Baadhi ya wapiga kura waliodaiwa kuwa wamefariki na kufutwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Zanzibar, wamejitokeza wakiwa hai na kutaka majina yao yarudishwe katika daftari hilo ili waweza kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu.
Wapiga kura hao wamejitokeza baada ya Tume ya Uchaguzi Zanzibar (Zec) kubandika majina ya wapiga kura katika vituo, huku ya baadhi ya wananchi yakiwa hayaonekani na wanapofatilia kuambiwa wamefariki wakati wapo hai.
Mmoja wa wananchi hao, Khamis Juma, Khamis Mkazi wa Mikarafuuni Wilaya ya Mgharibi (B) Unguja, alisema alipofutilia taarifa zake za uhamisho kutoka shehia ya Magogoni kwenda Mwanakwerekwe ameshangazwa kuambiwa amefariki wakati yupo hai.
Mbali na tatizo hilo, pia kumejitokeza matatizo kwenye maelezo ya baadhi ya wampiga kura kuwa tofauti na picha zao, hivyo kuwa katika hatari ya kupoteza sifa ya kupiga kura.
Miongoni mwa waliokumbana na mkasa huo ni Samir Suleiman Ally, mkazi wa Mtendeni, Zanzibar, ambaye maelezo katika shahada yake ni sahihi lakini picha siyo yake na kuwa katika hatari ya kutoshiriki uchaguzi huo.
Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa Chama cha Wananchi (Cuf), Omar Ali Shehe, alisema tangu kubandikwa majina ya wapiga kura wamepokea malalamiko mengi ya baadhi ya watu majina yao kutokuonekana kwenye Daftari la Wapiga Kura na wengine wakiambiwa wamekufa wakati wapo hai.
“Kuna watu wamefutwa katika Daftari la Wapiga Kura wakiambiwa wamefariki wakati wapo hai, wengine wameandikishwa na kupewa stakabadhi za kuandikishwa lakini wamekwama hadi sasa kupata shahada ya kuwa mpiga kura,” alidai Shehe.
Alisema wakati wa uchukuaji shahada za wapiga kura mwisho ilikuwa jana, idadi ya watu ambao hawajapewa shahada kwa sababu mbalimbali imekua ikiongezeka wakiwamo walioandikishwa na kupewa stakabadhi badala ya shahada za kuwa mpiga kura.
Shehe alisema kutokana na matatizo yanayoendelea kujitokeza, matumaini ya Zanzibar kuwa na uchaguzi huru na wa haki yameanza kupotea kwa kile alichoeleza idadi kubwa ya watu wamekwama kupata shahada za kupiga kura na wengine kufutwa kwa madai ya kufariki wakati wapo hai.
Hata hivyo, Msemaji wa Zec, Idrisa Haji Jecha na Mkurugenzi wa tume hiyo, Salum Kassim Ali, hawakupatikana ili kuzungumzia malalamiko hayo baada kupigiwa simu mara kadhaa jana na kuita kwa muda mrefu bila kupokelewa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment