Mgombea urais wa Tanzania kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, amepata mapokezi ya kifalme mjini hapa jana kabla ya kuuambia umati uliojitokeza kwenye mkutano wake kuwa umtafutie kura milioni 14 ili ajihakikishie ushindi.
Lowassa ambaye anaungwa mkono pia na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NLD, NCCR-Mageuzi na Chama cha Wananchi (CUF), aliwavutia maelfu ya watu katika mkutano huo wa kwanza wa kampeni kwenye jimbo lake la uchaguzi tangu alipoihama CCM na kuteuliwa kuwa mgombea urais kupitia Ukawa.
Kabla ya kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka huu utakaofanyika Oktoba 25, Lowassa amekuwa mbunge wa Monduli kwa miaka 20.
Akizungumza kwenye mkutano mkubwa alioufanya katika Kata ya Mto wa Mbu, kwenye viwanja vya Barafu, Lowassa alisema watu wengi wakiwamo wa Monduli wameamua kuingia katika basi lake la mabadiliko lakini wale ambao bado hawajaamua kufanya hivyo, wahurumiwe na kuelimishwa.
“Yule ambaye hataki kuingia basi langu la safari ya mabadiliko, tumhurumie,” alisema.
Alikuwa akimzungumzia mgombea ubunge wa jimbo hilo kupitia CCM, Namelok Sokoine, ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Waziri Mkuu wakati za serikali ya awamu ya kwanza, marehemu Edward Moringe Sokoine.
Alisema suala la Namelok linatarajiwa kuzungumzwa kesho (leo) na wagombea udiwani ili kupata muafaka na kama akikataa, basi wao watajipanga.
“Kwanza Sumaye (Waziri Mkuu mstaafu, Frederick), umenisaidia sana suala la ubunge. Nimekuwa mbunge wa jimbo hili miaka 20, sasa hivi kumekuwa na maneno maneno kuhusu suala hilo, naomba mniachie kesho (leo) tuzungumze na madiwani na Namelok ili tufikie muafaka,” alisema.
Lowassa alisema anaomba kila mwana-Monduli amtafutie kura popote pale Tanzania ili apate kura zaidi ya milioni 14 zitakazomuwezesha kuwa mshindi wa kiti cha urais, Oktoba 25 mwaka huu.
“Nipeni kura za kutosha, nasikia hao jamaa (CCM) ni hatari sana wa kuiba kura,” alisema.
Awali, Sumaye akimkaribisha Lowassa, alisema kuna baadhi ya watu bado wanashangaa kuona wao wametoka CCM na kujiunga na vyama vya upinzani.
“Lakini naomba msishangae, kwa sababu Tanzania haijapata manufaa yoyote kwa CCM kuwa madarakani. Kwa hiyo tumetoka CCM ili kuwapa Watanzania fursa nyingine ya kuongoza nchi.
“Tunaomba mumchague Lowassa kuwa rais wa awamu ya tano, na pia mbunge na madiwani watoke Ukawa.
“Najua tunaye hapa Namelok, hatuna ugomvi naye kwa sababu amechagua kuwa kwenye basi ambalo halina matairi. Huyo ni mdogo wetu, tutazungumza naye kumweleza aachane na kadi ya kijani… tutaongea na Namelok atoke huko na kuungana na Lowassa. Huyo ni mdogo wetu," alisema.
Alisema ana matumaini kwamba Lowassa atashinda kwa asilimia 80 katika uchaguzi mkuu unaokuja.
Aliiponda CCM kwa kudai kuwa ni chama kinacholea rushwa na ufisadi huku akihoji kuhusu kushamiri kwa biashara ya meno ya tembo, ununuzi wa meli mbovu, ununuzi wa mabehewa feki na ufisadi katika Wizara ya Ujenzi aliodai kuwa Lowassa akiwa rais atakabiliwa na mzigo mkubwa wa kulipa deni la zaidi ya Sh. bilioni 900. Hata hivyo, hakufafanua kiundani juu ya madai hayo.
Katika hatua nyingine, Lowassa alisema ataendelea kutekeleza ahadi zake zilizobaki kwenye Jimbo la Monduli na akawaomba kama watakuwa na tatizo lolote wasisite kumueleza.
“Nataka Monduli ibaki na amani ile ile tuliyokuwa nayo… tupendane na kuheshimiana, tumefanya mambo mengi sana ya maendeleo kama vile kutoa huduma mbalimbali za kijamii.
“Sitakuwa tena mbunge, naomba madiwani waniheshimu na watu wengine pia. Pale ambapo mtakwama naomba mje kwangu,” alisema na kuongeza, “naomba Monduli ibaki kuwa Monduli, nataka Monduli ibaki na amani ile ile iliyokuwa nayo.”
Baada ya kuzungumza na wananchi hao, Lowassa, alishuka jukwaani kabla ya kumpigia debe mgombea ubunge wa jimbo hilo, Julius Kalanga, huku baadhi ya watu wakitaka kujua kuhusu Namelok.
Hatua hiyo ilimlazimu Lowassa kupanda tena jukwaani pamoja na wagombea na kuwaombea kura mmoja baada ya mwingine.
SOURCE: NIPASHE
No comments:
Post a Comment