Hebu vuta picha, ni saa nane za usiku unakimbizana na muda kuwahi kurudi nyumbani baada ya kuchelewa kwenye mihangaiko yako, ukiwa unakatiza mitaa ya karibu na ikulu, unakutana na kitu kinachokufanya usiyaamini macho yako.
Unakutana uso kwa uso na mheshimiwa rais, akiwa anayumbayumba kutokana na kuzidiwa na pombe, tena akiwa amevaa bukta ya kulalia tu, yuko bize kusimamisha teksi eti zimpeleke kwenye mgahawa ambao uko wazi akanunue msosi kwa sababu anasikia njaa kali. Utahisi upo ndotoni si ndiyo?
Basi kwa taarifa yako tukio kama hilo limewahi kumkumba aliyekuwa Rais wa Urusi, Boris Yeltsin. Wakati wa utawala wa Rais Bill Clinton wa Marekani, mwaka 1995 alimualika Yeltsin, akiwa rais wa Urusi wakati huo kwenda kumtembelea kwenye Ikulu ya White House jijini Washington.
Sifa kubwa ya Yeltsin, kabla hajawa rais, alipokuwa rais na mpaka alipostaafu, ilikuwa ni kupiga mitungi mpaka anakuwa chakari. Basi baada ya shughuli zote za kiofisi kukamilika ikulu, jamaa alianza kujimiminia Vodka kwa uchu mpaka akawa tilalila. Kibaya alikuwa anakunywa bila kugonga msosi.
Akapitiwa na usingizi lakini mishale ya saa nane za usiku, alizinduka, pombe zikiwa bado kichwani na kukumbuka kwamba hakula usiku huo zaidi ya kupiga maji. Kutokana na njaa iliyokuwa inamsumbua, akaona isiwe tabu, akatoka akiwa amevaa bukta na kuwazidi ujanja walinzi wa ikulu, akaingia mitaani na kuanza kupiga kelele kusimamisha teksi impeleke kununua pizza.
Walinzi wa ikulu kuja kushtukia, rais tayari alishafika Mtaa wa Pennsylvania huku akiendelea kufanya mambo ya kilevi, wakagundua kuwa kumbe mtu huyo alikuwa rais wa Urusi, wakawa wanajiuliza imekuwaje awapite bila kumtambua?
Harakaharaka wakaenda kumchukua na kumrudisha ndani huku mlinzi mmoja akitumwa kwenda kumnunulia pizza kwani mwenyewe bado alikuwa akilalamikia njaa.
Kutokana na itifaki za White House, tukio hilo lilifanywa kuwa siri kubwa kuanzia siku linatokea mpaka miaka kumi baadaye, Rais Bill Clinton ndiye aliyeamua kulisimulia alipoamua kuandika kitabu cha kumbukumbu za maisha yake.
Kwa mara ya kwanza, Clinton alimsimulia mwandishi Taylor Branch aliyeandika kitabu cha historia ya Clinton kilichopewa jina la The Clinton Tapes: Wrestling History with the President. Rais Yeltsin alifariki miaka miwili iliyopita baada ya kuugua.
No comments:
Post a Comment