Balozi wa Tanzania nchini India, John Kijazi amesema msichana wa Kitanzania alishambuliwa nchini humo kutokana na ubaguzi wa rangi.
Balozi Kijazi alikaririwa na gazeti la Indian Express akisema kwa mtazamo wake, msichana huyo alishambuliwa kwa sababu alikuwa mweusi.
“Mwanafunzi huyo alikuwa anatishiwa maisha kwa ujumbe mfupi pamoja na marafiki zake. Ni tukio lililotushangaza. Tuko pamoja naye na wanafunzi wengine. Awali, alijihisi kama yuko Jehanamu, lakini sasa ametulia kisaikolojia ila kwa wengine ni tatizo,” alisema.
Hata hivyo, sakata hilo limechukua sura nyingine baada ya polisi nchini humo kuwasimamisha kazi askari watatu kwa tuhuma za kushindwa kutoa msaada kwa msichana huyo.
Kwa mujibu wa gazeti hilo, askari hao wametajwa kwa majina ya Inspekta Praveen Babu na makonstebo Manjunath na Rajashaker waliobainika kuwa hawakuonyesha ushirikiano wowote kwa binti huyo alipowakimbilia kuwaomba msaada.
Tukio hilo lililotokea Januari 31, kwa msichana huyo mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Bangalore kupigwa, kuvuliwa nguo na kulazimishwa na kundi la watu kutembea uchi katika eneo la Bangaluru. Inadaiwa kuwa askari hao wa Kituo cha Polisi cha Soladevanahalli walishuhudia tukio zima bila kumnusuru, licha ya kuwaomba wamsaidie.
Pamoja na kuwasimamisha askari hao, polisi juzi ilifanikiwa kuwakamata watu wengine wanne wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo, hivyo kufikisha idadi ya watuhumiwa tisa waliokamatwa.
Akitoa ufafanuzi bungeni juzi Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumetokana na juhudi za Serikali ya India ambayo iliguswa na unyama huo.
No comments:
Post a Comment