Tuesday, 10 November 2015
ONA UNYAMA HUU!
Kundi la vijana hao wakimtembeza Shakila mitaani huku akiwa mtupu.
Na Makongoro Oging’
DUNIA katili! Mrembo mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Shakila Kocho (21), mkazi wa Tabata- Kimanga jijini Dar amelazwa Wadi namba 24, Jengo la Mwaisela, Hospitali ya Taifa Muhimbili kufuatia majeraha yaliyotokana na kupigwa mawe na kuchomwa moto wa petroli kwa kisa cha tuhuma za kuwa kwenye mtandao wa wizi wa bodaboda.
Wakimshambulia kwa mawe.
WALIOTEKELEZA UKATILI
Msichana huyo alifanyiwa kitendo hicho hivi karibuni maeneo ya Buguruni Sukita, Dar na watu wanaodaiwa kuwa ni madereva wa bodaboda ambao ndiyo waliomtuhumu.
Taarifa zilizopatikana kwa mashuhuda zinadai kwamba, Shakila kabla ya kuchomwa moto alitembezwa mtupu mtaani huku watu wakimsonga na baadaye akapigwa mawe na fimbo halafu akamiminiwa petroli na kulipuliwa kwa kiberiti.
Shakila akiwa ameanguka.
MSOMALI ASAIDIA
Kwa mujibu wa mashuhuda hao, wakati Shakila akiwa chini kutetea roho yake huku akiungua moto, mwanaume mmoja mwenye asili ya Kisomali mwenye makazi yake maeneo hayo, alitokea na kupiga risasi juu kwa lengo la kuutawanya umati na kuwatisha watu hao kwa mbwa ndiyo ikawa salama ya Shakila.
…Akiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili
BASTOLA YATUMIKA
“Yule Msomali alitoka kwake nadhani ni baada ya kusikia kelele za auawe…auawe, alipomwona msichana yuko chini anatapatapa, alitoa bastola akafyatua risasi juu. Watu walikimbia kidogo, wakarudi, akamfungulia mbwa, ndipo watu wakatawanyika kabisa. Msomali akawasiliana na polisi Buguruni ambao walikuja kumchukua yule msichana akiwa ameumia sana na damu zikimtoka, wakamkimbiza Muhimbili,” kilisema chanzo.
UWAZI MUHIMBILI, MREMBO ATOA SIMULIZI
Ijumaa iliyopita, Uwazi lilimfuatilia majeruhi huyo Muhimbili ambapo lilimkuta akipatiwa matibabu. Hata hivyo, baadaye mrembo huyo alipata nafasi ya kusimulia mkasa mzima ulivyokuwa kama ifuatavyo:
“Nakumbuka ilikuwa mwishoni mwa mwezi wa kumi (Oktoba) kuja mwezi huu (Novemba). Siku hiyo mimi na mume wangu na mtoto wetu wa miaka mitatu, tulikuwa bado tumelala nyumbani Tabata Kimanga, akaja mtu, akabisha hodi. Mimi nikatoka kwenda kufungua mlango. Ghafla kundi la watu likaingia ndani wakiwa na magongo mikononi, wakaanza kumshambulia mume wangu bila kusema kisa.
“Kuona vile, mimi nikamchukua mwanangu ili tutoke nje. Wale watu wakakataa mimi kutoka na mtoto, hivyo nikatoka peke yangu. Kule nje nako nikakuta umati wa vijana, baadhi yao walikuwa wamekaa kwenye bodaboda.
“Wengine katika hao vijana niliwatambua. Walikuwa wamemshika kijana moja ambaye alitobolewa macho na damu zilikuwa zikimtoka kwa wingi. Mwenye nyumba tuliyopanga akatoka, alipoona hali ile akaniambia niende kutoa taarifa Kituo cha Polisi Tabata Shule.”
AKIMBIA, AINGIZWA MTEGONI KWA SIMU
“Niliondoka, mbele nikachukua bodaboda kwa lengo la kwenda polisi. Lakini nikaamua kwenda kwanza Buguruni Sokoni kwa shemeji yangu (kaka wa mumewe) kumpa taarifa.
“Nilimweleza shemeji hali ya nyumbani kisha nikamwomba simu yake ili nimpigie mume wangu kujua kinachoendelea na hali ya mtoto. Lakini simu hiyo ilipokelewa na mtu mwingine aliyejitambulisha kuwa ni msamaria mwema. Akasema mume wangu ana hali mbaya kutokana na majeraha ya kipigo, hivyo yupo naye kwenye zahanati iitwayo Afya Bora iliyopo Vingunguti.
“Mtu huyo alinitaka niende nikaongee na mume wangu. Nilimuaga shemeji, nikaondoka. Lakini cha ajabu, nilipofika kule zahanati nikaangukia mikononi mwa wale vijana.”
KILICHOMPATA
“Walinivamia na kuanza kunipiga huku wakisema mimi natumiwa na wezi wa bodaboda kama mteja na kuwapeleka kuuawa na kuporwa bodaboda. Niliwaambia si kweli, lakini hawakusikiliza utetezi wangu. Walinichukua hadi Buguruni Sukita.
“Kule walinivua nguo zote, nikabaki kama nilivyozaliwa kisha wakaanza kunitembeza uchi mitaani. Kwa kweli walinifanyia mambo ya kunidhalilisha sana kiasi kwamba mengine nashindwa kuyatamka.”
APIGWA KWA MAGONGO, MAWE NA MATOFALI
“Kunitembeza bila nguo hakukuwatosha, wakaanza kunipiga kwa magongo, mawe na matofali. Niliishiwa nguvu mpaka nikadondoka chini huku nikitokwa na damu nyingi. Bado wakaona haitoshi, wakaona wanimalizie kabisa, wakanimiminia petroli na kunilipua kwa kiberiti huku nikishuhudia ila sikuwa na nguvu ya kujinasua.
“Kule Sukita nilikuta watu wengine wawili wakiteketea kwa moto mpaka wakafariki dunia. Nimeambiwa katika watu wale, kumbe mmoja ni mume wangu.”
AMTAJA MSOMALI
“Ni Msomali mmoja ndiye aliyepita maeneo yale na kunizima moto kisha akapiga simu polisi. Sikujua kilichoendelea. Nilijitambua nikiwa hapa hospitali, nikaambiwa ni Muhimbili.”
AMZUNGUMZIA MTOTO WAKE
“Mpaka sasa sijui mtoto wangu yupo wapi. Na kama yupo nyumbani, yupo na nani!? Nakumbuka yeye alianza kulia mara tu alipomwona baba yake anasulubiwa kwa magongo.”
WITO WAKE KWA JESHI LA POLISI
“Naliomba jeshi la polisi kuwatafuta na kuwakamata wale wote waliohusika kunifanyia mimi unyama huu na kumuua mume wangu.”
WALIVYOSEMA WAENDESHA BODABODA
Uwazi lilipata nafasi ya kuzungumza na baadhi ya waendesha bodaboda wa maeneo ya Buguruni ambao walisema Shakila alituhumiwa kuwa mhusika mkuu anayetumiwa na wezi kukodisha usafiri huo kwenda eneo walipo wezi hao kisha kuporwa fedha na bodaboda, wakati mwingine hadi kuuawa.
Waliendelea kudai kuwa, mrembo huyo alishajulikana na watu wa bodaboda kwamba akikodisha pikipiki hairudi wala dereva kuonekana na wengine maiti zao kuokotwa mbali zikiwa na majeraha.
KAULI ZA WANANCHI
Baadhi ya wananchi walikilaani kitendo hicho cha kujichukulia sheria mkononi bila kuwafikisha watuhumiwa katika vyombo vya dola na wameitaka polisi kuwatafuta wahusika wote na wachukuliwe hatua za kisheria.
BAADHI YA WATUHUMIWA WADAKWA
Hata hivyo, habari kutoka Kituo cha Polisi Buguruni, Dar zinasema kuwa, vijana kadhaa wanaodaiwa kuhusika na tukio hilo wamekamatwa na bado polisi wanaendelea kuwatafuta wengine ili sheria ichukue mkondo wake.
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, SACP Lucas Mkondya alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na watuhumiwa saba wanashikiliwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment