Mgombea urais Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli amesema akiingia madarakani baada ya kushinda katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumapili ijayo atahakikisha anamaliza kero ya maji jijini Dar es Salaam na pia katika maeneo mengine yote nchini.
Magufuli aliyasema hayo kwa nyakati tofauti kwenye mikutano yake ya Kigamboni, Mbagala, Temeke, Ubungo na Kinondoni jijini Dar es Salaam jana.
Akieleza zaidi, alisema hivi sasa mahitaji ya maji jijini Dar es Salaam ni lita milioni 500 lakini yanayopatikana ni lita milioni 350, hali inayochangia kuwapo kwa uhaba wa maji katika baadhi ya maeneo jijini humo.
Hata hivyo, Magufuli alisema tatizo hilo la maji jijini Dar es Salaam litabaki kuwa historia ndani ya muda mfupi baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini ambao utakuwa ukizalisha lita milioni 780 kwa siku.
Alisema hivi sasa nchi inahitaji rais mkali ili mambo mengi yaliyokwama yaende sawa akitolea mfano wa mradi huo mkubwa wa maji ambao umekwama kutokana na mtu mmoja kufungua kesi mahakamani.
“Mradi ule ni mkubwa lakini kuna mtu kaipeleka serikali mahakamani watu wanakosa maji wanaugua kipindupindu na kufariki kwa kukosa maji safi na salama, sasa ngoja mimi Magufuli niingie Ikulu muone maana zimebaki siku nne tu,”
“Siwezi kuvumilia kuona kesi inacheleweshwa mahakamani wakati watanzania wanaendleea kufa kwa kukosa maji, hakyamungu ngoja niingie Ikulu nifanye kazi, kuna mambo mengine yanakera sana… mahakama inashindwaje kutoa uamuzi kwenye suala nyeti kama hili,” alihoji.
Aliwataka wananchi kuacha ushabiki wa vyama vya siasa na badala yake waangalie mtu kama yeye ambaye anaweza kuwaletea maendeleo.
MABADILIKO YA KWELI
Magufuli alisema Watanzania wasidanganyike na wanaoishutumu CCM kwamba haijafanya lolote tangu Uhuru kwani baadhi ya wanaoshutumu walikuwa na madaraka makubwa serikalini.
“Najua Watanzania mnataka mabadiliko ya kweli na mtu sahihi wa kuyaleta ni mimi, nafahamu hamna haja ya maamuzi magumu na mnataka mtu mwenye maamuzi makini kama mimi,” alisema Dk. Magufuli na kuongeza.
“Hata wizi na ujambazi wa kutumia silaha, kujinyonga ni maamuzi magumu, wapinzani wasiwadanganye kwamba mabadiliko yataletwa na kuzungusha mikono….nichagueni kwasababu kwangu mimi ni kazi tu,” alisema
Akiwa katika Jimbo la Kigamboni, Dk. Magufuli alisema anawapenda wananchi wa jimbo hilo na aliwataka kuwapuuza watu wanaomchonganisha nao.
Alisema watu hao wamekuwa wakieneza maneno ya uchochezi na uchonganishi kwa wakazi wa jimbo hilo kwa nia ya kumchafua lengo ikiwa ni kutafuta kura kwa ajili ya uchaguzi wa wiki ijayo.
Alisema yeye ni mtu safi na makini kwani angekuwa mpiga dili kama wengine angekuwa bilionea kwasababu amekaa serikalini muda mrefu huku akiongoza Wizara yenye matrilioni ya fedha.
AMRUSHIA KIJEMBE KINGUNGE
Bila kumtaja jina, Dk. Magufuli alisema anamshangaa mzee mmoja ambaye amezeekea serikalini lakini amegeuka na kuishutumu serikali kuwa haijafanya lolote tangu uhuru.
“Huyu mzee amezeekea serikalini lakini ameungana na wale waliokuwa washauri wa rais kwa muda mrefu na kuilaumu serikali...wamekaa madarakani muda mrefu lakini leo hii wamegeuka… kama hakuna lililofanyika wao walikuwa wanamshauri nini rais? alihoji Dk. Magufuli.
AWAFURAHIA VIJANA CHADEMA
Mgombea huyo alipofika Ubungo Mataa, karibu na kituo cha mabasi yaendayo mikoani alikuta umati mkubwa wa watu na wengine wakiimba ‘Lowassa, Lowassa’, huku wakiwa wamenyoosha vidole viwili juu.
Dk. Magufuli aliwapongeza wafuasi hao wa Chadema kwa kumpokea kwa wingi, huku akiwataka wamchague ili awalete maendeleo ya kweli kwani akiwa Rais hatabagua mtu kwa itikadi za vyama.
“Ukawa oyeee, Chadema oyeee, nawashukuru kwa kuja kunipokea kwa shamra shamra na naomba siku ya kupiga kura mnichague ili niwaletee maendeleo, Chadema ni wangu, Ukawa ni wangu, Cuf ni wangu na hata wasio na vyama ni wangu kwasababu maendeleo hayana chama,” alisema.
Dk. Magufuli alisema amefurahi kuona mji wa Dar es Salaam ukiwa umependeza kwa kupambwa kwa bendera za vyama mbalimbali vya siasa zikiwamo za CCM, Chadema, CCM na Cuf.
“Nimefurahi sana kuona bendera za kila chama tena mpya mpya, bendera za Chadema zinapendeza, bendera za CCM zinapendeza za Cuf zinapendeza na mimi kwasababu nitakuwa Rais mpya kwa Watanzania wote, nichagueni nilete mabadiliko ya kweli,” alisema Dk. Magufuli huku akishangiliwa na umati huo.
AELEZA CHANZO KIPINDUPINDU DAR
Dk. Magufuli alisema chanzo cha kuendelea kwa ugonjwa wa kipindupindu katika jiji la Dar es Salaam ni ukosefu wa maji uliokwamishwa na kesi iliyofunguliwa na matajiri waliogoma bomba la maji kutoka Mto Ruvu kupitishwa katika maeneo yao.
Alisema kitendo hicho kimesababisha mradi huo kukwama na kusabisha wakazi wa jiji hilo kukosa huduma muhimu ya maji salama na kuendelea kupoteza maisha kwa ugonjwa wa kipindupindu kutokana na kutumia maji yasiyo salama.
Dk. Magufuli aliyasema hayo alipokuwa kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika kwenye viwanja vya Biafra, Mnispaa ya Kinondoni jana.
Alisema kama yeye angekuwa Waziri wa Maji angejitoa mhanga kubomoa eneo hilo ili kupitisha boma la maji kunusuru wananchi wengi na kuugua na kufa kwa ugonjwa wa kipindupindu.
“ Ni bora mtu mmoja kufungwa kuliko wananchi wengi kuteseka kwa kosa la matajiri wachache, nikichaguliwa nitahakikisha suala hilo linamalizika mara moja,” alisema.
Alisema kama mradi huo ungekamilika ungetoa lita za maji milioni 780 na kutosheleza wakazi wote wa jiji la Dar es Salaam na kuepuka kipindupindu, lakini kutokana na ubinafsi wananchi wanaendelea kupoteza maisha.
UVCCM WADAI HUJUMA
KATIBU Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Shaka Hamdu Shaka, alidai umoja huo umebaini mpango unaoandaliwa na chama kimoja kumteka nyara mgombea urais wa chama kimoja cha upinzani, ili ionekane kuna njama za kumhujumu mgombea huyo kabla ya uchaguzi mkuu wa Jumapili.
Alisema mpango na mkakati huo unalenga pia kuipaka matope Tanzania ionekane mbele ya jumuiya ya kimataifa haiheshimu misingi ya demokrasia na inamhofia mgombea huyo.
Shaka alisema hayo katika mkutano wa kampeni wa Dk. Magufuli uliofanyika kwenye viwanja vya Biafra, wilaya ya Kinondoni jana.
Aidha, alidai kuna njama na mkakati wa chama hicho kuwavalisha vijana wake nguo za CCM na kumhujumu mgombea huyo wa urais kwa kulichoma moto gari analotumia ili kuiaminisha dunia kuwa anahujumiwa na serikali ya chama tawala na haiko tayari kwa matokeo.
AZZAN
Akiwasilisha kero za Hospitali ya Mwananyamala, mgombea ubunge Jimbo la Kinondoni, Idd Azan, alisema hospitali hiyo inakabiliwa na upungufu wa wodi za kulaza wagonjwa na wajawazito.
“Wodi hazitoshi hospitali inalaza wagonjwa kati ya 1,800 hadi 2,200 na pia watoto wanaozaliwa kwa siku ni kati ya 120 hadi 150, hivyo tunaomba utakapochaguliwa kuwa Rais majengo yaongezwe,” alisema.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment