Wednesday 2 December 2015

UZITO NA UKUAJI WA MTOTO


Mtoto mdogo anapaswa kukua na kuongezeka uzito haraka. Tangu kuzaliwa hadi umri wa miaka miwili, watoto wanapaswa kupimwa uzito mara kwa mara ili kufuatilia ukuaji wake. Upimaji wa uzito wa mara kwa mara ukionyesha kuwa mtoto haongezeki uzito, au wazazi na walezi wengine wanaona mtoto hakui, ifahamike kuwa kuna tatizo. Mtoto huyo anapaswa kuchunguzwa na mtaalamu wa afya.

Kuongezeka uzito ni dalili muhimu sana kwamba mtoto ana afya njema na anakuwa na kukomaa vizuri. Tangu kuzaliwa hadi umri wa mwaka mmoja, mtoto mchanga anapaswa kupimwa uzito angalau mara moja kila mwezi. Kuanzia umri wa mwaka 1 hadi miaka 2, watoto wadogo wanapaswa kupimwa uzito angalau mara moja kwa kila miezi mitatu. Kila mtoto mdogo anapopelekwa katika kituo cha afya, anapaswa kupimwa uzito. Hatua hii inasaidia kugundua mapema endapo kuna matatizo ya ukuaji ili hatua zinazostahili ziweze kuchukuliwa.


 Uchunguzi wa afya unaweza pia kugundua iwapo mtoto anaongezeka uzito haraka sana kuliko inavyostahili kwa mujibu wa umri wake. Hali hii inahitaji kumchunguza mtoto kuhusiana na urefu wake, ili kuamua iwapo mtoto ana uzito mkubwa zaidi kuliko inavyostahili. Iwapo mtoto ana uzito mkubwa kuliko umri wake, ni muhimu kuchunguza mlo wa mtoto na kuwapa wazazi au walezi wengine wa mtoto ushauri kuhusu lishe nzuri kulingana na umri wa mtoto.

 Kuna ongezeko kubwa la watu wanaopata chakula pungufu au kingi kupita kiasi katika familia. Kwa kawaida, mtoto anayenyonyeshwa maziwa ya mama pekee kwa miezi sita ya mwanzo hukua vizuri katika kipindi hiki. Unyonyeshaji maziwa ya mama husaidia kuwalinda watoto dhidi ya magonjwa ya kawaida na kuwahakikishia ukuaji bora wa kimwili na kiakili. Watoto wachanga wanaonyonyeshwa maziwa ya mama hujifunza haraka zaidi kuliko watoto wachanga wanaolishwa aina nyingine za maziwa. Katika umri wa miezi sita, mtoto anapaswa kuanza kula vyakula vya kulikiza vyenye virutubisho muhimu, pamoja na kunyonyeshwa maziwa ya mama ili kuhakikisha ukuaji wenye afya. Kila mtoto anapaswa kuwa na chati ya ukuaji inayofuatilia ukuaji wake. 


Chati hiyo inaweza kuonyesha iwapo mtoto anakua vizuri kulingana na umri wake. Kila anapopimwa, uzito wa mtoto lazima uwekewe alama ya nukta kwenye chati ya ukuaji na nukta hizo ziunganishwe kwa mstari. Uunganishaji huu wa nukta utaunda mstari unaoonyesha hali ya ukuaji wa mtoto. Iwapo mstari utaelekea juu, mtoto atakuwa anakua vizuri. Mstari unaoendelea kuwa sambamba au kuelekea chini hudokeza hali inayohitaji uchunguzi. Watoto wanapaswa si tu kuongezeka uzito bali pia urefu unaostahili. 


Urefu wa mtoto pia huonyeshwa katika chati. Lishe bora, matunzo, na usafi, hususani katika miaka miwili ya mwanzo tangu kuzaliwa, ni muhimu sana ili kuepusha mtoto kuwa mfupi sana kuliko umri wake (udumavu). Kama mama anapata lishe duni, au hapati lishe inayostahili wakati wa ujauzito, mtoto wake mchanga anaweza kuzaliwa akiwa mdogo mno. Hali hii humweka mtoto mchanga katika hatari ya udumavu hapo baadaye. 

Watoto wachanga wenye uzito mdogo wanahitaji uangalizi na matunzo ya ziada ili waweze kukua kikamilifu baada ya kuzaliwa. Mtoto asiyeongezeka uzito wa kutosha kwa kipindi cha mwezi mmoja au miwili, anaweza kuhitaji huduma kubwa zaidi, chakula chenye lishe nying zaidi, au milo ya mara kwa mara. 

Mtoto anaweza kuwa mgonjwa au anaweza kuhitaji uangalizi na matunzo ya karibu zaidi au kusaidiwa kulishwa na mlezi. Wazazi na wataalamu wa afya wanapaswa kutoa huduma haraka ili kugundua chanzo cha tatizo na kuchukua hatua za kutatua tatizo husika.

 Ili kusaidia kubainisha tatizo, yafuatayo ni maswali muhimu ya kuuliza: -

 Je, mtoto anakula mara kwa mara inavyopasa?

 Pamoja na kunyonyeshwa maziwa ya mama, mtoto mwenye umri kati ya miezi 6 na 8 anahitaji kula mara 2 hadi 3 kwa siku, na mara 3 hadi 4 kwa siku baada ya hapo. Vyakula vyenye virutubisho vya ziada kama vile kipande cha tunda au mkate na siagi (ya karanga) vinaweza kuhitajika mara 1 au 2 kwa siku. 

Mtoto mwenye mtindio au ulemavu anaweza kuhitaji msaada na muda wa ziada kumlisha

. - Je, mtoto anapata chakula cha kutosha? Mtoto mwenye umri wa miezi 6 hadi 8, mwanzoni anapaswa kupata vijiko vya chakula 2 hadi 3, huku vikiongezeka taratibu hadi kufikia nusu kikombe chenye ujazo wa mililita 250 wakati wa kila chakula. Watoto wenye umri wa miezi 9 hadi 12 wanahitaji kupata nusu kikombe chenye ujazo wa mililita 250 katika kila mlo, wakati watoto wenye umri kati ya miezi 12 na 23 wanahitaji robo tatu hadi kikombe kimoja chenye ujazo wa mililita 250 cha chakula kinacholiwa na familia katika kila mlo. Watoto wenye umri wa miaka miwili na zaidi wanapaswa kupewa angalau kikombe kizima chenye ujazo wa mililita 250 katika kila mlo. 

Akimaliza chakula chake na akahitaji zaidi, mtoto huyo anapaswa kupewa zaidi.

 - Je, milo ya mtoto ina vyakula vichache mno vya ‘ukuaji’ au ‘vya kuongeza nguvu’?Vyakula vinavyowasaidia watoto kukua ni maharage, jamii ya karanga, nyama, samaki, mayai, bidhaa za maziwa, nafaka, na jamii ya kunde. Ujumuishaji wa vyakula vyenye asili ya wanyama katika mlo ni muhimu sana. Kiasi kidogo cha mafuta kinaweza kuongeza nguvu. Mafuta mekundu ya mawese au mafuta ya kula yaliyoongezewa vitamini ni vyanzo vizuri vya vyakula vinavyoongeza nguvu.

Vyakula bora vya ‘ukuaji’ ni muhimu ili kuhakikisha kuwa watotowanaongezeka uzito na urefu unaotosha. Vyakula vinavyoongeza nguvu lakini havina vitamini na madini, na virutubisho vingine muhimu (kama vile vyakula vilivyosindikwa vyenye mafuta mengi au vyakula vyenye sukari) vinaweza kusababisha watoto kuongezeka uzito kupita kiasi bila uwiano na ongezeko la urefu.

 - Je, mtoto anakataa kula? Kama mtoto anaonekana kutopenda ladha ya aina fulani ya chakula, apewe vyakula vingine. Aanze kupewa vyakula vingine taratibutaratibu.

 - Je, mtoto ni mgonjwa?Mtoto mgonjwa anahitaji kuhimizwa kula milo midogo ya mara kwa mara. Baada ya ugonjwa, anahitaji kula chakula kingi kuliko kawaida ili kuongeza na kurejesha nguvu na virutubisho vilivyopotea kutokana na ugonjwa. Kama anaumwa mara kwa mara, mtoto huyo anapaswa kuchunguzwa na mtaalamu wa afya. 

Je, mtoto anapata vyakula vya kutosha vyenye vitamini A? Maziwa ya mama yana vitamini A za kutosha. Vyakula vingine vyenye vitamini A ni maini, mayai, bidhaa za maziwa, mafuta mekundu ya mawese, matunda ya rangi ya njano na ya chungwa, na mbogamboga. Kama vyakula hivi havipatikani kwa kiasi cha kutosha, mtaalamu wa afya anaweza kumpa mtoto dawa za vitamini A (vidonge au dawa ya maji) kila baada ya miezi 4 hadi 6. 

Je, mtoto analishwa maziwa ya kawaida kwa kutumia chupa? Kama mtoto ni mdogo chini ya miezi 6, ni vizuri akanyonyeshwa kwa maziwa ya mama tu. Kuanzia miezi 6 hadi 24, maziwa ya mama yanaendelea kuwa maziwa bora kwa sababu yana virutubisho vingi. Kama atapewa aina nyingine za maziwa, anapaswa kunyweshwa kwa kutumia kikombe safi na salama badala ya chupa.

 - Je, chakula kinatunzwa katika mazingira safi na salama? Kama si hivyo, mtoto ataumwa mara kwa mara. Vyakula vibichi vinapaswa kuoshwa kwa maji safi kutoka katika chanzo salama. Vyakula vilivyopikwa vinapaswa kuliwaa mara moja baada ya kupikwa. Chakula kilichobaki (kiporo) kitunzwe vizuri na kipashwe moto vizuri kabla ya kuliwa. 

-Je, maji yanahifadhiwa vizuri? Maji safi na salama ni muhimu sana kwa afya ya mtoto. Maji yanapaswa kutoka katika chanzo salama na kutunzwa kwa usafi kwa kuhifadhiwa katika vifaa vilivyofunikwa, ambavyo ni safi ndani na nje. Maji safi ya kunywa yanaweza kupatikana kutoka kwenye mabomba, mabwawa, visima vya umma, chemchem zinazotunzwa, au maji ya mvua yaliyovunwa. Kama maji yanachotwa kutoka kwenye mabwawa, vijito, na chemchem zisizolindwa, visima, au matanki, yanapaswa kusafishwa kwa kuwekwa dawa. 

Usafishaji wa maji unaofanyika majumbani unaweza kufanywa kwa kuchemshwa, kuchujwa, kuweka shabu , au kuondoa vijidudu kwa kuanika juani kwa kuzingatia taarifa zilizotolewa na mtaalamu wa afya.

 - Je, choo kinatupwa katika choo cha shimo, choo cha kusukuma kwa maji, au hufukiwa chini? Je, mikono huoshwa kwa sababu na maji au mbadala wake kama vile jivu na maji baada ya kutoka chooni? Kama hapana, mtoto anaweza kupata minyoo na magonjwa mengine mara kwa mara. Mtoto mwenye minyoo anapaswa kupewa dawa ya minyoo na mtaalamu wa afya. - Je, mtoto mdogo anaachwa peke yake muda mwingi au chini ya uangalizi wa mtoto mkubwa? Kama ndiyo, mtoto mdogo anaweza kuhitaji uangalizi na kuwa karibu zaidi na watu wazima, hususani wakati wa kula.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!