MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi mkoani hapa leo inatarajiwa kutoa hukumu ya kesi ya jinai inayomkabili Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shehe Ponda Issa Ponda. Hukumu hiyo iliahirishwa kutolewa Oktoba 19, mwaka huu baada ya Hakimu Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Mary Moyo kushindwa kukamilisha kuiandika kutokana na matatizo ya kiafya yaliyokuwa yakimkabili.
Kutokana na kushindwa kutolewa kwa hukumu hiyo, Ponda ameendelea kukaa rumande hadi leo ambapo hatima yake itajulikana. Wakati akiahirisha kesi hiyo, Hakimu alisema, sheria inataka hukumu hiyo isomwe ndani ya siku 90 baada ya kukamilika kwa taratibu za kesi hiyo.
Alisema, kutokana na sababu zake za kiafya alishindwa kukamilisha kuandika hukumu hiyo na kutokana na sheria hiyo anayo mamlaka ya kuahirisha kwa vile atakuwa bado ndani ya siku 90 zilizotajwa kisheria.
Kutokana na sababu hizo, aliwafahamisha mawakili hao kuwa hukumu hiyo ameipanga kuitoa Novemba 18, mwaka huu kulingana na matakwa hayo ya kisheria. Ponda alifunguliwa kesi namba 128/2013 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Morogoro awali akikabiliwa na mashitaka matatu anayodaiwa kuyatenda Agosti 10, mwaka 2013 katika eneo la Kiwanja cha ndege Manispaa ya Morogoro.
Alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Agosti 19 mwaka 2013 kwa makosa hayo matatu na baadaye alifutiwa shitaka moja na kubakia mawili ambayo ni kutoa maneno yenye kuumiza imani za dini na kushawishi watu kutenda kosa.
No comments:
Post a Comment