Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amesema watu wanaomiliki mashamba bila kuyaendeleza huku wakiyatumia kama dhamana ya kukopea fedha benki watanyang’anywa.
Lukuvi, akizungumza kwa mara ya kwanza baada ya kuripoti kazini jana pamoja na naibu wake, Angelina Mabula, alisema kuna watu wamehodhi mashamba makubwa lakini hawayaendelezi, hawayalipii kodi, na mbaya zaidi wanayatumia kukopa fedha benki.
“Mkuu wa idara anayehusika na ardhi ninaomba Jumatatu ijayo orodha ya watu tuliowapa ardhi lakini wameitumia kuombea mikopo ambayo wanaitumia kwa shughuli nyingine. Hao nitalala nao mbele,” alisema Lukuvi baada ya kujitambulisha kwa wakuu wa idara za wizara hiyo.
“Nipeni pia orodha ya watu wanaotakiwa kulipa kodi ya ardhi lakini hawalipi na tukikutana wiki ijayo nielezeni taratibu zinazotakiwa kuchukuliwa dhidi yao,” alisisitiza.
Akisisitiza kuhusu hilo, Lukuvi alisema wiki ijayo atakwenda kuchukua shamba lililohodhiwa na mwekezaji lenye ekari 1,600 huko Mbarali mkoani Mbeya na kuwarudishia wananchi.
Japokuwa Lukuvi hakumtaja mwekezaji atakayenyang’anywa shamba hilo wilayani Mbarali, lakini shamba la ukubwa huo lililokuwa na mgogoro kwa muda mrefu ni la Kapunga.
Akiwa kwenye kampeni mkoani Mbeya, mgombea urais wa CCM ambaye sasa ni Rais John Magufuli, aliahidi kurejesha shamba hilo kwa wananchi ili kumaliza mgogoro wa muda mrefu.
Aidha, Lukuvi aliwaagiza maofisa hao kuwasiliana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ili kuangalia wawekezaji waliopewa ardhi kama wanaitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Tukikutana Jumatatu ijayo nipewe taarifa za kila mwekezaji na ukubwa wa ardhi aliyopewa; aliomba kwa madhumuni gani, na je, anaitumia ardhi hiyo kwa madhumuni aliyoombea?” alihoji.
Kuhusu upimaji wa ardhi, Lukuvi alisema asilimia 10 ya ardhi nchini ndiyo imepimwa na kwamba juhudi zinahitajika ili kupima ardhi zaidi. Tunataka tukikutana wiki ijayo, ofisa anayehusika na upimaji aje na mpango wa upimaji ardhi na umilikishaji na atueleze utagharimu kiasi gani ili tuweze kuona serikali itawekeza vipi katika upimaji wa ardhi nchi nzima,” alisema.
Kuhusu ujenzi wa nyumba za kupangisha, Lukuvi alisema kumeibuka kampuni nyingi zinazofanya biashara ya kujenga nyumba kubwa na kuzipangisha lakini hakuna chombo chochote cha serikali kinachosimamia sekta hiyo.
“Hii ni biashara kubwa ambayo inakua siku hadi siku, hivyo ni lazima sasa wizara isimamie kwa kuweka chombo maalumu. Hivi sasa biashara inafanyika lakini hatupati kodi kwa sababu si rasmi,” alisema.
Waziri Lukuvi alimtaka mkurugenzi wa nyumba wa wizara hiyo kuandaa mpango wa namna ya kuwasaidia watu maskini ili kuwa na nyumba bora. “Tunataka atueleze serikali ifanye nini ili kuwasaidia wananchi maskini kuwa na nyumba bora ili waondokane na nyumba zilizoezekwa kwa nyasi,” alisema.
Bajeti ya 2015/16
Waziri Lukuvi amewaagiza wakuu wote wa idara kuwasilisha taarifa za matumizi ya fedha kuanzia Julai 1, 2015 hadi sasa na utekelezaji wa mipango mbalimbali.
Alisema kila mkuu wa idara awasilishe kwenye kikao hicho ripoti inayoonyesha malengo ya idara yake na fedha zilizotengwa na matumizi yake.
MWANANCHI.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment