Wednesday 16 March 2016

BALOZI MPUNGWE-TUSIJIDANGANYE ZANZIBAR KUNA TATIZO"


Dar. Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Ami Mpungwe ametahadharisha kuhusu hali ya kisiasa Zanzibar, akisema “tusijidanganye kuwa hakuna matatizo” kwenye visiwa hivyo na kutaka ufumbuzi utafutwe kabla haujasababisha madhara.


Balozi Mpungwe, ambaye amefanya kazi za kidiplomasia kwa takribani miaka 25, anaungana na wanasiasa na wachambuzi ambao katika siku za karibuni wamekuwa wakitoa wito wa kutaka ufumbuzi wa matatizo ya Zanzibar upatikane kabla ya kuelekea kwenye uchaguzi wa marudio.
Zanzibar ipo kwenye hali tete kisiasa baada ya Tume ya Uchaguzi (ZEC) kufuta matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, ikisema sheria, kanuni na taratibu zilikiukwa na kutangaza tarehe mpya ya kupiga kura kuwa Machi 20.
Hata hivyo, vyama vingi vya upinzani vimesusia uchaguzi huo vikisema ZEC haina mamlaka ya kufuta matokeo wala kuitisha uchaguzi mwingine, na kuitaka Tume hiyo kutangaza mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.
ZEC ilifuta uchaguzi huo Oktoba 28, siku ambayo ilitakiwa kutangaza mshindi wa mbio za urais wa Zanzibar. Ilifuta uchaguzi wakati tayari matokeo ya majimbo 31 yakiwa yameshatangazwa, huku matokeo ya majimbo tisa yakiwa yameshahakikiwa na kusubiri kutangazwa rasmi. Pia wakati huo, tayari washindi wa nafasi za uwakilishi na udiwani walikuwa wameshatangazwa.
Hali hiyo ilikifanya chama kikuu cha upinzani, CUF kupinga hatua hiyo ya ZEC kikisema hakikuwa na mamlaka ya kufuta matokeo kwa mujibu wa katiba na hivyo kutangaza kutoshiriki kwenye uchaguzi wa marudio.
“Tunaweza kupretend (kujifanya) kuwa Zanzibar kuna matatizo ya kisiasa ambayo yanahitaji suluhu ya kisiasa, lakini ukweli ni kwamba pale kuna tatizo,” alisema Mpungwe ambaye ni balozi wa kwanza wa Tanzania nchini Afrika Kusini aliyepelekwa mwaka 1994 mara baada ya nchi hiyo kutangaza kuachana na siasa za kibaguzi.
“Tunaweza tukajiridhisha kuwa tunakwenda kwenye uchaguzi, lakini lazima tukubali lipo tatizo ambalo linahitaji suluhu.”
Alisema tatizo lililopo visiwani humo ni la kihistoria na kuwa haliwezi kumalizwa kwa vyama vikuu vya kisiasa vya CCM na CUF pekee kuzungumza. Alisema badala yake yafaa atafutwe mtu wa tatu asiyeegemea upande wowote, akisema hiyo ndiyo njia pekee ya kumaliza mgogoro.
Tangu kutokee machafuko ya kisiasa Zanzibar baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2000, CCM na CUF ndivyo vimekuwa vikikutana kutafuta suluhisho ambalo lilipatikana baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 wakati vyama hivyo vilipokubaliana kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) iliyofanya kazi kuanzia mwaka 2010 hadi 2015 kulipotokea kutokubaliana.
“Ukiwaachia CCM na CUF pekee, hawawezi kufikia muafaka. Wanapaswa kutafuta mtu wa tatu ambaye atakuwa huru na atasimama katika kuleta suluhu,” alisema Mpungwe ambaye sasa anaingia kwenye bodi za taasisi mbalimbali akiwa mkurugenzi huru.
“Naamini hakuna ukomo wa mazungumzo na naamini mgogoro utatatuliwa kwa mazungumzo na amani ya Zanzibar itapatikana kwa njia hii tu.
“Mimi ni muumini wa kutatua matatizo kwenye meza maana ukiondoka kwenye meza sasa uende wapi? Bado tunayo nafasi, tuwashirikishe wazee wastaafu na watu wa kada mbalimbali weledi wa masuala ya usuluhishi wakae na kutafuta suluhu katika tatizo lililopo.”
Alisema ni vibaya kufumbia macho suala la Zanzibar kana kwamba hakuna tatizo na kwamba kusema kuendelea kuamini hivyo hakutasaidia zaidi ya kuchelewesha utatuzi wa tatizo.
Alisema uamuzi wa kuunda serikali ya mseto ulikuwa wa busara ambao ulipunguza migogoro kwa kiasi kikubwa.

MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!