Thursday 4 February 2016

KINACHOSABABISHA MTOTO KUZALIWA NJITI


Miaka ya karibuni limekuwapo ongezeko la wanawake kujifungua watoto kabla ya kufikia wakati wake. Anayezaliwa katika mazingira hayo huitwa mtoto njiti.


Mtoto anayezaliwa katika mazingira hayo hutunzwa katika mazingira maalumu hospitalini kwa kuwa wakati huo mwili wake unakuwa hauna uwezo wa kuhimili kikamilifu maisha nje ya tumbo la uzazi.
Kwa sababu hiyo, mama hubakia hospitali kwa muda fulani wakati akiwa anaendelea kupatiwa huduma maalumu itakayomsaidia aendelee kukua na kuimarika. Hali hii huongeza gharama kwa familia tofauti na mtoto anayezaliwa akiwa amefikia umri.

Wataalamu wa afya wanasema mama kujifungua mtoto ambaye hajatimiza miezi tisa ya ujauzito, kunasababishwa na mambo mengi yanayoweza kuepukika.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake nchini Cuba, Dk Jose Hernandez, anasema asilimia 80 ya sababu hizo zinaweza kudhibitiwa ikiwa mama atajipanga mapema kushika ujauzito miezi sita kabla, huku akitunzwa vema kwa kipindi chote mpaka kujifungua.
Dk Jose anasema matumizi yasiyo sahihi ya dawa ikiwamo dawa za magonjwa mbalimbali, pombe, dawa za kulevya yameongeza idadi ya wanawake kujifungua watoto njiti duniani.
Anasema matumizi ya Cocain, Heroin, bangi, mirungi, sigara au kupata moshi kutoka kwa mtu anayevuta ni sababu tosha zinazosababish mjamzito kujifungua mtoto njiti.
Anasema wanaume wengi wamekuwa wakivuta sigara mbele ya wake zao jambo linalohatarisha wajawazito.
Mambo mengine yanayoweza kusababisha tatizo hilo, anasema ni magonjwa mbalimbali kama shinikizo la damu na malaria.
“Kuna ugonjwa wa malaria; ikiwa mama atapata wale wadudu, moja kwa moja wanakwenda kushambulia kwenye kondo ambalo ni utumbo maalumu unaomlisha mtoto kutoka kwa mama.
Kwa kuwa atakuwa ameshambuliwa na bakteria, atakuwa dhaifu na hatimaye kusababisha mazingira yatakayomlazimisha mtoto azaliwe kabla ya wakati.
Anasema tatizo lingine ni upungufu wa vitamini mwilini, shambulio la bakteria kwenye njia ya mkojo maarufu kama UTI na upungufu wa damu.
Iwapo damu ya mama ni ndogo inakuwa haimtoshelezi yeye na mtoto hivyo, mazingira hayo yatalazimisha azaliwe kabla ya muda wake kufika.
Sababu nyingine ni uwepo wa magonjwa ya zinaa kama kaswende, kisonono na virusi vya ukimwi (VVU).
Dk Jose anataja mazingira mengine kuwa ni ya mama kuzaa mfululizo bila kupata muda wa kupumzika.
“Kujifungua mara kwa mara hasa bila kupitisha miaka miwili, huchangia kwa kiasi kikubwa kujifungua kabla ya wakati kwa kuwa kizazi chake kinakosa muda wa kupumzika na kujiandaa kwa ajili ya utungwaji wa mimba nyingine,” anasema.
Kinachoweza pia kusababisha mama kujifungua mtoto njiti, anasema ni mjamzito ambaye anapendelea kula vyakula vya vyenye sukari kwa wingi na wakati mwingine chumvi inapozidi.
“Vitu hivyo humsababishia mama matatizo katika uzazi na wengi hupata kisukari cha mimba ambacho kitabibu ni cha hatari,” anaongeza kusema.
Kifafa cha mimba
Muuguzi Mkuu katika wodi ya maalumu ya kutunza watoto waliozaliwa kabla ya wakati katika wodi ya Kangaroo, Hospitali ya Taifa Muhimbili, Cleopatra Mtei anasema kifafa cha mimba kimekuwa sababu kuu kwa kina mama walio wengi kujifungua kabla ya wakati.
Anasema kifafa hicho kimegawanyika mara mbili ikiwa ni pamoja na shinikizo la moyo kuwa juu zaidi ya 140/90.
“Katika mazingira hayo mama mjamzito huonyesha dalili za mwili kujaa na ukichunguza katika mkojo wake unakuta kuna protini nyingi,” anasema.
Anafafanua kuwa protini hizi zinapenya kwenda katika mkojo badala ya kukaa katika damu na kumsaidia yeye pamoja na kichanga.
Mwenye tatizo kama hilo inabidi apate msaada wa karibu wa daktari kwa kumchunguza na kushauri hatua mwafaka za kuchukuliwa ili kulinda uhai wa mama na mtoto.
Utoaji wa mimba
Cleopatra anasema utoaji wa mimba wa mara kwa mara ni miongoni mwa sababu zinazochangia mama kujifungua mtoto njiti.
Anasema kitendo cha utoaji mimba wa mara kwa mara husababisha misuli ya mlango wa kizazi kulegea na makovu kuwa mengi ndani ya kizazi.
Makovu mengi kwenye kizazi, anasema yanasababisha kondo kushindwa kujishika kikamilifu kwenye ukuta huo na kuifanya kuwa rahisi kujiachia.
Hali nyingine ambazo wanawake hawana budi kuziepuka anazitaja kuwa ni kubeba mimba katika umri mdogo au kuwa na vioteo ndani ya kizazi kama vile fibroidi.
Huduma kwa mtoto njiti
Cleopatra anasema mtu yeyote ana uwezo wa kutoa huduma ya ‘kangaroo’ kwa mtoto ikiwa hatakuwa na maambukizi ya magonjwa hasa ya ngozi na mengineyo.
“Muhimbili tunamlisha mtoto hapahapa hospitali kwa sababu wanalishwa kwa mfuko maalumu. Wanatoa maziwa kwa ajili ya kulisha hawa watoto alimradi tu mlezi asiwe na magonjwa ya ngozi,” anasema.
Huduma ya Kangaroo
Mkurugenzi wa Wauguzi Muhimbili, Agnes Mtau anasema licha ya Tanzania kuwa mojawapo ya nchi 10 zinazochangia kwa asilimia 66 ya jumla ya vifo vya watoto wachanga duniani, kwa kuzingatia kipaumbele cha kupunguza vifo hivyo, huduma ya Kangaroo imezaa matunda.
Mtau anasema kati ya asilimia 20 mpaka 25 za watoto wanaolazwa katika kitengo cha watoto wachanga ni kwa sababu walizaliwa wakiwa njiti au uzito mdogo.
Kulingana na takwimu za afya hapa nchini, anasema asilimia 13 ya watoto huzaliwa wakiwa na uzito pungufu ambao huchangia kwa asilimia 86 ya vifo vya watoto wachanga.
Anabainisha kuwa uzito pungufu wa kuzaliwa huathiri uwezo wa watoto wachanga kuishi na kukua.
Katika kitengo hicho cha Kangaroo, anasema watoto wanaozaliwa njiti ni wengi ila wanachukua watoto ambao wamezaliwa chini ya kilo 1.5 hadi gramu 500.
Changamoto zinazowakumba, anazitaja kuwa ni pamoja na mama kuathirika kisaikolojia baada ya kuzaa mtoto njiti.Anasema wamekuwa wakitumia muda mwingi kumtia moyo mama, kumwelezea nini anatakiwa kufanya katika malezi ya mtoto wake.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!