Thursday, 10 December 2015

TAASISI YA MKAPA YATAKA ITENGWE SIKU MAALU YA USAFI


Taasisi ya Mkapa (Mkapa Foundation) imetoa wito kwa mashirika, taasisi, majiji, manispaa na halmashauri mbalimbali nchini kuwa na utaratibu wa kutenga siku maalumu ya usafi, kwa lengo la kuimarisha afya za wananchi na kutokomeza magonjwa yasababishwayo na uchafu kama kipindupindu. 


Wito huo ulitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Rasilimali Watu na Utawala wa taasisi hiyo, Irene Kyara, katika mahojiano maalumu na Nipashe, baada ya shughuli ya usafi  iliyofanywa na wafanyakazi wa taasisi hiyo kwenye Zahanati ya Kawe. Kyara alisema wafanyakazi wa taasisi hiyo waliamua kufanya usafi katika zahanati hiyo kama sehemu ya kuitikia agizo la Rais John Magufuli, aliyetaka Watanzania waitumie Siku ya Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Uhuru Desemba 9 kufanya usafi wa mazingira ili kupambana na ugonjwa wa kipindupindu.
 
“Tukiwa wadau wa sekta ya afya tunapongeza agizo la Rais Magufuli la kuwataka Watanzania waitumie siku hii ya Uhuru kufanya usafi wa mazingira kote nchini, lakini ni vizuri sasa wadau wote kuanzia mashirika, taasisi, majiji, manispaa na wananchi tukaweka siku maalumu ya usafi badala ya kusubiri Desemba 9,” alisema.
 
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Kamati ya Afya ya Zahanati ya Kawe, Hilda Rwebangira, aliwataka wananchi kutosubiri agizo la Rais katika kutimiza wajibu wao wa kila siku, ikiwa  ni pamoja na usafi wa mazingira wa maeneo wanayoishi na kufanya kazi kwa bidii.
 
“Tunapaswa kuona aibu kwa hilo, kwani tunaweza kutimiza wajibu wetu kama tulivyofanya leo (jana), ambapo jiji letu linaonekana safi sasa na ndiyo maana napeleka pendekezo kwenye bodi yangu ili kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi iwe ni siku ya usafi kwenye zahanati yetu,” alisema.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!