Dk. John Magufuli, alizaliwa Oktoba 29, 1959 katika Wilaya ya Chato mkoani Geita. Jana wakati akitangazwa mshindi wa urais, pia alikuwa akisherehekea `Birthday’ yake.
“Siku hii ni kubwa na muhimu katika maisha yangu, sherehe yangu ya kuzaliwa na nimepata ridhaa ya kuwaongoza Watanzania katika nafasi ya Rais,” Dk. Magufuli aliandika katika ukurasa wake wa Twitter jana saa 10:32 jioni.
Kabla ya Dk. Magufuli kugombea urais, alikuwa ni mbunge wa Jimbo la Chato na Waziri wa Ujenzi.
ELIMU
Dk. Magufuli alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chato na masomo ya sekondari ya awali katika Seminari ya Katoke, Biharamulo.
Alimalizia kidato cha nne katika Shule ya Sekondari Lake jijini Mwanza. Kidato cha sita alimaliza katika Sekondari ya Mkwawa mkoani Iringa.
Dk. Magufuli ana shahada ya Umahiri wa Sayansi na Shahada ya Uzamivu ya Kemia, Stashahada ya Elimu ya Sayansi akibobea kwenye masomo ya Kemia na Hisabati katika Chuo cha Elimu Mkwawa mwaka 1982.
Aidha, Dk. Magufuli aliwahi kufundisha katika Shule ya Sekondari Sengerema miaka ya 1980 na ilikuwa ajira yake ya kwanza serikalini na kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Alipohitimu, Dk. Magufuli alianza kufanya kazi katika Kiwanda cha Nyanza Cooperative Union akiwa Mkemia na baadaye aliondoka hapo na kuwania ubunge. Aliteuliwa Naibu Waziri wa Ujenzi mwaka 1995 na kuanzia hapo, hajawahi kukaa nje ya Baraza la Mawaziri.
Wizara nyingine alizowahi kuziongoza ni Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
VYAMA VYA KITAALUMA
Mbali ya kuwa mwanasiasa, Dk. Magufuli pia ni mwanachama wa vyama vya kitaaluma kama Chama cha Wakemia Tanzania na Wataalam wa Hisabati Tanzania.
HODARI KUKARIRI TAKWIMU
Dk. Magufuli ana mahaba na namba. Si kwamba amesoma hisabati kama somo, lakini amekuwa akipenda masuala ya namba na moja ya alama yake kubwa ya kiutendaji ni uwezo wake mkubwa wa kuweka kumbukumbu kichwani wa takwimu mbalimbali kuhusu masuala anayoyafanyia kazi.
MACHAPISHO ALIYOANDIKA
Vile vile, Dk. Magufuli ameandika machapisho mbalimbali yakiwam: “A New Rate Equation for Solid State Decomposition and its Application to the Decomposition of Calcium Carbon Trioxide, The Control and Management of Heat as Challenge and Opportunity to Engineers, Funding for the EAC Road Network Project na The Potential of Anacardic Acid Self-Assembled Monolayer From Cashew Nut Shell Liquid As Corrosion Protection Coating (2009).
MBIO ZA KUWANIA URAIS
Dk. Magufuli alichukua fomu kimya kimya ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi ya urais Agosti 4, mwaka huu tofauti na wagombea wengine waliochukua fomu hizo kwa mbwembwe.
“Nilikwenda kimya kimya, nikachukua fomu kimya kimya na nikachaguliwa kimya kimya….kama kuna mtu ambaye nilimhonga hata senti wakati wa mchakato ndani ya CCM ajitokeze, mimi sina deni na hakuna mtu ambaye anaweza kusema alinisaidia,” hiyo ni kauli ambayo Dk. Magufuli alikuwa akiitoa mara kwa mara kwenye mikutano yake ya kampeni.
Mara baada ya mchakato wa kuwachuja watangaza nia kumalizika, Dk. Magufuli aliingia tano bora akiwa na wagombea wenzake, January Makamba, Amina Salum, Dk. Asha-Rose Migiro na Bernard Membe.
Katika mchujo wa mwisho kwenye Mkutano Mkuu wa CCM, Dk. Magufuli alijizolea kura 2,104 sawa na asilimia 87 za kura zote na hivyo kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama chake.
MKEWE
Mke wake anaitwa Janet Magufuli, ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Mbuyuni, shule aliyokuwa akifundisha mke wa Rais Jakaya Kikwete, Mama Salma.
No comments:
Post a Comment