Thursday, 26 November 2015

PAPA FRANCIS AWASILI KENYA KUANZA ZIARA

Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis (kulia) akipunga mkono kusalimia wananchi wa Kenya baada ya kuwasili kwenye Uwanja kodi kutoka kwa wafanyabiashara wa Ndege wa Jomo Kenyatta, Nairobi jana kuanza ziara ya nchi tatu za Afrika. Kulia kwake ni Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta na mke wake Margaret. (Picha na AFP).
KIONGOZI wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amewasili nchini Kenya jana jioni kuanza ziara ya kihistoria ya siku sita barani Afrika. 


Akiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini hapa, alipokewa na mwenyeji wake, Rais Uhuru Kenyatta aliyefuatana na mkewe Margaret pamoja na Naibu Rais, William Ruto pamoja na viongozi mbalimbali wa Kanisa Katoliki nchini humo.

Aidha, vikundi mbalimbali vya ngoma na kwaya vilijipanga uwanjani hapo na kuimba nyimbo mbalimbali za furaha na shangwe katika mapokezi hayo ya aina yake. Saa 10:30 jioni ndege iliyombeba Papa Francis, mali ya shirika la Alitalia ilitua katika ardhi ya Kenya huku maelfu ya Wakenya wakiwa wanapeperusha bendera za Kenya na Vatican na kuimba nyimbo mbalimbali, waliilaki ndege hiyo.
Milango ya ndege hiyo ilifunguliwa saa 10:50 na kuruhusu waandishi wa habari walioandamana na kiongozi huyo kuteremka na ilipofika saa 10:52 Papa Francis alitoka katika ndege na kupungia mkono maelfu ya Wakenya waliokuwa uwanjani hapo kabla ya kupokewa na Rais Kenyatta na mkewe Margaret.
Rais Uhuru alimtambulisha kwa viongozi mbalimbali wa Kenya wakiwa uwanjani hapo na miongoni mwao ni Gavana wa Jiji la Nairobi, Dk Evans Kidero na maaskofu wa Kanisa Katoliki. Papa Francis aliwasili Ikulu saa 11:40 na kupokelewa na mwenyeji wake kisha kupigiwa nyimbo za mataifa hayo mawili na kufuatiwa na mizinga 21 ya heshima kwa kiongozi huyo wa Vatican.
Papa pia alikagua gwaride la heshima lililoandaliwa kwa ajili yake katika Viwanja vya Ikulu. Mbali na kuzuru Kenya, pia atatembelea nchi za Uganda na Jamhuri ya Afrika ya Kati huku Papa akitarajiwa kueneza ujumbe wake wa amani, maridhiano, mashauriano na kuchochea juhudi za kuzima migawanyiko.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!