitisha kuwepo kwa viongozi hao akiwemo Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na mawaziri wa Serikali ya Muungano katika shughuli ya kuapa kwa Rais mteule Dk Shein.
Wakati Rais anaapishwa leo, amani na utulivu bado ni mkubwa visiwani hapa licha ya kuwa ulinzi umeendelea kuimarishwa katika maeneo mbalimbali nyeti na mitaani. Baadhi ya shughuli za kiuchumi kama maduka yameanza kufunguliwa jana, hali inaonesha kuwa utulivu upo wa kutosha kama ambavyo Serikal iliahidi kuwa itahakikisha amani inakuwepo visiwani hapa.
Dk Shein wa CCM anaenda kuongoza katika miaka mitano ijayo katikati ya mpasuko wa kisiasa uliopo visiwani hapa kutokana na Chama cha Wananchi (CUF) ambacho ni chama kikuu cha upinzani kususa kushiriki kwenye uchaguzi wa marudio ambao ulifanyika Jumapili iliyopita.
Tayari CUF wameshatangaza kuwa hawautambui ushindi huo wa Dk Shein kwa kile wanachoeleza kuwa umetokana na uchaguzi haramu baada ya demokrasia kubakwa kwani wananchi wa Zanzibar walishaamua kwenye uchaguzi wa Oktoba 25, 2015.
Chama hicho kimeahidi kuendelea kudai haki yake kwa amani na kimewataka wananchi kuendelea kuitunza amani iliyopo na watakuwa wanapatiwa taarifa za hatua itakayofikia chama hicho katika harakati za kudai haki. Kwa ujumla wananchi wa Zanzibar kuanzia juzi wanaonekana wamoja na kwa kuwa ulinzi uliopo unawakataza kukaa kwenye makundi.
No comments:
Post a Comment