Watu 11 wamefariki dunia papohapo katika ajali mbaya iliyohusisha basi la Simba Mtoto lililokuwa limejaa abiria kugongana uso kwa uso na lori lililokuwa limebeba mchanga, katika eneo la kijiji cha Pangamlima, kata ya Makole, wilayani Muheza, mkoa wa Tanga.
Ajali hiyo ilitokea jana saa 1:00 katika barabara kuu ya Tanga -Segera, wakati basi hilo likielekea Dar es Salaam na lori likielekea njia ya kwenda Tanga.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Miyao Msikhela, alisema imehusisha basi la kampuni ya Simba Mtoto lenye namba za usaji T. 393 DDZ, ambalo lilikuwa likiendeshwa na Mwalimu Sheja na lori la mizigo aina ya Scania lenye namba za usajili T 738 CFE ambalo lilikuwa linatoka Moshi kuelekea Tanga mjini likiwa limebeba mchanga ambao ulitawanyika barabara baada ya ajali.
CHANZO CHA AJALI
Alisema ajali hiyo ilisababishwa na dereva wa lori ambaye lilimshinda na kuacha njia yake kulifuata basi la abiria na kugongana uso kwa uso na kusababisha vifo vya watu 11 na majeruhi 26.
Alitoa onyo kwa madereva wote kuwa waangalifu wanapokuwa barabarani ili kuepusha ajali za kizembe kama hizo na kusababisha vifo vya watu wasio na hatia na vilema vya maisha.
MAITI ZAPELEKWA MUHEZA
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Elias Mayala, alisema walipokea maiti za watu 11waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
Alisema maiti sita zimetambuliwa na ndugu na jamaa zao na tano bado hazijatambuliwa na kwamba zimehifadhiwa katika chumba cha maiti hospitalini hapo.
WALIOKUFA
Aliwataja waliokufa na kutambuliwa kuwa ni, Fred Venus, Mwalimu Mbwana, Sada Ally, Nagiris Hamisi, Raya Saidi na Mohamedi Saidi.
WALIOJERUHIWA
Mganga mkuu huyo wa wilaya aliwataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo kuwa ni, Erasto Mlinga, mkazi wa Dar es Salaam, Christian Nkoal, mkazi wa Tanga mjini, Omar Mohamed, mkazi wa Zanzibar, Hussen Mabula, mkazi wa Muheza, Kibibi Athumani, mkazi wa kijiji cha Kasanga na Enocent Kileo, mkazi wa Moshi.
Wengine ni Makay Kitete, mkazi wa Tanga mjini, Hamza Sesige, mkazi wa Kicheba, Muheza, Sharifa Hatibu, mkazi wa Masuguru, Muheza, Hamad Mwinyi, mkazi wa Dar, Mussa Mohamed, mkazi wa Tanga, Abdallah Njama, mkazi wa Makorora, Tanga na Masudi Khatumu, mkazi wa Chambageni, Tanga.
Wengine ni Haruna Waziri, mkazi wa Tanganyika, Muheza, Ally Juma Iddi, mkazi wa Makanya, Same, Regina Robert, mkazi wa Tanga mjini, Dudu Hassan, mkazi wa Tanga mjini na Dominicka Isack, mkazi wa Tanga mjini.
Pia wapo, Chrstina Robert, mkazi wa Same, Mustafa Mohamed, Mary Kimasha, Marykioli Josephe, Hemed Said, Habudi Kilozo, Doto Andrea na Samia Juma, wote wamelazwa katika Hospitali Teule Wilaya ya Muheza kwa matibabu.
RAIS MAGUFULI ATOA RAMBIRAMBI
Rais John Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza, kufuatia vifo vya watu 11 waliopoteza maisha katika ajali hiyo.
Rais Magufuli pia amewapa pole ndugu, jamaa na marafiki wote waliofikwa na msiba huo na amewataka kuwa wavumilivu na wastahamilivu katika kipindi hiki kigumu.
"Nimepokea taarifa ya vifo hivi kwa mshituko mkubwa na kupitia kwako Mkuu wa Mkoa wa Tanga napenda kuwapa pole nyingi wote waliofikwa na msiba huu mkubwa na naungana nanyi katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo," alisema Rais Magufuli katika taarifa yake kwa vyombo vya habari na kuongeza:
“Nawaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi na natoa pole kwa majeruhi wote walioumia katika ajali hii.”
Aidha, Rais Magufuli amewakumbusha watumiaji wote wa barabara, hususan madereva wa vyombo vya moto kuwa makini watumiapo barabara kwa kuzingatia sheria zote zinazosimamia usalama barabarani ili kuepusha ajali.
NIPASHE.
NIPASHE.
No comments:
Post a Comment