Dar es Salaam. Wakiwa wamebakiza miezi michache kwenye mikataba yao, baadhi ya wachezaji wa kigeni wanaocheza Ligi Kuu kuwapo kwao nchini, kucheza soka ni bahati.
Baadhi yao wameandaliwa barua za kutemwa wakati wa usajili wa dirisha dogo.
Hatua ya timu hizo kuwatema nyota hao ambao baadhi yao waliingia nchini kwa mikwara inatokana na mchango mdogo walioutoa kwa timu zao mpaka sasa.
Nyota hao, licha ya mishahara mikubwa wanayolipwa na gharama nyinginezo ili kusajiliwa wamegeuka mzigo.
Wachezaji hao, baadhi yao wamekosa nafasi kwenye vikosi vya kwanza vya klabu zao na wengine kujikuta watazamaji baada ya nafasi zao kuchukuliwa na wazawa.
Wazawa, wameonyesha uwezo mkubwa, huku wageni hao wakishindwa kuonyesha ishara za kukua kwa viwango vyao kadri Ligi Kuu inavyosonga mbele.
Sababu za klabu zao kufikiria kuachana na wachezaji hao wa kigeni ni kupunguza gharama kubwa wanazotumia kuwahudumia, pamoja na kupata nafasi ya kuwaleta nchini wachezaji wengine, ambao pengine klabu hizo zinaamini kuwa wataongeza nguvu vikosi vyao.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwenye klabu mbalimbali umeonyesha kuwa wachezaji ambao huenda wakakumbwa na dhoruba ya kukatwa ni, Mnigeria Chidiebere Abasilim wa Coastal Union, Hamad Ndikumana (Stand United), Vincent Angban, Emiry Nimubona na Pape Ndaw, wote wa Simba na Andrey Coutinho na Vincent Bossou wa Yanga.
Ndikumana anayechezea Stand licha ya kushindwa kufurukuta mbele ya Hassan Dilunga na Erick Kayombo, pia amekuwa hana uhusiano mzuri na uongozi wa timu hiyo kutokana na masuala ya kimasilahi.
“Amekuwa akitanguliza fedha kuliko kuonyesha kiwango uwanjani. Tulimsajili tukiamini kuwa atatumia uzoefu wake kuisaidia timu badala yake amekuwa mzigo, tutaachana naye muda si mrefu,” alisema kiongozi mmoja wa Stand, ambaye hakupenda kutajwa jina.
Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha alikataa kuweka wazi ni mchezaji yupi atakayeondoka zaidi ya kusisitiza kumwacha mchezaji mmoja wa kigeni.
“Kuna mchezaji tunatarajia kumuuza, tayari kuna klabu moja iko Indonesia na nyingine Malyasia, zote zimeonyesha nia ya kumhitaji, ila hazijaleta barua rasmi zaidi ya mazungumzo ya simu.
“Tunasubiri barua rasmi ili kumweka wazi ni mchezaji yupi ambaye kama mpango huo utakubali ataondoka Yanga wakati wa dirisha dogo,” alisema Dk Tiboroha na kuongeza:
“Baada ya kumuuza, tutaongeza mchezaji mwingine wa kimataifa, lakini pia tumepanga kusajili nyota wapya wawili wazawa katika dirisha dogo.”
“Bossou amecheza mechi moja, lakini wengine wote wamepata nafasi hiyo, beki huyo kuna mechi ilikuwa acheze, lakini alikuwa majeruhi,” alisema Dk Tiboroha huku akisisitiza kuwa kiwango cha beki huyo ni kizuri.
Nayo Simba, imeamua kuanzisha mazungumzo ya washambuliaji Laudit Mavugo wa Burundi na Erisa Sserukamba wa Uganda kwa lengo la kuwasajili.
Usajili huo utafanyika wakati wa dirisha dogo, huku ikitajwa wachezaji watatu wa kigeni wanaotarajiwa kutemwa ni Simon Sserunkuma (Uganda), Pape N’daw (Senegal) , Emiry Nimubona (Burundi) au Angban (Ivory Coast).
No comments:
Post a Comment