Saturday, 30 January 2016

WAZANZIBAR WAANDAMANA NCHINI CANADA KUPINGA KURUDIWA KWA UCHAGUZI ZANZIBAR‏

Na Mwaandishi wetu Washington 
Wakati hali ya kisiasa Visiwani Zanzibar ikiwa inazidi kutokota, bila kujali theluji na baridi kali, Wazanzibari waishio nchini Canada mnamo tarehe 27 mwezi huu walifanya maandamano katika Mji Mkuu wa nchi hiyo, Ottawa katika juhudi za kutafuta uingiliaji kati wa kimataifa katika kusaka suluhisho la amani kwa mgogoro wa kisiasa Visiwani humo.
Mandamano ya Wazanzibari waishio nchini Canada wakiwa mwenye ofisi ya European Union  Mjini Ottawa
Wazanzibari hao waliandamana hadi kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu wa Canada kwa lengo la kufikisha ujumbe wao kukhusiana na hali mbaya ya kisiasa huko Zanzibar.



Akizungumza na Swahilivilla, mmoja wa waandaaji wa maandamano hayo Bwana Zamil Rashid alisema kuwa lengo la maandamano hayo ni kuwaunga mkono ndugu zao Wazanzibari katika harakati za kudai demokrasia ya kweli na kupinga hatua za kufutwa kwa uchaguzi Mkuu Zanzibar.
"Madhumuni ya maandamano yetu yalikuwa ni kuwaunga mkono ndugu zetu wa Zanzibar kwa mambo yaliyofanyika, na kwamba hatukubaliani nayo" alisema Bwana Zamil na kuendelea "Wazanzibari walioko nchini Canada wanapinga jambo hilo lilofanywa na Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na matamshi aliyoyatoa Bwana Jecha Salim Jecha ya kufuta uchaguzi"
Aidha maandamano hayo yalikuwa na lengo la kuiomba Serikali ya Canada kuingilia kati katika kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa Visiwani Zanzibar kabla hali haijawa mbaya zaidi.
Mbali na Ofisi ya Waziri Mkuu wa Canada, Wazanzibari hao pia waliandamana hadi kwenye Ofisi za Umoja wa Ulaya nchini humo kwa dhumuni hilo hilo.
"Vilevile tumefikisha ujumbe wetu kwa Umoja wa Ulaya (EU) ili walishighulikie swala hili haraka iwezekanavyo kabla hayajatokea maafa kwa Wazanzibari", alisema Bwana Zamil.
Katika Risala yao kwa pande zote mbili, waandamanaji hao wametoa wito wa kutangazwa mshindi badala ya kurejewa kwa uchaguzi kama ilivyotangazwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Bwana Jecha Salim Jecha. "Tumetoa wito wa yule aliyeshinda uchaguzi atangazwe, na siyo kurejea uchaguzi" alisisitiza Bwana Zamil.
Kwa kufikisha ujumbe wao kwa Umoja wa Ulaya, wazanzibari hao pia walikuwa na lengo la kutoa wito kwa nchi nyengine duniani kusaidia katika kuupatia suluhu mzozo wa kisiaza Zanzibar, ikiwemo pia kusitisha missada ya kiuchumi kwa Tanzania.
"Tumeziomba serikali za Canada, Umoja wa Ulaya na nchi nyengine duniani kusitisha misaada kwa Zanzibar na Tanzania ili kushinikiza haya mambo yaliyotokea yasifanyike tena", alisema Bwana Zamil.
Mbali na Wazanzibari, maandamano hayo pia yalihudhuriwa na wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Ottawa, Vyuo vyengine, Waandishi wa Khabari pamoja na wapenda amani na demokrasia duniani.
Kufutwa kwa uchaguzi wa Zanzibar kinyume na sheria na tangazo la kurudiwa tena kwa uchaguzi huo kuliwakasirisha Wazanzibari wengi, na ndiyo moja ya siri ya kujitokeza kwa wingi kwa Wanzibari katika kufanikisha maandamno hayo.
"Wazanzibari walijitokeza kwa wingi na tumefarajika kwa hilo", alisema Bwana Zamil na kuongeza kuwa "Wazanzibari walikasirishwa na kitendo kile kilichofanywa na Jecha Salim Jecha pamoja na Serikali ya CCM cha kufuta Uchaguzi na kutaka kurudiwa mwengine"
Alifafanua msingi wa demokrasia umejikita kwenye msemo wa Kiswahili usemao kuwa "asiyekubali kushindwa si mshindani".
"Maana ya kuwa na mfumo wa vyama vingi ni kukubali kushinda au kushindwa, sasa ikiwa mmoja kashindwa na hakutaka kukubali kushindwa, basi itakuwa hakuna haja ya kufanya mambo ya vyama vingi" alifafanua Bwana Zamil na kusisitiza "Hilo ndilo lililowakasirihswa Wazanzibari, kwani wanahisi wanadharauliwa".
Itafaa kukumbusha kuwa mfumo wa vyama vingi ulikuweko Zanzibar kabla ya Mapinduzi ya mwaka 1964. Kufuatia Mapinduzi hayo mfumo huo ulitoweka na kurejea tena mwaka 1992 ambapo uchaguzi wa mwanzo ulifanyika mwaka 1995. Chaguzi zote ambazo hufanyika kila baada ya miaka mitano visiwani humo huwa zinagubikwa na utata huku Chama Kikuu cha Upinzani cha Wananchi (CUF) kikidai kuporwa ushindi wake.
Katika sherehe za kuadhimisha miaka 52 ya Mapinduzi ya Zanzibar zilizofanyika tarehe 12 mwezi huu, baadhi ya wanachama wa Chama Tawala cha CCM walibeba mabango yaliyokuwa na maneno ya kibaguzi kama vile kuwataka machotara waondoke na kwamba Zanzibar ni nchi ya Waafrika.
Mabango hayoyalikuwa kama kidonda kipya juu ya kovu mbichi na kupelekea hali tete zaidi visiwani humo. Kukhusiana na hilo Bwana Zamil alisema "Eti wanasema machotara wende kwao, haya yote yamewakera Wazanzibari, kwa sababu, matusi kama yale ni matusi ya kibaguzi"
Mada hiyo pia ilijitokeza kwenye maadamano ya jijini Ottwa ambapo baadhi ya mabango yalibeba ujumbe uliosomeka "Ubaguzi ni saratani kwa jamii ya Zanzibar yenye mchanganyiko wa watu wa rangi tofauti, wakati umefika sasa wa kumaliza ubaguzi wa rangi"
Baadhi ya mabango hayo yaliyoandikwa kwa lugha rasmi za Canada za Kiengereza na Kifaransa, yalibeba ujumbe ukiitaka serikali ya nchi hiyo kukata uhusiano wa Kibalzi na Tanzania, kusimamaisha misaada ya kiuchumi kwa Tanzania na Zanzibar, kupinga kurudiwa kwa uchaguzi na badala yake kutangazwa mshindi wa Uchaguzi uliopita, kumsuta Rais Magufuli kwa kujishughulisha na kuzuia ubadhirifu wa fedha za taifa badala ya kuzuia damu za Wazanzibari zisimwagike na mengineyo.
Akijibu swali la mwandishi wetu iwapo kuna majibu yoyote kwa risala yao, Bwana Zamil alisema "Wamesema kuwa watalishughulikia haraka iwezekanavyo kabla mambo hayajaharibika zaidi Zanzibar".
Aliongeza kuwa Afisa wa Umoja wa Ulaya aliepokea risala yao aliahidi kuifanyia kazi mara moja. "Amesema leo hii ataisambaza kwa wanachama wote wa Umoja huo ile risala ili waisome na kuchukua hatua za haraka zaidi" alisisistiza Bwana Zamil.
Kukhusu ukimya wa Rais wa Tanzania juu ya yale yanayoendelea Zanzibar, Bwana Zamil amlimtolea wito Dkt John Pombe Magufuli kuushughulikia mzozo wa Zanzibar ili kuepusha janga la kibinadamu.
"Rais wa Tanzania ana jukumu, ni lazima asimamie haki na usalama wa Wazanzibari wote, na Wazanzibari lazima haki yao aisimamie, siyo kama hivi kukaa kimya" alisihi mwanaharakati huyo, na kuongeza, "Hii inaonesha kama kwamba anakubaliana na yale yanayotokea Zanzibar"
Kwa upande mwengine, mwanaharakati huyo aliwatolea nasaha WanaCCM wa Zanzibar kwenda na wakati na kuwa washindani wa kweli, huku wakijua demokrasia ni kubadilishana madraka kwa njia za amani.
"Zanzibar ni mali ya Wazanzibari wote na wala siyo milki ya CCM. Kwa hiyo aliyeshindwa akubali kushindwa, na aliyeshinda wampongeze ili watu waishi kwa hali ya mapenzi na amani kuliko kusubiri mpaka watu kupigana, mambo ambayo yataleta madhara makubwa", alisema Bwana Zamil na kuonya "...inaweza kufika mahala watu kufikishana kwenye Mahakama za Kimataifa"
Alitoa ukumbusho kwa viongozi walioko Madarakani Zanzibar kuwa kinga ni bora kuliko tiba, na kusema "Ningeiomba Serikali isikubali kufika huko" Halkadhalika alitoa wasia maalum kwa Rais wa Zanzibar Alhaj Ali Mohammed Shein kwa kusema "Namuusia Rais Shein asikubali kufikishwa mahala ambapo patakuja kumletea khasara hapa dunianiu na huko Akhera"
Maandamano ya Wazanzibari nchini Canada yanakuja kufuatia yale ya Jumuiya ya Wazanzibari waishio nchini Marekani (ZADIA) yaliyofanyika Ikulu ya nchi hiyo (White House), na kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York.
Maandamano kama hayo pia yalifanyika nchini Uingereza na sehemu nyengine za Ulaya. Kwa muqtadha huu Bwana Zamil amewatolea wito Wazanzibari popote Ulimwenguni kuchukua hatua za kushinikiza kupatikana ufumbuzi wa amani kwa mgogoro wa kisiasa visiwani Zanzibar.
"Nawashauri Wazanzibari walioko katika sehemu nyengine duniani waungane na Wazanzibari wenzao ili kupigania demokrasia ya kweli katika nchi yao" alishauri, na kunasihi "Na katika kufanya hivyo, wapiganie kwa njia za amani haki na usawa"
Vile vile, Bwana Zamil alitoa shukrani maalum kwa Polisi wa Canada kwa ushirikiano wao mzuri tangu mwanzo mpaka mwisho wa shughuli yao.
Ikumbukwe kwamba, mgogoro wa sasa wa kisiasa Zanzibar uliripuka kufuatia Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 25 Oktoba mwaka jana baada ya uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar Bwana Jecha Salim Jecha wa kutangaza kuufuta uchaguzi wa Zanzibar na matokeo yake kwa madai ya kuwepo kwa kasoro nyingi za uchaguzi khususan Kisiwani Pemba ambako ndiko kwenye ngome kuu ya Chama cha upinzani cha CUF.
Wataalamu wa maswala ya Sheria za Zanzibar wanaona kuwa hatua hiyo ya Bwana Jecha haikuwa ya kisheria, na wasimamizi wa uchaguzi, wachunguzi, wadadisi na wachambuzi wa nje na ndani ya nchi waliuelezea uchaguzi huo kuwa ulifanyika katika mazingira huru na ulikuwa wa haki.
Inaaminika kuwa hatua ya kufutwa kwa uchaguzi huo ilikuja baada ya kubainika kuwa mgombea wa Urais kwa tiketi ya Chama cha CUF Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa amemtangulia mpizani wake mkubwa aliyekuwa akitetea kiti chake Rais Ali Mohammed Shein.
Kufuatia kufutwa kwa uchaguzi huo, vikao vya siri vya mzungumzo vilifanyika kwa zaidi ya miezi miwili katika Ikulu ya Zanzibar vikiwashirikisha Rais Ali Mohammed Shein, Makamo wake wa Kwanza Maalim Seif Sharif Hamad, Makamo wa Pili Balozi Seif Ali Idd pamoja na Marais wastaafu wa Zanzibar, Mabwana Amani Karume, Salmin Amour na Ali Hassan Mwinyi.
Wakati vikao hivo vya siri vikiwa vinaendelea, mitaani kukazaliwa msamiati mpya uliojulikana kwa jina la "drips" zikiwa ni tetesi kuhusu kile kinachoendelea katika mazungumzo hayo.
Hatimaye mfuko wa drips ukapasuliwa baada ya mazungumzo hayo kushindwa kufikia mwafaka, na Bwana Jecha kujitokeza tena na kutangaza kuwa uchaguzi utarudiwa tarehe 20 Machi mwaka huu na hivyo kupelekea mtafaruku zaidi wa kisasa Visiwani humo.
Kufuatia uamuzi huo, chama cha CUF kimesema kuwa hakitoshirki kwenye uchaguzi wa marudio, na kushikilia msimamo wake wa kutaka matokeo ya uchaguzi wa Oktoba yatangazwe, kwa vile uchaguzi ulikuwa huru na wa haki.
Hali ya mgando wa kisiasa Zanzibar imepelekea athari mbaya za kiuchumi na kijamii, huku mfumko mkubwa wa bei khususan bidhaa muhimu kama vile chakula ukiarifiwa kufikia zaidi ya asili mia 10

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!