Waziri wa Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga, amekutana na Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza, Ikulu jijini Bujumbura nchini Burundi.
Anachukua hatua hiyo kufuatia maagizo ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (JAM) Rais John Magufuli, kuchukua jukumu la kutafuta suluhu ya kisiasa ya migogoro iliyojitokeza baina ya serikali na vikundi vinavyohatarisha amani nchini humo.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje, Ushirikiano Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa,iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana ilisema, katika mazungumzo hayo Waziri Mahiga alimueleza Rais Nkurunziza azma ya Rais kuanzisha mazungumzo ya kisiasa ya kuleta amani.
Kadhalika alielezwa kuwa msuluhishi aliyeteuliwa na JAM, Rais Yoweri Museveni ameanza maandalizi ya uzinduzi wa mazungumzo hayo. Iliongeza kuwa yatafanyika Entebe nchini Uganda kuanzia Jumatatu ijayo. Dokta Mahiga pia alieleza maoni yake kuhusu hali ya utulivu aliyoiona kwa kipindi cha takriban saa 24 alizokuwa jjijini Bujumbura na kwamba hakusikia sauti za milipuko wala silaha zozote.
Rais Nkurunziza alimshukuru mjumbe huyo wa Rais Magufuli nakumhakikishia ushiriki wa Burundi akieleza kuwa mazungumzo ya Entebe yatasaidia kuleta amani na mshikamano baina ya wananchi wa Burundi Hata hivyo Rais Nkurunziza taarifa ilisema alisisitiza kuwa ili mazungumzo hayo yawe na tija ni lazima yawe muendelezo wa mazungumzo ya ndani bayo yeye na serikali yake wamekwisha yaanza.
Aliongeza kuwa ana matumaini kuwa makundi yote nchini humo yataungana kwenye mazungumzo hayo yatakayojumuisha asasi za kiraia, kidini, vyama vya siasa ili kujadili mustakabali wa taifa lao kwa pamoja na kuridhia ushiriki wa Burundi kwenye mchakato huo wa JAM.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment