Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ikiendelea kutangaza matokeo ya urais yanayoonyesha kuwapo kwa mchuano mkali kati ya wagombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli na wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, muungano wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeibuka na kupinga matokeo hayo kwa kudai kuwa ‘yamechakachuliwa’.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, viongozi wakuu wa Ukawa, walisema wanayapinga matokeo hayo ya urais kwavile wamebaini kuwa ni batili kwani hayaendani na matokeo halisi waliyoyakusanya kutoka katika majimbo mbalimbali nchini.
Kadhalika, kutokana na hali hiyo, Chama Cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema) kimeitisha Kamati Kuu ya dharula leo kujadiliana ili kufahamu ni hatua gani watazichukua dhidi ya utangazaji huo wa matokeo yasiyoendana na uhalisia.
Mbali na Kamati Kuu ya Chadema, pia leo Kamati Kuu ya Ukawa itakutana kujadili na kutangaza uamuzi wao kutokana na kuwapo kwa hali hiyo.
Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, alisema katika matokeo ambayo Ukawa wameyakusanya kutoka sehemu mbalimbali, inaonnyesha kuwa mgombea wao, Lowassa, amepata kura nyingi tofauti na matokeo ambayo yamekuwa yakitangazwa na Nec.
Mbowe alisema wamebaini kuwa wapo watu maalum ambao wameandaliwa kwa kazi maalum ya ‘kuchakachua’ matokeo hayo kupitia mfumo mpya unaotumika kuyatangaza, ambao baadhi yao wametolewa nje ya nchi na wanafanya kazi hiyo katika hoteli mbalimbali nchini.
“Kama amabvyo tulikataa hapo awali kutokuwa na imani na mfumo wa kutangazia matokeo hayo, na kutokuwa na imani na NEC, sasa ni kweli imetokea… mfumo huo umechezewa na watu ambao wengine wametolewa nje ya nchi na wamesambaa katika hoteli mbalimbali nchini ili kufanya kazi hiyo,” alisema Mbowe.
“Hivi sasa inawezekana hata Jaji Damian Lubuva anatangaza matokeo ambayo hata hajui yametoka wapi, yamescaniwa, akapelekewa… yeye anatangaza tu. Na ndiyo maana walitumia Jeshi la Polisi kuvamia vituo vyetu vya kukusanyia matokeo na kuchukua vifaa vyetu ili tusikusanye matokeo, wakijua kwamba ndiyo watakuwa wametumaliza pasipo kufahamu kwamba zipo njia nyingine ambazo tunatumia kubaini matokeo ya kweli,” alisema Mbowe.
Kwa upande wake, Mwanasheria wa Chadema, Prof. Abdallah Safari, alitaja baadhi ya majimbo ambayo tayari yamechakachuliwa na kutangazwa na Nec kwamba ni yale yanayoonyesha kuwa mgombe urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Magufuli, ameongoza katika majimbo ya Tandahimba na Tunduma wakati ukweli ni kwamba kote huko ameachwa mbali na Lowassa.
Hadi kufikia juzi ambapo matokeo ya majimbo 27 yalishatangazwa, Magufuli alionekana akiongoza kwa kura 455,454 dhidi ya 308,240 za Lowassa.
Mwenyekiti mwenza wa Ukawa, James Mbatia, alisema NEC wamekuwa wakifanya hivyo kwa kujua kuwa matokeo ya urais huwa hayahojiwi mahakamani, lakini wao hawataa ha kuitafuta haki.
UBABE POLISI
Ukawa wamelalamikia pia ubabe unaofanywa na polisi katika majimbo ambayo vyama vyao vinaonekana kushinda baada ya maafisa wa NEC kuchelewesha matokeo na pindi wananchi wakitaka watangaziwe washindi, askari polisi huingilia kati kwa kuwapiga mabomu na kumwaga maji ya kuwasha kabla ‘uchakachuaji’ zaidi wa matokeo kufanywa na kuwapa ushindi Chama Cha Mapinduzi (CCM).
NIPASHE
1 comment:
Inawezekana kabixha kwan NEC haiko huru kabisa .n chama Tawala pia hawataki kukubali upinzan uchukue nchi ..nawahakikishia Tanzania itakuwa n aman iwapo ccm watatoka madarakan cc watanzania n wavumilivu tu maisha yetu hayaelewek ingawaje tunavyo vyanzo vingi vya kuwezapata hela
Post a Comment