Wednesday 16 March 2016

Mattaka wa ATCL kizimbani


ALIYEKUWA Mkurugenzi wa Shirika la Ndege (ATCL) David Mattaka, na wenzake wawili, wamepandishwa kizimbani wakikabiliwa na mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 86.5.


Mattaka anadaiwa kusababisha hasara hiyo kutokana na kusaini mkataba wa kukodi ndege bila kufuata Sheria ya manunuzi ya umma pamoja na ushauri wa kiufundi. Mbali na Mattaka washtakiwa wengine waliofikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) Ramadhani Mlinga pamoja na Mkurugenzi wa Sheria wa mamlaka hiyo, Bertha Soka.
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani jana na kusomewa mashitaka sita na Wakili wa Serikali Mkuu, Vitalis Timony pamoja na mawakili kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Peter Vitalis na Stanley Luoga mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Respicius Mwijage.
Wakili Timony alidai kuwa, Oktoba 9, 2007 katika ofisi za ATCL Dar es Salaam, Mattaka akiwa Mkurugenzi wa shirika hilo, alitumia madaraka yake vibaya kwa kusaini makubaliano ya kukodi ndege yenye namba A 320-214, kati ya ATCL na kampuni ya Wallis Trading Inc, bila kufuata sheria ya manunuzi ya umma na taratibu za zabuni.
Aliendelea kudai kuwa, Oktoba 27, 2007, Mattaka alitumia madaraka vibaya kwa kusaini makubaliano ya kukodi ndege hiyo bila kufuata ushauri wa kiufundi. Katika mashitaka mengine, inadaiwa kati ya Oktoba 27, 2007 na Aprili 24, 2008, Mattaka alisaini makubaliano hayo bila kufuata ushauri wa kiufundi jambo ambalo lilisababisha shirika hilo kupata hasara ya dola za Kimarekani 772,402.08 ambazo zililipwa kwa kampuni ya Aeromantenimiento kama gharama ya matengenezo ya ndege hiyo.
Aidha inadaiwa kati ya Oktoba 27 na Novemba 29, 2007, Mattaka aliidhinisha makubaliano hayo bila kufuata ushauri wa kiufundi na kusababisha hasara ya dola za kimarekani 35,984.82, ambazo zililipwa kwa kampuni ya Lantal textiles kwa ajili ya kununua vifaa mbalimbali vya ndege hiyo.
Wakili Timony aliendelea kudai, kati ya Oktoba 27, 2007 na Oktoba 26, 2011, kwa kutumia madaraka yake vibaya, Mattaka aliidhinisha makubaliano hayo na kuisababishia serikali hasara ya dola za Kimarekani 42,459,316 ambazo ATCL iliilipa kampuni ya Wallis Trading Inc.
Katika mashtaka yanayowakabili, Mlinga na Soka, inadaiwa Machi 19, 2008, katika ofisi za PPRA, Ilala Dar es Salaam, kwa lengo la kufanya udanganyifu, walighushi muhtasari wa kikao cha Machi 19, 2008, kwa lengo la kuonesha siku hiyo, PPRA ilifanya kikao kujadili maombi ya kuruhusu makubaliano ya ATCL kukodi ndege.
Baada ya kusomewa mashitaka, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu mashtaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu. Wakili Timony alidai upelelezi wa kesi bado unaendelea, pia hawana pingamizi la dhamana kwa Mlinga na Soka kwa kuwa shitaka linalowakabili lina dhamana.
Hata hivyo alidai wanapinga dhamana ya Mattaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa dhamana kwa mashtaka ya Uhujumu Uchumi pia mashitaka yanayomkabili yanahusisha zaidi ya Sh bilioni 10, hivyo alishauri awasilishe maombi ya dhamana katika Mahakama Kuu.
Mlinga na Soka waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na mdhamini mmoja alisaini hati ya Sh milioni 10, Mattaka alirudishwa rumande. Hakimu Mwijage aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 29 mwaka huu itakapotajwa tena.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!