Manispaa ya Kinondoni kwa
kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi , kama
msimamizi na mtekelezaji wa sera ya Taifa ya Ardhi, inakusudia kuendesha
zoezi la kubomoa nyumba zilizojengwa bila kufuata taratibu za ujenzi.
Maeneo yaliyotengwa mijini kwa matumizi ya umma ikiwa ni pamoja
na maeneo ya wazi, njia za miundombinu na huduma nyinginezo za umma,
mara kwa mara hutumiwa vibaya au kuvamiwa na waendelezaji binafsi hivyo
kuukosesha umma manufaa yaliyokusudiwa.
Tamko Na. 6.6.1 la Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995:
i. Serikali itahakikisha kwamba maeneo yote mijini yaliyotengwa
kwa shughuli za umma yanatumika kwa shughuli zilizokusudiwa na
yanalindwa ili yasivamiwe.
Tamko Na. 8.2.1 la Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995:
ii. Serikali za mitaa zitawajibika kushirikiana na Wizara ya Ardhi kuhakikisha usimamizi mzuri wa ardhi katika maeneo yao.
Sera ya Taifa ya Ardhi imebainisha sababu inayopelekea Wizara
kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni kuendesha zoezi hili la ubomoaji.
Ubomoaji huu utahusisha nyumba zote zilizojengwa
a) Bila kibali cha ujenzi
b) Bila kufuata michoro ya mipango miji
c) Bila kufuata matumizi ya ardhi (maeneo ya wazi)
Zoezi hili la ubomoaji litaendeshwa na Manispaa ya kinondoni na
Wizara ya Ardhi itasimamia sera za ardhi na taratibu za uendelezaji
kuhakikisha zinafuatwa na kila mmiliki wa ardhi.
Maeneo ambayo ujenzi wake umekiuka matumizi kusudiwa na
yatahusika na ubomoaji huu ni Mbezi, Tegeta, Bunju, Mwenge na Kinondoni –
Biafra. Kazi hii inatarajiwa kufanyika kwa siku tatu kuanzia jumatano
tarehe 18/11/2015 hadi ijumaa tarehe 20/11/2015.
No comments:
Post a Comment