Sunday, 17 January 2016

UCHUMI HUU UWANUFAISHE KWANZA WAZAWA


Serikali ilishaonyesha dhamira ya kuendesha mafunzo ya uelewa mpana wa teknolojia  ya gesi na mafuta kwa vijana wazawa, nia ikiwa ni kuwawezesha kupata ajira kwenye sekta hiyo katika kipindi hiki ambacho taifa linategemea kuingia kwenye uchumi mkubwa utakaotegemea umeme wa gesi. 



Dhamira hiyo ilitangazwa na Wizara ya Nishati na Madini mwanzoni mwa mwaka huu wakati wa warsha ya kuweka mikakati ya elimu kwa wadau ambayo iliandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Jamii (ESRF) ikishirikiana na VTEC-Afrika na taasisi nyingine za kimataifa.

Ofisa Mwandamizi wa Ugani wa Wizara ya Nishati na Madini, Neema Lugangira aliyemwakilisha Waziri alisema ni wakati muafaka wa Tanzania kuona fursa za kufaidika na sekta ya gesi.  

Lugangira alitoa angalizo kuwa pamoja na matarajio ya kupata gesi nyingi nchini, bado lipo tatizo kubwa la kutokuwa na elimu na teknolojia katika sekta hiyo mpya.

Lugangira alisema Serikali ilitarajia kuitoa hiyo sera mpya kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa fedha 2015/2016, na sera hiyo ingezingatia ushiriki wa Watanzania na ingeweka wazi mfumo wa kisera wa ushirikishaji wazawa wengi, pia alisisitiza kuwa mikataba ya wawekezaji wa nje ingewekwa wazi.

Alisema dhamira ya serikali ni kutoa elimu kwa vijana wazawa kupitia vyuo vya Mamlaka ya Mafunzo na Ufundi stadi (VETA) ili kuwawezesha vijana kupata elimu na teknolojia itakayowapa nguvu ya kunufaika na ajira katika sekta ya gesi.

Wakati huo huo, Mshauri Mwandamizi wa Ufundi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dr. Alan Copeland alisema mafunzo yatakayoendeshwa yataweza kupunguza utegemezi wa wataalamu toka nje, hali aliyosema itaokoa fedha nyingi, alisisitiza kuwa vyuo vya VETA ni mtaji mkubwa wa kuwekeza teknolojia kwa vijana.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Dr. Hossiana Bohela alisema uchumi wa gesi iliyopo, ni lazima utafsiriwe kwa kuwapatia ajira wazawa, na akasisitiza kuwa elimu na ujuzi kwa vijana ndio msingi mkubwa wa ushirikishwaji katika viwanda vya gesi.

Dr. Bohela alisema ni wajibu kutoa elimu inayokidhi matarajio ya uzalishaji, na akaonya kuwa kutoa mafunzo nusu nusu, hasa katika matumizi ya gesi kwa ajili ya kuzalisha umeme ni hatari. 

Aliwashukuru wafadhili waliokubali kushirikiana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Wizara ya Nishati na Madini katika warsha hiyo muhimu kwa uchumi wa taifa.

Mchakato wa kutoa elimu ya teknolojia mpya inayohusu matumizi ya gesi kwa viwanda nchini ni msingi mkubwa utakaoweza kuokoa fedha nyingi ambazo zingewalipa wataalamu wa kutoka nje.

Dhamira hiyo inawezekana kutokana na ukweli kuwa asilimia kubwa ya malighati muhimu kwa viwanda vinavyotarajiwa kuanzishwa inapatikana kwa urahisi nchini.

Mwishoni mwa wiki hii, Waziri wa Madini na Nishati Prof. Sospeter Muhongo aliwahakikishia wachimbaji wadogo wa madini nchini kuwa serikali imedhamiria kuwaendeleza wachimbaji hao ili kukuza uchumi wa taifa. 

Aliwapa uhakika huo wachimbaji wa mikoa ya Simiyu a Mara kuwa serikali kwa jitihada iliyojiwekea, itahakikisha kuwa wachimbaji wadogo wananufaika ipasavyo, ingawa pia alisema wachimbaji wakubwa pia watapewa fursa ya kuwekeza katika sekta hiyo.

Kwa muda mrefu sasa wananchi wamekuwa wakiilalamikia serikali kuwa haiweki milango wazi ya nafasi za wazawa kunufaika na rasilimali zilizopo, kwamba zinawanufaisha baadhi ya wazawa wachache tu na wawekezaji wa kutoka nje.

Kwa kasi ya uwajibikaji unaojionyesha kipindi hiki cha uongozi mpya, ni dhahiri kuwa viongozi walioteuliwa kusimamia sekta mbalimbali, watahakikisha faida kubwa inayopatikana inawagusa wananchi wa kawaida kwa kuwapunguzia mzigo wa gharama za maisha.

Ninaamini mabadiliko ya kupata unafuu wa maisha hayawezi kupatikana kwa muda mfupi, ni mchakato wa muda mrefu ujao, na pia utategemea ushiriki wa dhati wa uzalishaji wa kila Mtanzania aliko.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!