Thursday, 24 March 2016

MAKONDA AZISHUKIA GEREJI, NA GROSARI BUBU


Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, amesisitiza kuwa ataendeleza azma yake ya kuondoa gereji za mitaani, baa na grosari, ikiwa mpango wake wa kusafisha jiji.
 
Makonda aliyasema hayo alipokuwa akikabidhiwa ofisi na aliyekuwa mkuu wa mkoa huo, Saidi Meck Sadiki, ambaye amehamishiwa mkoani Kilimanjaro.
 
Mbali na gereji na baa, pia alisema atahakikisha anaondoa yadi za magari ambazo zimezagaa kila kona ya jiji na kuzihamishia maeneo maalum. 
 
“Uchafu unaanzia moyoni mwako, nawaomba wananchi kila mmoja asafishe maeneo yao,” alisema. 
 
Aidha, aliwataka viongozi wa serikali za mtaa wampatie idadi ya wananchi wanaoishi maeneo yao ili kuimarisha ulinzi. 
 
“Nashukuru Rais John Magufuli kwa kunichagua kufanya naye kazi. Namshukuru baba yangu Meck Sadiki, leo ni siku iliyofungua ukurasa mpya ambao sikuwahi kuusoma,” alisema.
 
Sadiki kwa upande wake, alifunguka kwa kusema moja ya changamoto alizokumbana nazo wakati akiwa Dar es Salaam, ni vuguvugu la uchaguzi mkuu la mwaka 2010.
 
Uchaguzi huo ulihusisha wagombea wa vyama vyote wakiwemo Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete wa CCM na Dk. Willibrod Slaa wa Chadema.
 
Sadiki ambaye sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika sherehe ya kuagwa, iliyohusisha viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo.
 
Aidha, aliwaomba viongozi wa dini wamuunge mkono Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, katika kampeni ya ‘Safisha Jiji Ondoa Uchafu’.
 
“Wananchi wa Dar es Salaam ndio wamenifikisha hapa nilipo  hadi  Rais (Dk. John) Magufuli alipoamua kunipeleka Kilimanjaro kwenda kuendeleza mazuri niliyoyafanya hapa,” alisema.
 
“Nakuombea Makonda ufanye kazi pamoja na kamati ya viongozi wa dini uwashirikishe katika changamoto utakazokumbana nazo ili wakusaidie katika kukuombea,” alisema.
 
Kwa upande wake, aliyekuwa  mgeni rasmi, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Abdulla Ali Hasani Mwinyi, alisema hana tatizo na ungozi wa Paul Mkaonda kwa kuwa ni kiongozi bora.
 
Mwinyi alimtaka Makonda kuwa msikivu kwa viongozi wa dini na viongozi wengine ili kuwa kiongozi bora.
SOURCE: NIPASHE

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!