Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema ulaji wa bidhaa za viwandani zilizotengenezwa kutoka kwa nyama husababisha saratani.
Ripoti hiyo inasema ulaji wa gramu 50 za nyama iliyopitia viwandani au kupitia shughuli yoyote ya kuifanya ikae muda mrefu bila kuharibika, huongeza hatari ya kuugua saratani ya utumbo mkubwa kwa asilimia 18.
Shirika hilo limesema pia ulaji wa nyama nyekundu “huenda husababisha saratani” lakini hakuna ushahidi wa kutosha.
WHO hata hivyo imesisitiza kwamba nyama pia huwa na manufaa yake.
Shirika la utafiti wa saratani la Cancer Research UK limesema matokeo ya utafiti huo wa WHO ni sababu ya kufanya watu kupunguza, na si kuacha kabisa kula nyama nyekundu na nyama iliyopitia viwandani.
Shirika hilo liliongeza pia kuwa kula mkate uliotiwa nyama mara kwa mara si vibaya.
Nyama iliyopitia viwandani ni nyama ambayo imefanyiwa shughuli Fulani kuongeza muda wake wa kukaa bila kuharibika au kuiongezea ladha, kwa mfano kwa kuipulizia moshi, kuikausha au kuongeza chumvi au kemikali za kurefusha muda wake wa kukaa bila kuharibika.
Mambo haya huenda ndiyo yanayoongeza hatari ya watu kuugua saratani. Kupika nyama kwa kiwango cha juu cha joto, au kuchoma nyama huenda kukasababisha kutokea kwa kemikali zinazosababisha saratani.
WHO imefikia uamuzi wa kutangaza kwamba nyama iliyopitia viwangani husababisha saratani baada ya kupokea ushauri kutoka kwa Shirika la Kimataifa la Utafiti kuhusu Saratani, ambacho hutathmini ushahidi wa kisayansi uliopo.
Shirika hilo sasa limeweka nyama iliyopitia viwandani kwenye kundi sawa na madini ya plutonium, sigara na pombe.
Hili hata hivyo, halimaanishi kwamba hatari ni sawa. Hatari ya nyama si sawa na ya uvutaji sigara.
Inakadiriwa kwamba watu 34,000 wanaofariki kila mwaka kutokana na saratani huenda waliugua kwa sababu ya kula chakula chenye nyama nyingi iliyopitia viwandani.
Idadi hii ni ndogo sana ikilinganishwa na watu milioni moja wanaofariki kutokana na saratani inayosababishwa na uvutaji sigara na 600,000 kutokana na saratani inayosababishwa na unywaji pombe.
Nyama nyekundu huwa na manufaa pia kwani husaidia kuupa mwili madini ya chuma, zinc na vitamini B12.
Hata hivyo WHO imesema kuna ushahidi mdogo kwamba gramu 100 za nyama nyekundu husababisha kuongezeka kwa hatari ya kuugua saratani kwa 17%.
No comments:
Post a Comment