MTU mmoja aliyetambuliwa kwa jina la Erasto Lwiza (27) (pichani)amemuua mama yake mzazi, Magreth Lwiza (50), kwa kumkatakata mapanga mwili wake na kuugawa vipande vidogo vidogo.
Tukio hilo limetokea juzi Mtaa wa Butiama, eneo la Vingunguti, ambapo mtuhumiwa ambaye ni marehemu kwa sasa alitekeleza unyama huo kabla hajauawa.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, kabla marehemu Erasto hajamuua mama yake alianza kumshambulia kwa visu na mapanga mwanamke aliyetambuliwa kwa jina la Mwanahamisi Masoud, ambaye alikuwa mama wa rafiki yake na kumuua hapo hapo.
Mashuhuda walieleza kuwa chanzo cha mauaji hayo ni ugomvi baina Erasto na rafiki yake, Aweso Said.
Mwandishi wa habari hizi alilifika eneo la tukio na kushuhudia dimbwi la damu eneo la jirani na alipokuwa anaishi Erasto na mama yake, huku sehemu nyingine zilizokuwa na damu zikiwa zimemwagiwa mchanga.
Akizungumza tukio hilo, msemaji wa familia aliyejitambulisha kwa jina Cornel Alphonce, alisema lilitokea juzi majira ya saa saba usiku, baada ya Erasto ambaye ni mtoto wa kwanza wa Magreth kurudi nyumbani akiwa amelewa na kumkuta Mwanahamisi akiwa nyumbani kwao anagonga mlango huku akimuita mama yake.
“Mimi nilipigiwa simu saa saba kasoro usiku na majirani, walikuwa wanapiga kelele na nilipofika waliniambia Erasto anamuua mama yake kwa kumkata mapanga,” alisema Alphonce.
Alisema baada ya kupata taarifa hizo alikwenda eneo la tukio na kukuta miili ya marehemu imeshaondolewa.
Alphonce alisema taarifa alizozipata kwa walioshuhudia mauaji hayo zilieleza marehemu Erasto alimpiga kijana aliyetajwa kwa jina la Aweso wakiwa katika mabishano ya kawaida.
Alisema Aweso alikwenda kushitaki kwa mama yake, Mwanahamisi ambapo mama huyo alikwenda nyumbani kwa kina Erasto ili kulalamikia kitendo cha mwanawe kupigwa, lakini kabla mama huyo hajafunguliwa mlango, Erasto alifika na kumvuta pembeni huku akisikika akisema ‘afadhali nimekuona, nilikuwa nakutafuta’ na kuanza kumkata kwa panga na kisu.
Alisema baadhi ya majirani ambao walikuwa wakishuhudia tukio hilo walianza kupiga kelele huku wakimtaka mama mzazi wa Erasto kutoka nje ili aweze kumuokoa mama huyo.
“Mama Erasto alipotoka alianza kumwita Erasto huku akimsihi aache kufanya tukio hilo, ndipo mwanawe alimuacha mama aliyekuwa akimshambulia ambaye alikimbia umbali mfupi kisha alianguka na kuzirai.
“Kijana alihamishia hasira kwa mama yake kwa kuanza kumshambulia huku akiwataka wananchi kubaki katika nyumba zao na kusisitiza yeyote atakayetoka atamuua,” alisema Cornel.
Alisema alimkatakata kwa mapanga na baadhi ya viungo vyake alivikata vipande vidogo vidogo kwa takribani dakika 45 huku akimnyonya damu sehemu mbalimbali za mwili wake.
Alieleza zaidi kuwa majirani ambao waliogopa kwenda kumuokoa mama huyo walipiga simu polisi, lakini kabla ya polisi kufika mmoja wa watoto wa mama huyo alifika katika kituo cha polisi jamii kilichopo eneo hilo na kuwaelezea kuwa kuna mtu alikuwa anafanya mauaji, lakini walimtaka atoe Sh 30,000 ili waweze kumsaidia.
Alisema baadaye polisi walifika eneo la tukio na kumkuta Erasto akiendelea kumkata mapanga mama yake mzazi na walipomtaka ajisalimishe alikataa na kuwataka polisi wamuache amalizie kumuua mama yake.
“Polisi baada ya kuona anakaidi amri walipiga risasi moja juu, bado muuaji aliendelea kumchinja mama yake hadi mtu mmoja alipojitokeza na kumpiga jiwe kichwani ambalo lilimuangusha chini.
“Polisi walidhani kazimia na walianza kushauriana jinsi ya kumpeleka hospitali, lakini muda mfupi tu aliamka na kuanza kukimbia. Wakati huo hakuwa na silaha, ndipo wananchi walimkamata na kuanza kumpiga huku polisi wakijitahidi kuwazuia,” alisema.
Alisema polisi walimuokoa Erasto akiwa hai na kumpeleka Hospitali ya Amana, lakini kabla ya kufika alifariki njiani.
“Miili imeharibika sana, hasa mama yake amekatwakatwa karibu atoke vipande na hapa ninavyokwambia asubuhi tumeokota vidole vitatu na kipande cha nyama, kijana amefanya tukio la kinyama mno,” alisema Cornel.
Shuhuda mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Allan Mwaisemba, alisema alishuhudia tukio hilo kupitia dirishani akiwa kitandani na alishindwa kutoka kwa sababu ana matatizo ya miguu.
Alisema wakati tukio hilo likianza alisikia sauti ya mwanamke akipiga kelele kumwita mama Erasto, lakini kipindi hicho mama huyo alikuwa bafuni anaoga.
“Baada ya kusikia kelele mama yake akatoka akiwa amevaa kitenge kimoja, lakini alipojaribu kumuita na kumsihi mwanawe asiendelee kumpiga jirani yake alimfuata na kuanza kumshambulia yeye kwa mapanga mpaka alipoanguka.
“Hapa nje walipokuwa akifanya tukio ni pembeni ya dirisha langu, huyu kijana amefanya kitendo cha kinyama, pia amefanya tukio la aibu kwa mama yake.
“Kilichonishangaza alimkalia mama yake kiunoni alafu akawa anamchoma kisu eneo la makalio, kisha anakichomoa analamba damu zinazotoka katika sehemu ile,” alisema Mwaisemba.
Kijana aliyepigwa na marehemu Erasto, alisema kabla ya kutokea kwa tukio hilo walikuwa wakinywa pombe, ndipo ghafla Erasto alianza kumkunja bila sababu na kumuingiza katika mtaro wa maji machafu.
“Hata mimi ningerudi nyumbani angeniua, alianza kunikunja na kaniangusha kwenye mtaro nikakimbia, alitubadilikia wote, nilipofika huku nikamhadithia mama, akatoka kwenda kwao lakini wakati anakwenda na mimi nilitoka nikaenda kwa rafiki zangu wanakaa bondeni,” alisema Aweso.
Alisema wakati akiongea na rafiki zake baada ya muda alisikia watu wakipiga kelele na baadaye walimfuata na kumwambia mama yake ameuawa, lakini alipofika eneo la tukio alikuta maiti zimeshaondolewa na polisi.
Katika hatua nyingine, baadhi ya majirani walidai kuwa siku za hivi karibuni Erasto alikuwa akijichanganya na makundi ya kihuni na alikuwa akivuta bangi na kunywa viroba.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Yuriki Matei, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo kwa kueleza kuwa uchunguzi umeshakamilika na miili ya marehemu imeshakabidhiwa kwa familia kwa ajili ya mazishi.
NA AZIZA MASOUD-MTANZANIA DAR ES SALAAM
No comments:
Post a Comment