Thursday, 4 February 2016
WAGENI WAUZAJI WA ARDHI KUTIMULIWA
WAGENI waliomilikishwa mashamba makubwa kwa minajili ya uwekezaji na badala yake kuyatumia kama vigezo vya kuchukulia mikopo kutoka taasisi za fedha nchini, watanyang’anywa ardhi hizo na kutimuliwa.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alisema adhabu hiyo itatolewa pia kwa wamiliki wa ardhi wa Kizungu, ambao wamekuwa wakiwauzia wageni wenzao ardhi walizopewa kuziendeleza kwa kilimo, ufugaji au uwekezaji mwingine wenye tija na badala yake kuyakalia maeneo hayo na baadaye kuyafanyia udalali. “Na tayari serikali iko mbioni kutaifisha mashamba yasiyopungua kumi wilayani Babati mkoani Manyara na mengine kadhaa katika Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani kutoka kwa wageni ambao ama wameshindwa kuyaendeleza, au wamebadilisha matumizi yake na hata wale walioamua kuyauza kwa wawekezaji wengine kinyemela,” alisema Lukuvi. Alibainisha hayo wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika Ranchi ya Darakuta iliyopo Kijiji cha Gijameda ndani ya Bonde la Kiiru wilayani Babati mkoani Manyara. Shamba hilo linamilikiwa na wageni kutoka Uswisi, Rafael Bapstna na mkewe Rita ambao wanasema walilinunua eneo hilo tangu mwaka 1985. Hata hivyo, shamba la Darakuta siyo miongoni mwa maeneo ambayo wizara ina mpango wa kuyarudisha kwa wananchi, badala yake, Waziri amewaagiza wamiliki hao kulifanyia marekebisho makubwa eneo hilo wanalotumia kwa ufugaji wa kibiashara ili liwe na tija zaidi ikiwamo kuongeza ajira kwa wananchi wa kawaida. “Kumekuwa na tabia ya raia wa kigeni kuja nchini na kudai wao ni wawekezaji, kisha kujipatia ardhi ambazo baadaye huzitumia kupata mikopo kutoka benki zetu hapa nchini,” alibainisha Lukuvi. Aliongeza kuwa mwekezaji yeyote anayewasili Tanzania ni sharti awe na mtaji, teknolojia na utaalamu wa kile anachotaka kufanya na siyo atumie rasilimali zilizomo nchini ili kujipatia fedha kutokana na mikopo. Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Babati, Crispin Meela alisema tayari amekabidhi ripoti maalumu ya masuala ya ardhi kwa waziri yakiwemo majina ya mashamba makubwa zaidi ya 10 ambayo awali yalikuwa chini ya wawekezaji wakubwa na sasa yatafutiwa hati miliki zake na kugawiwa kwa wananchi wa eneo hilo. Mbunge wa eneo hilo, Jitu Soni alitahadharisha kuwa iwapo wananchi watapewa mashamba hayo, basi iwepo sheria itakayowazuia kuyauza tena kinyemela “maana unaweza kuwapa maeneo, baadaye wakarubuniwa na watu wenye pesa halafu wakayauza tena na kubaki bila kitu
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment