Friday, 19 February 2016

WAPINZANI UGANDA KUSUSIA MATOKEO YA UCHAGUZI MKUU




Kampala, Uganda. Wakati matokeo ya Uchaguzi Mkuu nchini Uganda yakianza kutolewa, baadhi ya wagombea wameanza kuonyesha wasiwasi wao kuhusu mwenendo wa uchaguzi huo.
Uchaguzi huo ambao unafuatiliwa kwa karibu na waangalizi wa kimataifa umewajumuisha wagombea wanane wa urais kati ya hao, watatu wanatajwa kuchuana vikali katika kinyang’anyiro hicho.


Mgombea anayewania muhula mwingine wa kusalia madarakani, Yoweri Museveni amekuwa akichuana vikali na waziri wake mkuu wa zamani, Amama Mbabazi na mwanasiasa wa siku nyingi, Kizza Besigye
Akizungumza baada ya kupiga kura, Mbabazi ambaye anawania urais wa nchi hiyo kama mgombea huru, alisema yuko tayari kukubali matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika jana kama yatatoa utashi halisi wa wananchi.
“ Niko tayari kukubali matokeo ya uchaguzi huu iwapo kutakuwa na sura halisi ya maoni ya wananchi. Lakini iwapo matokeo hayo yatachezewa sitakuwa tayari kuyakubali,” alisema.
Kauli kama hiyo imetolewa pia na mgombea wa chama cha FDC aliyesema kuwa ataheshimu matokeo hayo uchaguzi utakuwa huru na wa haki.

Kasoro zajitokeza vituoni
Wapigakura wamelalamika kucheleweshwa kwa vifaa vya kupigia kura kupelekwa vituoni licha ya wao kuwahi kufika kabla ya saa moja asubuhi.
Baadhi ya wananchi walilazimika kusubiri kufunguliwa vituo kwa zaidi ya saa mbili na kulikuwa hakuna taarifa yoyote juu ya hali hiyo.
Kwa ujumla wananchi walijitokeza kwa wingi kwenye vituo hivyo huku wengine wakionekana kuchukua tahadhari ikiwamo kupiga kura na kuondoka mara moja vituoni.
Tume iliwataka wananchi hao wasibaki katika vituo hivyo baada ya kupiga kura.
Pia, baadhi ya vituo vya kupigia kura vilifunguliwa saa moja kamili huku saa 1.45 upigaji kura katika maeneo mengi ulianza.
Kulikuwa na ripoti kuwa kuchelewa kwa kupiga kura katika baadhi ya maeneo kulisababishwa na vifaa na karatasi kutofikishwa kwa wakati. Mjini Kampala, ambako kuna makao makuu ya Tume ya Uchaguzi, kulikuwa na vituo vingi vilivyochelewa kufunguliwa.
Hata hivyo, tume hiyo kwenye ukurasa wake wa Twitter, iliandika kuwa: “Tunabaki kuwa na matumaini na tunawahakikishia kwamba nyote mtaweza kupiga kura leo. Tunasikitika kutokana na kuchelewa huku. Asanteni,” ilisomeka taarifa hiyo.

Vituo vyachelewa kufungwa
Kutokana na baadhi ya vituo kuchelewa kufunguliwa, tume hiyo ililazimika kusogeza mbele muda wa kufungwa kutoka ule wa awali wa saa kumi alasiri hadi saa moja jioni.
Tume ilisema kuwa imelazimika kuchua uamuzi huo ili kuwapa fursa wale wasiopiga kura kufanya hivyo.

Askari wamwagwa mitaani
Maofisa wa polisi walisema wametawanya vikosi vya kutosha vya askari ili kukabiliana na hali yoyote itakayoweza kujitokeza.
Kulikuwa na taarifa kuwa askari 150,000 wakiwamo wanajeshi 70,000, walitawanya nchini kote huku kukianzishwa vituo maalumu kwa ajili ya kutoa huduma za dharura pindi itakapohitajika.
Uganda imewahi kukumbwa na mashambulizi ya kigaidi kutoka kwa wapiganaji wa kundi la Al Shabaab. Hata hivyo, hakuna tishio lolote lililotolewa na wapiganaji hao kutoka nchini Somalia.

Tume yatangaza matokeo kila baada ya saa mbili
Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Taifa ya Uganda, Bandru Kiggundu alisema tume yake imejiandaa vya kutosha na kwamba matokeo hayo yatakuwa yakitolewa kila baada ya saa mbili.
Alisema ni wajibu wa tume hiyo kutoa matokeo haraka kutoka kwenye vituo vyote vilivyotumika kupiga kura hizo.
Kituo kikuu cha ukusanyaji wa kura kimefunguliwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa mpira wa miguu wa Mandela uliopo Bweyogerere wilayani Wakiso, ambako kura zote zimekuwa zikihesabiwa.
MWANANCHI.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!