Baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, leo yatakumbwa na bomoabomoa ya nyumba ambayo ujenzi wake umekiuka matumizi yaliyokusudiwa ikiwamo kujenga bila kibali, bila kufuata michoro ya mipango miji na matumizi ya ardhi.
Kazi hiyo inafanywa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni.
Maeneo yatakayobomolewa nyumba hizo kwa siku tatu mfululizo kuanzia leo hadi keshokutwa huu ni Mbezi Beach, Tegeta, Bunju, Mwenge na Kinondoni eneo la Biafra.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam jana na Msemaji wa wizara hiyo, Hassan Mabuye, wizara hiyo inakusudia kubomoa nyumba hizo zilizokiuka Sheria na taratibu za Ardhi.
“Maeneo yaliyotengwa mijini kwa matumizi ya umma ikiwa ni pamoja na maeneo ya wazi, njia za miundombinu na huduma nyinginezo za umma, mara kwa mara hutumiwa vibaya au kuvamiwa na waendelezaji binafsi hivyo kuukosesha umma manufaa yaliyokusudiwa. Nyumba hizo tutazibomoa,” alisisitiza Mabuye katika taarifa yake hiyo.
Taarifa hiyo ilirejea tamko namba 6.6.1 la Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, serikali inahakikisha kwamba maeneo yote ya mijini yaliyotengwa kwa shughuli za umma yanatumika kwa shughuli zilizokusudiwa na yanalindwa ili yasivamiwe.
“Tamko namba 8.2.1 la Sera ya Taifa ya Ardhi ya mwaka 1995, linasema serikali za mitaa zitawajibika kushirikiana na Wizara ya Ardhi kuhakikisha usimamizi mzuri wa ardhi katika maeneo yao,” ilisema taarifa hiyo.
Ilibainisha kuwa Sera ya Taifa ya Ardhi inaeleza sababu inayofanya Wizara kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni kuendesha kazi ya ubomoaji huo.
NIPASHE
No comments:
Post a Comment