Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, amesema muda wake wa urais utaanza rasmi muda mfupi kuanzia sasa, baada ya kuapishwa kutokana na ushindi aliupata katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Alisema wakati ukifika watamuapisha tu, na wajue muda wake wa urais utaanza siku atakayoapishwa kwa mujibu wa Katiba.
Maalim Seif aliyasema hayo jana alipokuwa akihutubia mkutano ambao ulioandaliwa kwa ajili ya viongozi wa wilaya, majimbo na matawi kisiwani Pemba uliofanyika katika ofisi za uchaguzi za CUF kisiwani humo.
Maalim Seif aliwataka wananchi kisiwani Pemba watembee kifua mbele kwa sababu ni suala la muda tu kabla hajatangazwa kuwa mshindi wa urais wa Zanzibar na kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Nane.
Alisema wanachofanya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hivi sasa ni kuchelewesha muda, lakini kwa kuwa wananchi wa Zanzibar wamemchagua yeye kuwa Rais na Dunia nzima inafahamu hilo, hatimaye watamwita wenyewe na kumuapisha kuwa Rais wa Zanzibar.
“Wananchi wa Pemba kuleni mshibe, laleni bila ya hofu na tembeeni kifua mbele, hawana njia, lazima watakubali maamuzi ya wananchi wa Zanzibar walionichagua niwe Rais wao,” alisema Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Alisema jambo linalowatia kiwewe CCM na kutoa visingizio kuhusiana na kura za Pemba ni kutokana na fedha nyingi walizotumia kwa lengo la kupata majimbo kadhaa.
Alisema CCM wamesahau kuwa miaka yote hawapati majimbo kisiwani Pemba na uchaguzi wa mwaka huu haikuwa ajabu kukosa kukosa viti vyote vya ubunge, uwakilishi na udiwani.
“Viongozi wa CCM walimdanganya sana Dk. Shein kuwa watapata viti Pemba na kura za kutosha za Rais, wametumia fedha nyingi katika uchaguzi huu, lakini walisahau hali halisi ya Pemba na sasa wanahangaika,” alisema Maalim Seif ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CUF.
Alidai kuwa zipo taarifa kuwa kiasi cha Sh. milioni 70 zilitumiwa na CCM katika jimbo moja la Mtambwe, ambalo katika chaguzi zote zilizofanyika chama hicho hakijawahi kupata kura zaidi ya asilimia tano.
Aidha, Maalim Seif aliwapongeza mawakala wa CUF katika majimbo yote 54 ya Zanzibar kutokana na walivyolinda kura za chama chao na kukiwezesha kupata ushindi mkubwa ambao hakikuwahi kuupata kwa upande wa Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema uchaguzi mkuu uliofanyika kisiwani Pemba mwaka huu ni mfano mzuri wa uchaguzi uliokuwa huru na wa haki nchi nzima.
Mazrui alisema wale wanaodai kuwa kura zimezidi kisiwani humo ni waongo wanaotapatapa kwa sababu kuna watu waliojiandikishwa zaidi ya 20, 000 hawakupiga kura na waliojitokeza kupiga kura ni 119,000.
Matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar yalifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec), Jecha Salim Jecha, Oktoba 28 wakati matokeo yakiendelea kutangazwa akidai kuwa kulikuwapo na kasoro kadhaa.
Kabla ya hatua hiyo, Maalim Seif alijitokeza na kutangaza hadharani idadi ya kura alizozipata kutokana na matokeo aliyoyapokea kutoka vituoni.
NIPASHE.
No comments:
Post a Comment