Rais mstaafu, Benjamin Mkapa, amempongeza Rais Jakaya Kikwete pamoja na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa kusimamia utekelezaji wa ujenzi wa Daraja la Kigamboni linalotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.
Mradi wa daraja hilo lenye urefu wa mita 680, unaogharimiwa kwa pamoja kati ya NSSF na Serikali kwa gharama ya Dola milioni 143.5 za Marekani (sawa na Sh. bilioni 248), ulipangwa kumalizika ndani ya miezi 36 tangu kuzinduliwa kwake Septemba, 2012.
Akizungumza baada ya kupokea taarifa ya kina kuhusiana na mradi huo jijini Dar es Salaam alipotembelea daraja hilo mwishoni mwa wiki kwa mwaliko maalum kutoka NSSF, Mkapa alisema uamuzi wa kutekeleza mradi huo ni wa kijasiri kwa kuwa unahusisha kiasi kikubwa cha rasilimali fedha na muda.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo, Meneja Miradi wa NSSF, Mhandisi John Msemo, alisema kwa sasa ujenzi wa daraja hilo umekamilika kwa asilimia 94 huku akibainisha kuwa zimebaki mita 25 ili kuunganisha kabisa daraja hilo.
“Awali, mradi ulipangwa ukamilike Januari, mwaka huu, lakini kutokana na changamoto zilizojitokeza, ujenzi utakamilika mwishoni mwa mwaka huu na daraja litaanza kutumika mapema Januari, mwakani,’’ alisema.
Kwa mujibu wa Mhandisi Msemo, wakati wa kusimika nguzo zinazoshikilia daraja hilo, ilibainika kuwa umbali wa mita 56 kutoka sakafu ya bahari kulikuwa na uwazi ambao ungeathiri daraja hilo.
Hata hivyo, alisema kukamilika kwa mradi huo kutazaa changamoto kadhaa ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi na serikali mapema zikiwamo suala la msongamano wa magari kwenye makutano ya barabara za Kilwa – Mandela, Nyerere - Mandela, Veta Chang’ombe - Kawawa pamoja na uduni wa barabara unganishi zikiwamo zile za Vijibweni - Mji Mwema pamoja na Gerezani - Ohio.
“Lakini pia faida kubwa zaidi ambayo kama taifa tumeipata kwenye mradi huu ni pamoja na suala la uzoefu wa kusimamia na kuendesha miradi ya namna hii ambapo wataalam wetu wengi wa ndani wameelimika kiasi cha kutosha kusimamia miradi ya namna hii…Kifupi kama taifa, tunao wataalam wa kusimamia ujenzi wa daraja la Dar es Salaam – Zanzibar muda ukifika,’’ alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, alitoa wito kwa wahandisi wa mradi huo kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo huku pia wakiangalia namna itakayomwezesha Rais Kikwete kufanya uzinduzi wa daraja hilo (Soft Opening) kabla hajamaliza muda wake.
Kwa upande wake pia, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau, mbali ya kumshukuru Mkapa kwa kuasisi mradi huo mwaka 2002, alisema daraja hilo likikamilika litainua uchumi wa eneo la Kigamboni na kuwa sehemu nzuri ya uwekezaji.
Hivyo aliwataka wananchi kulitumia kikamilifu kwa ajili ya maendeleo yao.
Mbali na daraja hilo, Mkapa pia alitembelea miradi mingine inayotekelezwa na mfuko huo ukiwamo ile ya ujenzi wa nyumba za makazi eneo la Kijichi na wa ‘Dege Eco Village,’ yote ikiwa eneo la Kigamboni.
No comments:
Post a Comment