Tanzania ni nchi iliyojaaliwa utajiri wa aina ya kipekee. Ukiachilia mbali mali asili zilizosheheni, Watanzania wenyewe wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha jina hili linazidi kujizolea sifa ulimwenguni.
Katika kipindi cha hivi karibu fani ya mitindo imekuwa ikitajwa kuwa miongoni mwa tasnia zinazokuja kwa kasi nchini. Tayari wabunifu kadhaa wameonyesha umahiri wao.
Kupitia fani hiyo wameweza kuitanga nchi. Wabunifu hao wamebuni mavazi kwa ajili ya watu maarufu, pia washiriki maonyesho kadha wa kadha ya kimataifa. Leo Tanzania si jina geni tena katika ulimwengu wa mitindo.
Pamoja na kazi za wabunifu hawa wapo wanamitindo walioweza kuipandisha chati Tanzania na hata kuwapa hamu watu walio nje, kutamani kuitembelea nchi hii yenye ukarimu wa kutosha?
Tausi Likokola
Huyu ni mkongwe katika tasnia ya mitindo ambaye alifanya kazi kubwa ya kuitangaza Tanzania. Hivi sasa staa huyu anaishi Marekani akifanya biashara na pia akijishughulisha na uandishi wa vitabu. The Tauch of an Angel ni kitabu chake kilichozidi kumpa umaarufu.
Likokola aliwahi kupamba majarida kadha wa kadha ya mitindo Marekani pia kushirikia katika maonyesho makubwa nchini humo. Miongoni mwa mavazi aliyowahi kuonyesha ni kutoka kwa wabunifu wenye nembo za Gucci, Escada, Tommy Hilfiger, Christian Dior na Issey Miyake.
Kwa sasa staa huyu amefanikiwa kutengeneza pafyumu yake mwenyewe aliyoizundua mwanzoni mwa mwaka huu hapa nchini.
Millen Magesse
Mshindi wa Miss Tanzania 2001. Staa huyu ni miongoni mwa wanamitindo wakongwe wanaofanya vizuri katika tasnia ya mitindo nchini Marekani na Canada.
Nyuma ya Likokola aliweza kuwavutia wanamitindo wengi na kuamini kuwa wanaweza kufika katika ngazi za kimataifa. Safari yake ya kuwa mwanamitindo wa kimataifa, ilianzia nchini Afrika ya Kusini ambapo alifanikiwa kufanya maonyesho kadhaa katika jukwaa la South Africa Fashion Week.
Millen amewahi kupamba majarida mbalimbali ya mitindo na urembo duniani jambo lililochangia kuwavutia wengi ulimwenguni. Hivi sasa anamiliki taasisi ya Millen Magese inayojishughulisha na ukuzaji wa vipaji vya wanamitindo wachanga duniani.
Flaviana Matata
Nyota yake ilianza kung’aa pale aliposhinda taji la Miss Universe mwaka 2007. Tangu hapo staa huyu amekuwa akifanya kazi mbalimbali za uanamitindo Marekani, Italia na Uingereza.
Staa huyu amepanda kwenye majukwaa kadhaa ya kimataifa akionyesha mavazi ya wabunifu wakubwa duniani. Miongoni mwa wabunifu hao ni pamoja na Vivienne Westwood, Tory Burch, Suno , Louise Gray na Alexander McQueen.
Mbali na kazi hizo Flaviana amepamba majarida makubwa ya mitindo duniani. Baadhi ya majarida hayo ni pamoja na Dazed & Confused, Glass, L’Officiel na i-D . Mbali na hilo Flaviana pia ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Flaviana Matata.
Miriam Odemba
Ni mwanamitindo wa kimataifa anayefanya shughuli zake Ufaransa na Uingereza. Amekuwa akionyesha mavazi kwenye majukwaa mbalimbali kwenye nchi hizo. Odemba ni zao la Miss Earth, taji alilopata 2008. Hadi hivi sasa staa huyo ameonyesha mitindo katika majukwaa ya London Fashion Week na Paris Fashion Week. Pia, amekuwa akipamba majarida kadhaa ya mitindo nchini humo.
Odemba kwa muda mrefu amekuwa akipamba majarida makubwa kadhaa duniani akiwavutia watu wengi wanaofuatilia mambo ya mitindo ulimwenguni. Bado anaitangaza Tanzania kwa kasi kupitia fani yake hiyo.
Rosemary Kokuhilwa
Huyu ni mtaalamu wa mitindo anayeishi Marekani. Kwa muda mrefu amekuwa akiwavalisha wanamitindo mbalimbali hususani wale wanaopanda jukwaani kuonyesha mavazi kwenye matamasha makubwa ya mitindo kama vile New York Fashion Week.
Pamoja na hilo Kokuhilwa amekuwa akifanya kazi ya kuwavalisha wanamitindo wanaofanya matangazo kadhaa ya televisheni lakini hata wale wanaofanya mitindo ya kwenye majarida kadha wa kadha ya mitindo.
Staa huyu kwa miaka kadhaa amekuwa akiandika dondoo na habari za mitindo ya urembo kupitia mtandao wake maarufu unaofahamika kama Fashionjunkii. Kokuhilwa ana mchango mkubwa kwa wanamitindo wa Kitanzania hususan wale wanaofanya kazi zao Marekani.
Hariet Paul
Ukimlinganisha na wenzake unaweza kumuweka kwenye kundi la wanamitindo chipukizi. Lakini umahiri wa kazi yake ulitosha kabisa kuiweka Tanzania kwenye ramani ya dunia.
Mwanamitindo huyu anaishi nchini Canada na amekuwa akifanya kazi zake jijini New York Marekani, London, Uingereza na Milan, Italia.
Hivi karibuni staa huyu amesaini mkataba wa vipodozi na kampuni maarufu duniani ya Calvin Klein na ametokea katika kurasa mbele za majarida mashuhuri mbalimbali kama Elle Magazine, Teen Vogue na VogueItalia.
Ni miongoni mwa warembo wanamitindo watatu waliochaguliwa katika kampeni ya kutangaza mavazi ya msimu wa joto, kutoka kwa mbunifu wa kimataifa Tom Ford.
No comments:
Post a Comment