RAIS John Magufuli amepongezwa kwa kasi ya utendaji kazi anayoionesha, inayoelezwa kuwa inadhihirisha dhamira ya dhati na ya kizalendo aliyonayo ya kuwatumikia Watanzania.
Aidha, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) imeanza utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa juzi na Rais Magufuli, yakiihusu MNH pamoja na Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI).
Mbali ya pongezi kwa Dk Magufuli, baadhi ya wananchi wamewabeza watu wanaodai kwamba kasi hiyo ni nguvu ya soda, wakimtaka Rais asivunjike moyo na ajue wananchi wengi wanafarijika kwa namna alivyoanza kazi na kumtaka aongeze juhudi kurejesha uadilifu na utendaji bora hasa katika ofisi za serikali.
Wananchi hao walitoa maoni yao kwa nyakati tofauti katika kipindi cha siku tano za kuanza kazi rasmi Dk Magufuli, walipozungumza na waandishi wa habari wa gazeti hili wa Dar es Salaam, Dodoma na Kahama.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Amani kwa Waislamu ya Islamic Peace Foundation (TIPF), Sadiki Godigodi alisema Dk Magufuli anafanya kazi kwa vitendo na kwamba utendaji huo wa kasi siyo wa nguvu ya soda, kwani ndivyo alivyofanya wakati wote alipokuwa waziri, hivyo watendaji wazembe wasitegemee kasi hiyo kupoa.
Godigodi alisema kwa siku chache alizokaa Ikulu, ameonesha mwanzo mzuri kwa kukutana na watendaji wa Wizara ya Fedha na makatibu wakuu ambao hakika amewapa maelekezo ya serikali yake anavyotaka iwe.
Alisema katika ziara yake ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili amechukua hatua stahili ili Bodi mpya aanze kazi kwa kiasi anayotaka. Mwenyekiti huyo amemtaka kufanya hivyo sehemu nyingine zenye uzembe.
Alisema kitendo cha Rais Dk Magufuli kutaka kulipa fedha ya matibabu kwa mgonjwa (alipotembelea Muhimbili juzi) kimeonesha jinsi alivyoguswa na matatizo ya pale hospitalini na anavyomwamini Mungu.
Naye mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam, Fred Kazimoto alisema utendaji huo wa Magufuli ni salamu kwa watendaji wa serikali waliozoea kufanya kazi kwa uzembe na kwamba kama hawawezi kubadilika ni vyema kuachia ngazi sasa.
Alisema kutembelea Muhimbili na kuzungumza na wagonjwa kunaonesha dhamira yake ya kutenda kazi kwa manufaa ya wananchi na siyo watendaji, kwani angekuwa kiongozi mwingine, angezungumza na watendaji kisha akaondoka bila kuzungumza na wagonjwa.
Naye Caroline Mbayo alimtaka Rais Magufuli kuhakikisha anateua Waziri Mkuu na mawaziri watakaoendana na kasi yake kwani akipata wazembe hawatamsaidia kufikia malengo yake. “Kwa kweli nimeridhishwa na kasi hii.
Akiendelea ninaanza kuwa na imani na serikali, tunaomba ashughulikie na sekta nyingine za umma kwani baadhi ya watumishi wamejisahau kabisa,” alisema mkazi wa Mbezi Kwa Yusufu, Ezekieli Jonasi.
Naye mwendesha bodaboda na mkazi wa Mbezi Luis, Alfred Lashau, alisema ana imani na Dk Magufuli na anaamini kwa kasi hiyo, rushwa itapungua serikalini. Wakazi wengine walimuomba Rais kutupia jicho Shirika la Umeme (Tanesco) huku wakiamini huenda kuna hujuma katika shirika hilo, kwani pamoja na ahadi ya umeme kwamba hautokatika mara kwa mara, hali hiyo inaendelea.
Mkazi wa Tegeta, Salome Abbasi, kwa upande wake, alimpongeza Dk Magufuli kwa namna alivyoanza utendaji wake, kwamba tangu aapishwe ameonesha ni kiongozi anayejali maslahi ya wananchi wake zaidi.
Naye Jeffrey Mshana ambaye ni wakili mwanafunzi, alisema Rais huyo, tayari amegusa maeneo muhimu ambayo ni fedha na afya, lakini bado anahitajika aguse maeneo mengi zaidi kama vile shule za umma, hospitali za wilaya, Bandari, reli, ofisi na mashirika ya umma na Polisi hasa Kitengo cha Usalama Barabarani ambako bado utendaji wake hauridhishi.
Mkazi ambaye hakuwa tayari kuandikwa jina lake gazetini alisema yeye anaunga mkono Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), lakini anaamini kasi ya mabadiliko ya kweli ya Dk Magufuli, yataleta faida.
“Hii ni nguvu ya povu la pombe maana huwa halikatiki tangu unapoanza kunywa bia, yaani hapa kazi tu. 2020 Magufuli atapita uchaguzi bila kupingwa kutokana na utendaji wake,’’ alisema Benedictor Peter.
Pamoja na kumpongeza, wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama mkoani Shinyanga wamemwomba Dk Magufuli kuagiza kuondolewa kwa maduka ya dawa yaliyopo jirani na hospitali ya wilaya ili kuwezesha wagonjwa kupata huduma stahiki hospitalini.
Wananchi hao walisema juzi kwa nyakati tofauti kuwa, endapo maduka hayo ya dawa yataondolewa wananchi wa hali ya chini watapata huduma zote hospitalini badala ya kuagiziwa kwenye maduka hayo binafsi ambayo mengi walisema yanamilikiwa na maofisa tiba wa hospitali hiyo.
Mjini Dodoma, wananchi wametaka watendaji wa wilaya na mikoa nchini kwenda na kasi aliyonayo Magufuli. Mkazi wa Dodoma, Abdurahman Gombati alisema utendaji wa Rais Magufuli unaonesha nia yake ya dhati kwa nini aligombea urais wa Tanzania.
“Hii inaonesha dhamira ya kweli ya kuwatoa watanzania kwenye hatua moja kuelekea nyingine na kitachotakiwa ni kumpa ushirikiano wa kila namna ili aweze kufanikisha azma yake,” alisema Gombati.
Alisema sasa ni wajibu kwa wakuu wa mikoa na wilaya nao kuiga anachofanya mkubwa wao ili utendaji huu ushuke hadi ngazi ya chini na wananchi kuhakikisha wanawafichua watendaji wanaokwamisha huduma za jamii badala ya kumsubiri Magufuli kwani rais hawezi kufika kila mahali.
“Kila mtendaji anatakiwa kumuunga mkono ili asihangaike mwenyewe bali aungwe mkono na watendaji walio wa ngazi za mkoa, wilaya, tarafa, kata na hata vijiji,” alisema mkazi wa Miuji, Prosper Ganjala.
Katika hatua nyingine, utekelezaji wa maagizo ya Dk Magufuli umeanza katika MNH na MOI; miongoni mwa utekelezaji wa maagizo hayo ni kufanyia matengenezo kwa mashine za MRI na CT Scan pamoja na kumfanyia vipimo mgonjwa Chacha Makenge ambaye rais alijitolea kugharamia matibabu yake.
Katika hatua nyingine inayoonesha utekelezaji huo, ni kuripoti kazini kwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Profesa Laurence Mseru ambaye baada ya kuripoti, alifanya kikao cha pamoja na wakuu wa idara za hospitali hiyo.
Ofisa Uhusiano wa MNH, Aminiel Aligaesha alithibitishia kuanza kazi kwa Profesa Mseru pamoja na kikao alichofanya ambapo amemkariri akiomba ushirikiano kwa watu wote ili kufikia malengo ya taasisi.
Alisema Profesa Mseru ameanza kushughulikia suala la matengenezo ya mashine za MRI na CT Scan, ambazo zimeamriwa kutengemaa ndani ya wiki. Aligaesha alisema tayari Kaimu Mkurugenzi Mtendaji huyo ameshawasiliana na Kampuni ya Philips ambao ndio hufanyia matengenezo mashine hizo na wameahidi kuanza kazi mara moja.
Meneja Ustawi wa Jamii na Uhusiano wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa, Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu (MOI), Almas Jumaa alisema tayari taasisi hiyo imeanza kusimamia kwa karibu matibabu ya kijana, Chacha Makenge aliyelazwa katika wodi ya Sewa Haji 17 kwa kuvunjika uti wa mgongo.
“Tayari Makenge leo (jana) saa 5:00 asubuhi alipelekwa kufanyiwa vipimo na majibu yake yanaweza kupatikana wakati wowote kuanzia leo ili matibabu yake yaendelee,” alisema Jumaa.
Jumaa pia amepongeza ziara hiyo ya Rais kwa kusema inamfanya kujifunza namna taasisi zake zinavyofanya kazi pamoja na kujionea mwenyewe changamoto ambazo hospitali za rufaa kama hiyo ya Muhimbili zinakabiliana nazo.
Aidha baadhi ya wagonjwa hospitalini hapo wamesema tangu kupita kwa Rais Dk Magufuli juzi hali ya huduma hospitalini hapo imebadilika tofauti na awali. Habari hii imeandikwa na Mroki Mroki, Gloria Tesha, Halima Mlacha, Theopista Nsanzugwanko, Fransisca Emmanuel, Dar es Salaam na Raymond Mihayo, Kahama, Sifa Lubasi, Dodoma.
No comments:
Post a Comment