Wednesday, 30 September 2015

KIPINDUPINDU CHAUA 36 JIJINI DAR



Dar es Salaam. Watu 36 wamefariki dunia kwa ugonjwa wa kipindupindu katika Jiji la Dar es Salaam tangu Agosti 15.
Manispaa ya Kinondoni inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watu waliokumbwa na kipindupindu kwa kuwa na wagonjwa 1,194; Ilala 996 na Temeke 71.


Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mussa Natty alisema jana kuwa idadi ya waliokufa kwa kipindupindu katika manispaa hiyo imefikia 17, huku kukiwa na wagonjwa wapya 15.
Natty alitoa takwimu hizo jana wakati akipokea vifaa na dawa kwa ajili ya wagonjwa zenye thamani ya Sh15 milioni kutoka Benki ya CRDB baada ya Mganga Mkuu wa manispaa hiyo, Dk. Aziz Msuya kuomba msaada.
Alisema manispaa hiyo imetumia Sh537 milioni kwa ajili ya matibabu ya wagonjwa, ikiwamo ununuzi wa vifaa na dawa kwa waliolazwa katika kambi maalum zilizopo Mburahati.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Dk Charles Kimei alisema benki yake imeguswa na idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.
“Kwa kutambua hali iliyopo Kinondoni, tumeamua kutoa vifaa tiba na dawa kwa ajili ya wagonjwa waliolazwa,” alisema Dk Kimei na kuongeza: “Kila mwaka CRDB hutenga asilimia moja ya faida yake kwa ajili ya kusaidia jamii na kwamba kupitia uzinduzi wa Huduma ya Wiki ya Wateja tumetoa msadaa huo.”
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Victorina Ludovick alisema hadi sasa watu 19 wamefariki dunia tangu ugonjwa huo ulipoingia katika wilaya hiyo.
“Leo (jana) wagonjwa wapya wapo 28 na waliolazwa katika kambi ni 43,” alisema.

No comments:

 

ADVERTISE WITH US

AFRICAN FASHION

PLACE YOUR ADS HERE!