Katika hali isiyokuwa ya kawaida watu watano wamefariki dunia papo hapo kwa kukatwa katwa mapanga kama wanyama katika kitongoji cha Kisesa kata ya Bugalama wilaya ya Maswa Mkoani Simiyu.
Watu hao ambao ni wa familia moja walifanyiwa unyama huo kwa kukatwa katwa mapanga sehemu ya shingoni, huku wahusika wa tukio hilo wakiwa hawajajulikana.
Akitoa taarifa mbele za waandishi wa habari Kamanda wa polisi Mkoani hapa Gemine Mushy alisema tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 9 ambapo Baba, Mama pamoja na watoto wao 3 ndiyo waliouawa.
Mushy aliwataja waliofanyiwa unyama huo kuwa George Charles (30) ambaye ni Baba wa familia, Siku John (23) Mama wa Familia na watoto wao ambao ni Mchambi George (7) Tuma George (5) pamoja na Amos George (Miezi 9) wote wasukuma wa kitongoji hicho.
Aidha Kamanda Mushy alieleza chanzo kuwa ni mgogoro wa ardhi kati ya marehemu (George) pamoja na Baba yake wa kambo ambaye alinunua kipande cha ardhi alikokuwa akiishi marehemu.
Aliongeza kuwa baada ya tukio hilo jeshi la polisi lilifanya msako na kuwakamata watuhumiwa 3 ambao aliwataja kuwa ni Migata Lusalago (50) Jihelya Migata (30), Solo Kengele (31) wote wasukuma wa kijiji cha Bugalama.
Kamanda mushy alieleza kuwa waliokamatwa ni Baba wa kambo wa Marehemu pamoja na watoto wake wawili ambao ilidaiwa kuwa wameweza kushiriki katika kutenda tukio hilo la kinyama.
Hata hivyo Mkuu huyo wa polisi alisema kuwa uchunguzi wa kina unaendelea kufanyika ili kuwapata wahusika zaidi wa tukio hilo, ambapo aliwataka wananchi kutoa ushirikiano katika kudhibiti uhalifu ususani mauaji yatokanayo na ukataji wa mapanga.
Chanzo-SIMIYU NEWS BLOG
No comments:
Post a Comment