Zikiwa zimesalia siku 13 kabla ya Uchaguzi Mkuu, baadhi ya wachambuzi wamesema unaonekana utakuwa wa kihistoria.
Idadi kubwa ya watu waliojiandikisha kupiga kura wanaokaridiwa kufikia milioni 24 ni historia tangu nchi ipate Uhuru mwaka 1961.
Baadhi ya madhehebu ya dini kuamua kufuta ibada zao siku ya Uchaguzi Mkuu na kujitokeza kwa watu wengi kwenye mikutano ya kampeni kunafanya tukio hilo liwe la kihistoria.
Mwamko wa wananchi katika kushiriki matukio mbalimbali ya mchakato huo, ushindani mkubwa baina ya wagombea wa urais, kitendo cha vigogo wengi kuhama vyama vyao vya zamani au kuachana na siasa na kuanzishwa kwa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vinatajwa kuwa chachu ya mabadiliko makubwa ya kiuchaguzi.
Wasomi, wananchi, wanaharakati na baadhi ya viongozi wa dini wanasema uchaguzi wa mwaka huu una hamasa kubwa ambayo haijawahi kutokea kiasi cha kuonyesha kuwa wananchi wameshatambua wajibu wao huku vijana wakitajwa kujiandikisha kwa wingi kuliko miaka ya nyuma.
Mhadhiri wa Idara ya Sayansi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Damian Shumbusho anasema kiwango cha ushindani mwaka huu ni kikubwa sana ukilinganisha na miaka ya nyuma, hivyo ni vigumu kutabiri mshindi kabla ya Oktoba 25.
“Uwezekano wa kutabiri mshindi kwa uchaguzi huu ni mdogo sana, kila mpiga kura anaamini mgombea wa urais anayemuunga mkono atashinda.
“Hata wapiga debe kwa wagombea hao wanawapa tu matumaini kuwa watashinda, lakini kiuhalisia wote hawajui mwelekeo halisi kwa kuwa wapo ndani ya chama ila watu wa nje wanaweza kuwa na majibu halisi,” alisema Shumbusho.
Uchaguzi huu ni wa tano tangu kurudishwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 na kufanyika uchaguzi wa kwanza mwaka 1995.
Katika kinyang’anyiro cha urais, ushindani mkali upo baina ya mgombea wa CCM, Dk John Magufuli na mgombea wa Chadema anayeungwa mkoni na Ukawa, Edward Lowassa.
Kutokana na hamasa ya wananchi katika uchaguzi huu, Shumbusho alisema hakuna shaka idadi ya watakaojitokeza kupiga kura itakuwa kubwa, isiyopungua asilimia 70 ya waliojiandikisha.
“Harakati za uchaguzi wa mwaka huu nchini hazina tofauti na zile za Kenya mwaka 2002 zilizoking’oa chama cha Kanu madarakani,” alisema Onesmo Ole Ngurumwa, Mratibu wa Wapiganiaji wa Haki za Binadamu.
“Unafanyika wakati wananchi wameamka, wameona miaka 54 ya utawala wa chama kimoja hauna tija kwa kuwa muda uliotumika kukaa madarakani na maendeleo haviendani, hivyo kudai mabadiliko ya kimfumo na kiutawala,” alisema.
Alisema Watanzania pia wameshuhudia vigogo wengi wakihama vyama vyao kama ilivyokuwa hivi karibuni kwa Mzee Kingunge (Ngombale-Mwiru).
“Vitendo hivyo vina nguvu sana katika uchaguzi kama unakumbuka hata Kenya akina Joseph Saitoti na Raila Odinga waliungana na Mwai Kibaki kuanzisha Narc, baada ya Rais Daniel Arap Moi kumteua Uhuru Kenyatta na Kibaki alishinda na kuiangusha Kanu,” alisema Ole Ngurumwa.
Uchaguzi wa mwaka huu umevunja historia kwa vigogo wengi wa kisiasa kuvihama vyama vyao wakiongozwa na waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliyetimkia Chadema baada ya kuituhumu CCM kuwa ilivunja taratibu wakati wa mchakato wa kumtafuta mgombea urais.
Katika kundi hilo la vigogo waliotoka CCM, pia yupo waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, mawaziri wawili, Makongoro Mahanga na Goodluck Ole Medeye na wenyeviti wa mikoa wa chama na wengineo.
Vivyo hivyo, upinzani ulipata pigo baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kujivua cheo hicho huku aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa akipumzika kufanya siasa za vyama.
Mratibu wa Umoja wa Wanawake Wanasiasa Tanzania (Ulingo) Dk Ave Maria Semakafu, pia alisema mchuano wa vyama na wagombea upo juu sana tofauti na miaka ya nyuma na mwamko miongoni mwa wananchi na vyama vya siasa umeongezeka kiasi cha kuonyesha elimu ya uraia imewafikia.
Alisema makundi mbalimbali ya kutetea wanawake, watoto, vijana na watu wenye ulemavu yamejitokeza kwa wingi na kuainisha masuala ambayo wanataka yapatiwe kipaumbele.
“Zamani ulikuwa unasikia chagua chama changu na kuahidi mambo mengi bila kuanisha utekelezaji, lakini mwaka huu wagombea wamejitahidi kueleza utekelezaji utakuwaje,” alisema Dk Semakafu.
Muungano wa Ukawa
Semakafu pia alisema jambo jingine linaloufanya uchaguzi kuwa wa kihistoria ni kitendo cha vyama vya upinzani vinne vya NLD, Chadema, NCCR-Mageuzi na CUF kuungana na kukubaliana kusimamisha mgombea mmoja wa urais na ngazi zote za chini.
Alieleza miaka ya nyuma walikuwa wanazungumza bila vitendo, ila mwaka huu wametekeleza licha ya kukumbana na changamoto za kutoelewana katika baadhi ya majimbo na kata.
Taasisi za dini na kupiga kura
Mwamko wa wananchi kushiriki katika uchaguzi umewalazimu viongozi wa makanisa mbalimbali nchini, kufikiria namna ya kuwawezesha waumini wao kupiga kura.
Mkuu wa Habari na Mawasiliano wa Jumuiya ya Kikrsitu Tanzania (CCT), Mchungaji John Kamoyo alisema wameona uchaguzi wa mwaka huu kuwa na hamasa kubwa, hivyo walitoa uhuru kwa maaskofu kuamua njia rafiki itakayowezesha wananchi kupata muda mzuri wa kupiga kura.
“Uchaguzi wa mwaka huu unaonyesha uelewa miongoni mwa Watanzania ni mkubwa katika haki zao na wengi wamejiandikisha kupiga kura.
Alisema ili kuhakikisha kila muumini katekeleza haki yake ya kikatiba, baadhi ya makanisa yameamua kufanya ibada siku ya Jumamosi badala ya Jumapili ambayo ni siku ya uchaguzi au kupunguza idadi za ibada na kufanywa asubuhi na mapema.
Jana, Mchungaji Huruma Nkone wa Kanisa la Victory Christian Centre (VCCT) alitangaza kuahirisha ibada ya Jumapili ya Oktoba 25 kuwapatia nafasi waumini wake kupiga kura.
“Jumapili hatutakuwa na ibada ili mpate nafasi ya kupiga kura, ibada yetu tutaifanya siku ya Jumamosi, misa ya kwanza itaanza saa tatu asubuhi kwa ibada ya Kiingereza na ile ya Kiswahili itaanza saa tano,” alisema Nkone.
Mtafiti Mwandamizi wa Taaisisi ya Utafiti wa Masuala ya Afrika iliyopo Uingereza (ARI), Nick Branson alisema uchaguzi wa mwaka unaonyesha mabadiliko makubwa katika nyanja mbalimbali hasa kitendo cha vijana wengi kujitokeza kuwania nafasi za ubunge.
Alisema iwapo Bunge litaendelea kulinda uhuru wake kutoka kwa Serikali na kutekeleza wajibu wake wa kuiwajibisha Serikali inayoonekana kuwa na nguvu sana bila shaka demokrasia itakua zaidi nchini.
Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Dickson Kikoti alisema uchaguzi wa mwaka huu una hamasa kutokana na kuwapo kwa sera zinazogusa maisha yao moja kwa moja kama masuala ya afya, elimu, na ajira.
“Siyo kwamba ni ngeni hizi sera hizo la hasha ila zimekua porojo kwa chama tawala kwa miaka nenda rudi na kwamba vyama vya upinzani vinaonekana mbadala wa CCM,” alisema Kikoti.
Nyongeza na Vicky Kimaro
MWANANCHI.
MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment