Chama Cha Mapinduzi (CCM), jana kiligaragazwa na muungano wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwenye uchaguzi wa nafasi ya Meya na Naibu Meya katika Halmashauri za Manispaa ya Kinondoni na Ilala, jijini Dar es Salam, ambapo risasi tatu zilirushwa Magomeni na chama tawala kususa Ilala.
Kwa upande wa Kinondoni, aliyeshinda nafasi ya Meya ni Boniface Jacob wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kura 38 dhidi ya mpinzani wake, Benjamin Sita wa CCM, aliyepata kura 20.
Mbali na Chadema, vyama vingine vinavyounda Ukawa ni CUF, NCCR Mageuzi na NLD.
Nafasi ya unaibu Meya ilichukuliwa na Jumanne Mbunju wa Chama cha Wananchi (CUF), aliyeshinda kwa kura 38 dhidi ya mpinzani wake, George Manyama wa CCM, aliyepata kura 19.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Kagurumjuli Titus, alimtangaza Jacob kuwa ndiye Meya wa Manispaa hiyo na Naibu wake kuwa ni Mbuju katika uchaguzi ambao ulikuwa na ulinzi mkali wa polisi.
Awali, kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo, wabunge, madiwani na maofisa walioshiriki uchaguzi huo, walipata fursa ya kula kiapo na kisha wagombea hao wawili kujinadi na kuomba kura huku kila mmoja akitumia dakika 5 kujieleza.
Uchaguzi huo ulijumuisha wajumbe 58 ambapo 38 walikuwa wanatoka Ukawa na wajumbe 20 kutoka CCM.
Pia katika uchaguzi huo uliofanyika kwenye ofisi za Manispaa Magomeni, kura moja kati ya 58 zilizopigwa iliharibika hivyo mgombea wa unaibu Meya wa CCM, George Manyama kuambulia kura 19.
HALI ILIVYOKUWA AWALI
Kabla ya uchaguzi huo kufanyika, Polisi walitanda eneo hilo ili kuimarisha ulinzi na usalama huku wakikagua watu wanaoingia ndani na kuzuia wasiohusika kuingia.
Askari hao pia walikuwa katika mlango wa kungia ukumbi wa mkutano wakikagua majina ya wabunge na madiwani wanaotakiwa kuingia kwenye kikao hicho cha uchaguzi, na wakati uchaguzi ukiendelea ndani askari waliokuwa wamevalia kiraia na wale waliovalia sare walionekana pia wakiwa nje ya mlango wakifuatia uchaguzi huo.
POLISI WARUSHA RISASI
Majira ya 4:9 asubuhi Jeshi la Polisi lilizamika kurusha risasi tatu hewani ili kutuliza ghasia zilizoanza kufanywa na wafuasi wa Chadema.
Wafuasi hao walianza vurugu hizo wakipinga kitendo cha kuzuiliwa kuingia ndani ya uwanja wa ukumbi, wakati wafuasi wa CCM wakiingia ndani.
Kufuatia vurugu hizo, Meya wa Manispaa hiyo, Boniface Jacob (kabla hajachaguliwa), alilazimika kutoka nje na kuwatuliza akiwahakikishia kuwa hakuna mfuasi wa CCM aliyeingia bila utaratibu.
KATIBU CCM ANUSURIKA KIPIGO
Wakati wabunge na madiwani wakisubiri utaratibu wa kuingia kwenye ukumbi wa mkutano, Katibu wa CCM Wilaya hiyo, Athumani Shesha, alinusurika kipigo wakati akitaka kuingia kwenye viwanja hivyo.
Hatua hiyo ilikuja baada ya kutakiwa kuingia ndani ili akaeleze utaratibu na alipojaribu kuingia ndipo wafuasi wa Chadema walianza kumshambulia kwa maneno wakimtaka asiingie.
Katibu huyo alisaidiwa na askari waliotumia nguvu kubwa kumwingiza ndani ambapo alienda moja kwa moja kwenye ofisi za Manispaa hiyo.
Askari wanaolinda eneo hilo, walieleza kuwa Katibu huyo wa CCM alikuwa amefika eneo hilo tangu saa 1:30 asubuhi kwa shughuli rsmi na kwamba siyo mamluki kama ambavyo wafuasi hao walikuwa wakidhani.
MEYA AHIIDI USHIRIKIANO
Akitoa shukrani zake mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi, Jacob aliahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na watu wa vyama vyote.
“Nashukuru kwa kuniamini na kunipa nafasi hii," alisema Jacob na kufafanua, "si kwamba mimi naweza sana kuliko wengine bali ni fursa tu nimepata.
Nawaahidi kwamba nitashirikiana na kila mtu kuleta maendeleo bila kujali tofauti zetu za kisiasa.
"Pia naomba mawaziri na wabunge walioshiriki uchaguzi huu pia tushirikiane kuleta maendeleo.”
Jacob ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ubungo, aliahidi kuongeza mapato ya Halmashauri kutoka bilioni 44 hadi kufikia bilioni 100 kwa mwaka.
WAFUASI WASEREBUKA
Mara baada ya Meya kutangazwa kuwa mshindi, wafuasi waliovalia sare za Chadema na CUF, walionekana wakiimba nyimbo mbalimbali kwa furaha pamoja na kucheza mziki uliokuwa kwenye gari ambao walikuja nao.
Wakati hayo yakiendelea, magari ya askari polisi pamoja na lile la maji ya kuwasha yalikuwa yametanda eneo hilo ili kulinda usalama.
Wafuasi hao walikuwa na mabango mbalimbali yaliyokuwa na jumbe tofauti tofauti huku wakiendelea kucheza mziki.
Ilala mambo yalikuwaje?
Licha ya CCM kususia uchaguzi huo kwa kutoka nje ya ukumbi wa mkutano, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, ambaye alikuwa Katibu wa mkutano wa uchaguzi, Raymond Mushi jana alimtangaza Charles Buyeko (Chadema) kuwa Meya wa Manispaa hiyo baada ya kupata kura 31 za ndiyo kati ya 54.
Pia alimtangaza Omari Said (CUF) kuwa Naibu Meya wa Manispaa hiyo baada kupata ushindi wa kura 31 za ndiyo kati ya 54.
Wajumbe halali waliofika na kutakiwa kupiga kura ni 54, kati yao 36 wakiwa ni madiwani wa kuchaguliwa, madiwani viti maalum 13, wabunge wa majimbo watatu na wabunge wa kuteuliwa wawili.
Wajumbe wa mkutano wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walitoka nje ya ukumbi na kususia uchaguzi baada ya kuambiwa kuwa wajumbe kutoka Zanzibar hawataruhusiwa kupiga kura.
Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa mkutano huo wa uchaguzi, Isaya Mngurumi alitangaza utaratibu wa kupiga kura na kusema wabunge wawili wa viti maalum kwa upande CCM na Chadema nao wataruhusiwa kupiga kura.
Alisema suala la umeya ni suala la serikali za mitaa na Katiba ya mwaka 1977 pamoja na ya Zanzibar ya mwaka 1984 hazionyeshi kipengele cha serikali za mitaa kama ni suala la Muungano.
Baada ya kauli hiyo, wajumbe ambao walikuwa ni wapiga kura, pamoja na waliofika kwa ajili ya kushuhudia uchaguzi huo upande wa CCM, waliamua kuzomea na kuleta fujo katika mkutano huo huku mmoja wa wanaCCM akidiriki kulinyanyua sanduku la kupigia kura na kutokomea nalo.
Baada ya kuona hivyo, Mngurumi alisema uchaguzi utafanyika kwa utaratibu huo na ambaye anaona ameonewa na kutoridhika aende mahakamani.
Mngurumi aliwataja wabunge wawili wa viti maalum ambao watapiga kura kuwa ni Sophia Simba (CCM) pamoja na Annatropia Theonest (Chadema), huku wabunge wa viti maalum kutoka Zanzibar waliofika kwa ajili ya kupiga kura kuambiwa hawataruhusiwa kupiga kura.
“Nimekwishaamua utaratibu ndio huu ambao hawako tayari waende mahakamani na Jeshi la Polisi lipo hapa kwa ajili ya kuhakikisha usalama," alisema Mgurumi kabla ya kuamuru polisi "nawaomba mfanye kazi yenu uchaguzi unaendelea kufanyika kama kawaida.
"Wajumbe kutoka Zanzibar suala la serikali za mitaa si la Muungano, hamruhusiwi kupiga kura.”
UCHAGUZI WAANZA SAAA 8
Mbali na ratiba ya uchaguzi kuonyesha kuwa muda wa kuanza ni saa 4 asubuhi, ulicheleshwa kutokana na kikao cha awali kilichowakutanisha viongozi wa pande zote waliosimamisha wagombea.
Mngurumi alisema kikao hicho kilipitisha utaratibu wa kuruhusu wapiga kura wa viti maalum sita kwa kila chama, licha ya baadaye kutengua makubaliano hayo baada ya wajumbe wa CCM kuleta vurugu.
Katika kura halali za kumchagua Meya wa Manispaa hiyo, kura halali zilikwa ni 54, kura zilizoharibika hazikuwepo huku Chadema ikipata 31 na CCM sifuri.
Kura ya kumchagua Naibu Meya, kura halali zilikuwa 54, kura zilizoharibika hazikuwepo huku Chadema ikipata kura 31 na CCM sifuri.
MBOWE ANENA
Akizungumza mara baada ya uchaguzi kumalizika, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema Manispaa hiyo itaongeza mapato yake kutoka Sh. Bilioni 78 zinazokusanywa sasa hadi kufikia Sh. Bilioni 200 kwa mwezi.
“Ilala itatia fora... ni kati ya Manispaa zilizo na vyanzo vya mapato zaidi kuliko nyingine, kukusanya Sh. Bilioni 200 inawezekana kabisa,” alisema Mbowe.
No comments:
Post a Comment