Monday 9 November 2015

ZANZIBAR WAPENDEKEZA ZEC IVUNJWE KABLA YA KURUDIA MATOKEO

Image result for vote hand

Baadhi ya wananchi katika manispaa ya  Zanzibar wamesema Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), inapaswa kuvunjwa kabla ya marudio ya uchaguzi.



Wito huo wameutoa walipokuwa wakizungumza na Nipashe Jumapili, mjini hapa jana kwa nyakati tofauti siku chache baada ya Mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi (Zec) Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi kwa madai haukuwa huru na wa haki.

Aboud Salim, mkaazi wa Mkunazini alisema  wananchi wamepoteza imani Zec chini ya mwenyekiti wake na badala yake wametaka kuundwe tume huru ya kusimamia uchaguzi huo.

Alisema tangu mwanzo Zec ilionekana uwezo wake mdogo baada ya watu wengi kuandikishwa kuwa wapigakura na kupewa stakabadhi badala ya shahada za kupigia kura.

“Kuundwe tume huru ya uchaguzi kabla ya kufanyika uchaguzi wa marejeo, hatuna imani na tume hiyo,” alisema Aboud.

Alisema, wakati umefika wa kuletwa majaji kutoka Jumuiya ya Madola waje kusimamia uchaguzi wa marudio ili kurudisha imani ya wananchi kufuatia kuvurugika uchaguzi wa awali visiwani hapo.

Saidi Juma Khatib, mkaazi wa Bububu Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, alisema kama wajumbe wa Tume wamefikia kuvua mashati na kupigana kwa kutetea maslahi ya vyama, wamepoteza sifa za kuendelea kubaki ndani ya chombo hicho.

Asha Kombo, mkaazi wa Chumbuni alisema inashangaza kuona mpaka sasa hakuna watu waliofikishwa katika vyombo vya sheria pamoja kuwepo kwa taarifa za kuhujumiwa uchaguzi na baadhi ya watendaji wa Tume ya Uchaguzi.

Alisema, kama kuna watu wamehujumu uchaguzi kwa maslahi yao binafsi, vyombo vya dola vinatakiwa kuchukua hatua za kisheria kutokana na kitendo hicho kuchafua hali ya kisiasa pamoja na kusababisha hasara kubwa kwa kwa serikali.

Hata hivyo Abdalla Fadhil Khatib, mkaazi wa Kikwajuni, alisema ufumbuzi pekee wa kumaliza mgogoro wa uchaguzi matokeo ya uchaguzi wa awali yahakikiwe na kama kuna kasoro zirekebishwe na kumtangaza mshidi badala ya kufuta matokeo.

Waalisema kama kuna vitendo vya udanganyifu vilivyofanyika katika majimbo yatakayothibitika, uchaguzi urudiwe na sio kufuta matokeo yote.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!