Gari lililotumiwa na walinzi wao likiwa limetelekezwa.
Makongoro Oging’ na Haruni Sanchawa
Taarifa toka vyanzo vyetu makini vya habari vinadai kwamba zaidi ya shilingi bilioni 1.8 (1,800,000,000) zimeibwa na baadhi ya walinzi wa kampuni binafsi ya ulinzi ya G4S kisha kutoweka nazo kusikojulikana, Uwazi limegundua.
Habari zinadai kwamba, walinzi hao baada ya kufanya tukio hilo lililotokea Alhamisi ya wiki iliyopita walilitelekeza gari hilo maeneo ya Chuo cha Ualimu Duse kilichopo Chang’ombe, Dar na lilikutwa siku hiyohiyo saa mbili usiku.
Kamanda wa Mkoa wa Polisi Ilala, SACP Lucas Mkondya.
Kamanda wa Mkoa wa Polisi Ilala, SACP Lucas Mkondya (pichani) alipohojiwa na waandishi wetu alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema gari hilo lipo Kituo Kikuu cha Polisi, Dar (Central) kwa uchunguzi zaidi.
Kamanda Mkondya alisema kwamba taarifa ya kutoonekana kwa gari hilo katika mtandao wa kufuatilia ruti za magari ya kampuni hiyo sanjari na walinzi hao, ilitolewa polisi na Albert Shelukindo ambaye ni mkuu wa kitengo cha dharura kwenye kampuni hiyo.
“Baada ya kupata taarifa hiyo, msako mkali ulianza na kufanikisha kupatikana kwa gari hilo maeneo ya Chuo cha Ualimu cha Duse huku walinzi wake wakiwa wametoweka na fedha ambazo sisi kiasi chake hatujakijua mara moja.
“Ndani ya gari mlikutwa bunduki, sare za kazi na baadhi ya vielelezo. Inasemekana fedha hizo walizichukua kwenye mabenki mbalimbali, ikiwemo NBC makao makuu (Dar). Ilikuwa wazisambaze katika mashirika mbalimbali na ATM lakini hawakufanya hivyo,” alisema kamanda huyo.
Kamanda Mkondya aliendelea kusema kwamba, baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo wanashikiliwa kwa kuisaidia polisi.
Aliwataja wanaohojiwa kuwa ni pamoja na meneja na mkuu wa kitengo cha tahadhari wa kampuni hiyo. Pia alisema mameneja wa mabenki hayo nao watahojiwa kuhusiana na tukio hilo.
No comments:
Post a Comment