Saturday, 19 March 2016

MENO YA TEMBO YAWAFUNGA WACHINA 53


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imewahukumu raia wawili wa China kulipa faini ya Sh. Bilioni 108.1 ama kwenda jela miaka 35 baada ya kukutwa na hatia ya makosa mawili ya kukutwa na karibu tani 2 za meno ya tembo na kuwashawishi maofisa wa serikali kupokea rushwa.
 
Washtakiwa hao ni Huang Gin na Yu Fujie.
Hukumu hiyo ilisomwa jana na Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Cyprian Mkeha aliyesikiliza kesi hiyo.
 
Hakimu alisema baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi tisa wa upande wa Jamhuri bila kuacha shaka mahakama imewaona washtakiwa wana hatia dhidi ya makosa mawili.
 
Alisema  upande wa Jamhuri bila kuacha shaka umeithibitishia mahakama tuhuma za kukutwa na nyara za serikali, vipande 728 vya meno ya tembo vilivyokuwa na uzito wa kilo 1,889 yenye thamani ya Sh. Bilion 5.4.
Pia, mahakama imemkuta na hatia katika shtaka la tatu la kuwashawishi maofisa wa maliasili na jeshi la polisi kupokea rushwa ya Sh. Milioni 30.2 ili wasiwafanyie upekuzi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria.
 
Hakimu alisema ushahidi wa Jamhuri ulithibitisha kukamatwa kwa nyara hizo zilizokuwa zimefungwa kama mizigo wa kuni na kuhifadhiwa kwenye mifuko ya salfeti.
 
“Baada ya kuwatia washtakiwa hatiani, mahakama yangu inawahukumu kulipa faini ya Sh. Bilioni 54 ama kwenda jela miaka 30 kila mshtakiwa kwa kosa la kukutwa na nyara za serikali, faini ya Sh. Milioni Moja ama kwenda jela miaka mitano kwa kosa la pili… pia mahakama hii inawaachia huru washtakiwa kwa kosa la pili la kukutwa na ganda la risasi kinyume cha sheria,” alisema Hakimu Mkeha.
 
Kabla ya hukumu hiyo kusomwa upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, akisaidiana na Mawakili wa Serikali Paul Kadushi na Simon Wankyo ulipewa nafasi ya kutoa hoja kuhusu adhabu itakayotolewa kwa washtakiwa.
 
Nchimbi alidai kuwa kutokana na wimbi la kuuawa tembo kuongezeka kwa kasi kati ya mwaka 2010 na 2014 ni wazi kuwa washtakiwa ni majangili wazoefu na wamekamatwa na shehena kubwa kuliko watuhumiwa wengine wote waliokamatwa na nyara hizo, mahakama itoe adhabu kali.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!