Marehemu Oscar Kambona alizaliwa mwaka 1925 katika kijiji cha Kwambe kilichopo mwambao mwa ziwa Nyasa, karibu na Mbamba-bay, wilaya ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma. Alikuwa mtoto wa marehemu Rev. David Kambona na Bibi Miriam Kambona. Rev. Kambona alikuwa ni miongoni mwa waafrika wa kwanza kupata upadre katika kanisa la Anglikana la Tanganyika.
Wakati Oscar Kambona akiwa mdogo, baba yake alikuwa akimweleza kuhusu ndoto zake juu ya uhuru wa nchi yake, hivyo Oscar alikuwa akiwa na hamu sana ya kuitumikia nchi yake. Oscar alipate elimu ya msingi nyumbani kwao, chini ya mwembe (ambao bado upo), katika kijiji chao kwa kuwatumia wazazi wake wote wawili na mjomba wake, ambao wote walikuwa walimu.
Baada ya hapo alipelekwa shule ya kati ya Mt. Barnabas, Liuli, na baadaye shule ya Sekondari ya Alliance, ambako alilipiwa ada na Askofu mzungu wa Anglikana kwa vile baba yake hakuweza kumudu kulipa ada ya paundi 30 kwa mwaka. Oscar alikuwa akisimulia jinsi alivyoweza kumshawishi Askofu huyo amlipie ada kwa kusema sala ya Baba yetu kwa kizungu. Oscar alichaguliwa kwenda ‘Tabora Boy’s Senior Government School’, ambako alionana na Julius Nyerere
kwa mara ya kwanza; wakati huo Nyerere alikuwa anafundisha katika shule ya kikatoliki. Baada ya kumaliza masomo ya sekondari alienda katika shule yake iliyopita ya Alliance kama mwalimu na baadae alichaguliwa kuwa ‘Schoolmaster’.
Ilikuwa katika mkutano wa kitaifa wa walimu, mnamo mwaka 1954, ambapo Kambona na Nyerere walikutana tena. Kambona alikuwa tayari kukitumikia chama cha TANU ambacho kilikuwa kimeanzishwa muda si mrefu, lakini Nyerere akasema wasingeweza kumwajiri kwa vile chama kilikuwa hakina fedha. Kambona akasema chama hakikuwa na fedha kwa vile hakikuwa na ‘organising secretary, na ndipo alipoamua kufanya kazi hiyo ili kujenga chama, bila ya malipo’. Aliishi kwa kutegemea akiba aliyojitunzia kwa kufanya kazi miezi 6.
Katika kipindi hiki Kambona alisafiri sehemu mbalimbali za nchi na kuonana na machifu na wazee wa vijiji ili kusajili wanachama. Katika miezi 6 alifanikiwa kusajili wanachama 10,000, na hadi kufikia mwaka mmoja alikuwa amepata wanachama hai 100,000. Kambona alitumia michango aliyopata kufungua akaunti ya kwanza ya TANU. Kisha alienda Butiama kumshawishi Nyerere achukuwe uongozi wa chama moja kwa moja.
Baada ya miaka mitatu Kambona aliamua kwenda kusomea sheria katika Chuo cha Middle Temple, nchini Uingereza mwaka 1957 kwa ufadhili wa Gavana. Akiwa London Kambona alikuwa kiongozi wa chama cha wanafunzi wa Tanganyika na Mwenyekiti wa tawi la TANU la London. Ni wakati huo ambapo Kambona alipata fursa ya kukutana kwa mara ya kwanza na watu mashuhuri kama George Padmore, mwanaharakati wa umoja wa Afrika, ambaye alimshawishi ahudhurie mkutano wa mwaka 1958 wa waafrika wote(All Africa’s Peoples Conference), uliofanyika nchini Ghana muda mfupi baada ya kupata Uhuru.
Akiwa Ghana Kambona alipata nafasi ya kukutana na mwanaharakati mwingine maarufu wa siasa za Afrikla, Kwame Nkurumah. Akiwa uingereza Kambona alikuwa mwaafrika wa kwanza kutangaza taarifa ya habari kwa Kiswahili katika idhaa ya kiswahili ya BBC. Aliporudi nchini Tanganyika, mwaka 1959, TANU ilikuwa imeshaweka bayana madai yake ya kupewa serikali ya madaraka, vinginevyo TANU ilikuwa tayari kuanzisha mapambano kama ilivyokuwa kwa Mau Mau ya Kenya.
Wakiwa London wakisubiri kupewa madaraka ya ndani, Nyerere na Kambona walijadili hatua mbalimbali ambazo zingechukuliwa ili kuepuka kutoweka kwa amani. Wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Londoni 1991, Kambona alikumbuka matukio kama hivi, ‘’Bwana Nyerere alikuwa akiishi nami katika chumba kidogo nilichopewa chuoni. Tulijadiliana ni namna gani angeweza kurudi nyumani na kuonana na wafuasi wake bila kupewa serikali ya madaraka.
Baadae nilifanikiwa kumshauri kuwa wakati atapozungumza na vyombo vya habari katika the East African Arch aseme kuwa walowezi wa kizungu ambao wapo Tanganyika wana hekima zaidi katika kanda ya Afrika Mashariki. Alikubali kusema hivyo endapo na yeye Kambona angekubali kukatisha masomo yake ya sheria huko London na kurudi Tanganyika ili ampe nguvu na kumuunga mkono katika kikao cha kamati kuu ya TANU wakati akitetea tamko lake la wenye hekima zaidi. Katika uchaguzi wa kwanza TANU ilishinda viti vyote isipokuwa kimoja.
TANU iliunda serikali ya mambo ya ndani chini ya Nyerere ambaye alikuwa Waziri kiongozi wa kwanza. Na katika harakati hizo za matayarisho ya serikali ya ndani, Kambona alimwoa Flora Moriyo wakati wakiwa kwenye msafara wa harakati za kukamilisha matayarisho ya uhuru na serikali ya Uingereza.
Harusi ilifungwa katika kanisa la Mt. Paul, London, na Nyerere ndiye alikuwa msimamizi. Kambona aliteuliwa kuwa waziri wa Elimu. Baadaye alishika nyadhifa za waziri wa Mambo ya Ndani, Mambo ya nchi za nje na Ulinzi na Tawala za Mikoa. Pia alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika na mwenyekiti wa utayarishaji wa AOU charter.
Mwaka 1964, Kambona alifanya kazi kubwa katika kuunganisha Zanzibar na Tanganyika, akiwa pamoja na Raisi Nyerere, Raisi Karume na Waziri Kiongizi Hanga. Hii ilikuwa ni baada ya mapinduzi ya Zanzibar.
Wakati wa wanajeshi wa kikosi cha Calito walipoasi mwaka 1964 Kambona alikuwa msuluhishi mkuu kati ya serikali na wanajeshi hao. Nyerere na Kawawa walienda mafichoni Kigamboni. Baada ya siku tatu za majadiliano Kambona aliafiki kuongeza kasi ya kuwawezesha waafrika kushika hatamu jeshini. Katika mahojiano na gazeti la Daily Telegraph la London
Kambona alisema, ‘baada ya kuwatuliza wanajeshi nilikwenda kuwatafuta viongozi wengine na kuwarudisha mjini kwa kutumia Land Rover yangu’. Hatimaye maasi hayo yalidhibitiwa kabisa na majeshi ya Uingereza na Nyerere alimsifu Kambona busara na uaminifu wake.
Tofauti kati ya Nyerere na Kambona zilianza kujitokeza baada ya maasi ya wanajeshi. Nyerere alitaka kuanzisha mfumo wa chama kimoja nchini ili kuimarisha usalama. Kambona alipinga hoja hiyo kwa maelezo kwamba mfumo huo ungezorotesha uhuru wa watu na maendeleo ya demokrasia.
Hata hivyo, Kambona alishindwa bungeni; alikataa kusaini muswada (bill). Mwaka 1967, baada ya safari ya China ya mwaka 1965, Nyerere akiwa amependezwa na mfumo wa kikomonist wa Mao, alitaka kuanzisha mfumo kama huo kwa jina la ujamaa. Dhana ya msingi ya mfumo wa ujamaa ilikuwa ni kuwahamishia watu katika vijiji vya ujamaa na kutaifisha viwanda ana mali. Kambona hakukubaliana na utaratibu huo kwa maelezo kwamba ungeongeza umaskini na udhibiti wa serikali kwa watu.
Alijiuzulu kutoka katika serikali na Chama na hatimaye yeye na familia yake walikimbilia Kenya na kisha Uingereza ambako walipatiwa uhifadhi wa kisiasa. Mara baada ya kuondoka mali za Kambona zilichukuliwa.
Ndugu zake wawili, waliwekwa kizuizini bila ya kufikishwa mahakamani na kufungwa kwa zaidi ya miaka kumi. Wanafamilia wengine walinyanyaswa na kuwekwa kizuizini. Wengine kati yao walibambikiziwa kesi za uhaini, wakafikishwa mahakamani na kisha kufungwa na serikali. Kati yao walikuwa
Bibi Titi ambaye alipigania uhuru pamoja ana Nyerere na alikuwa kiongozi wa jumuia ya kina mama. Alikuwepo pia Michael Kamaliza ambaye alikuwa mwanaharakati wa chama cha wafanyakazi, mwanachama wa TANU na waziri. Wengine ni pamoja na Gray Mattaka, John ana Eliya Chipaka na Prisca Chiombola. Kambona alituhumiwa kuwa kiongozi wa wahaini wakati akiwa London na alihukumiwa bila kuwapo. Watuhumiwa hatimaye walikata rufaa katika mahakama kuu ya Afrika Mashariki na wakaachiwa huru.
Hata hivyo, baadae walikamatwa na serikali na kufungwa tena. Kambona alituhumiwa kuwa aliiba pesa nyingi sana zikiwa ni mali ya umma, kitu ambacho Kambona alikataa katika taarifa yake na waandishi wa habari Septemba 6 huko London 1967.
Tuhuma hizo zilisema kuwa ‘’ Kambona amekutwa na pesa nyingi sana kama karanga alipopekuliwa katika Uwanja wa ndege Embakasi Nairobi’’ Hata hivyo Kambona katika taarifa yake kwa waandishi wa habari alikanushkuhusika na tuhuma hizi na badala yake akaipa serikali ya Tanzania kuiomba serikali ya Kenya kutoa ukweli juu ya jambo hilo- jambo halikufanyika.
Akiwa Londoni Kambona aliishi maisha ya shida na dhiki. Katika mwaka 1982 ndugu zake Kambona na Otini Kambona walifunguliwa kutoka kizuizini baada ya juhudi za waziri mkuu wa New Zealand Robert Muldoon.
Katika mwaka 1990 Kambona akiwa na matumaini makubwa ya mabadiliko ya kisiasa katika Tanzania hususani mabadiliko ya demokrasia, aliunda chama kiitwacho Tanzania Democratic Alliance.
Wakati vyama vingi vilipoanzishwa Tanzania 1992 Kambona aliomba kurudi Tanzania. Serikali ya Tanzania ilimkatalia katakata na kudai kuwa Kambona hakuwa Mtanzania. Kambona badala yake aliomba Serikali ya Uingereza kumpa pasi ya kusafiria kurudi Tanzania.
Hata hivyo Serikali ya Tanzania ilitamka kwamba pamoja na kupata pasi hiyo itamweka ndani pindi atakapoingia Tanzania. Pamoja na msimamo huo wa Serikali, Kambona alitua kwenye ardhi ya Tanzania tarehe 5 september 1992. Hakuna mamlaka iliyomkamata bwana Kambona bali alipewa miezi mitatu awe amekamilisha utata wa uraia wake.
Baada ya kurudi, Tanzania aliona kuwa harakati za kuelekea kwenye demokrasia ya kweli zilikuwa zikienda kwa mwendo wa kinyonga. Hata hivyo Kambona hakuweza kujihusisha kwa kiasi kikubwa na siasa kutokana na matatizo ya kiafya hususani shinikizo la damu.
Hatimaye Oscar Kambona alifariki akiwa katika matibabu mjini London mwezi Juni 1997. Mdogo wake Otini Kambona naye alifariki katika kipindi hichohicho kutokana na magonjwa ya moyo.
Wote wawili walizikwa Tanzania, na serikali ya Tanzania iligharimia gharama zote za usafirishaji miili ya marehemu ndugu hawa.
Oscar Kambona ameacha mke na watoto wawili. Mtoto wao wa kwanza Mosi Kambona aliuawa mjini London katika mazingira ya kutatanisha.
Roho ya Oscar Kambona na ndugu na jamaa wote waliotangulia MWENYEZI MUNGU aziweke pema peponi, Amin.
No comments:
Post a Comment